Serikali yaombwa kuwawezesha vijana mitaji

0
772

Susan Uhinga, MuhezaSerikali imeombwa kuwaandaa vijana kwa kuwapa elimu ya ujasiriamali, mafunzo kwa vitendo pamoja na mikopo ili waweze kujikwamua kiuchumi na kushiriki kuchangia pato la taifa.

Hayo yameelezwa na Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, Zawadi Nyambo, wakati akisoma risala iliyoandaliwa na vijana jumuiya hiyo mkoani hapa kwa mgeni rasmi Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalah Ulega wakati wa kufunga kambi ya vijana wa CCM iliyokuwa wilayani Muheza.

Amesema Vijana wengi wamekuwa na changamoto ya kutoandaliwa vyema ili kuweza kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali jambo linalopelekea vijana kuzurula mitaani huku wakilalamika ukosefu wa ajira.

“Vijana wakiandaliwa vizuri hasa katika mafunzo na vitendo pamoja na mitaji hatutasikia vilio vya ajira vijana watajiajiri kwa ujuzi walionao huku mikopo ikiwasaidia kwenye suala la mtaji,” amesema.

Amesema kambi ambayo ilikuwa na vijana zaidi ya 200 kwa muda wa siku 14 wakifundishwa masuala mbalimbali ya uzalendo imefungwa rasmi leo.

Kwa upande wake Ulega, amesema Serikali itahakikisha inawatumia vijana katika maeneo mengi ya miradi ya serikali pamoja na kuwapatia elimu juu ya masuala ya ujasiriamali na kuwapatia mikopo kupitia Halmashauri zao.

“Serikali imeliona hili na ni jambo la kutiliwa mfano kwa vijana hawa ambao wameweza kujitolea nguvu kazi katika ujenzi wa hospitali hii ya wilaya, niahidi hii itakuwa chachu katika maeneo mengine ya Tanzania,” amesema Ulega.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here