31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yalipa madeni ya bilioni 85.2/-

ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

SERIKALI imelipa madeni ya ndani yanayofikia Sh bilioni 85.72, tangu kuanza kwa robo ya kwanza ya mwaka mpya wa kifedha wa Serikali, Julai hadi Septemba mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuendeleza nidhamu ya kulipa madeni kwa watumishi wa umma na watoa huduma wengine serikalini.

“Kwa hiyo, kati ya Julai na Septemba 2019, Sh bilioni 85.72 zimeshatolewa ikiwemo Sh bilioni 50 za madai ya pensheni, Sh bilioni 22 madai ya watumishi wa umma, ikiwemo kiinua mgongo kwa wastaafu 3,019 na malimbikizo ya mishahara kwa watumishi 1,435.

“Lakini pia, katika mkakati huo, tayari Sh bilioni 10.24 zimelipa watoa huduma mbalimbali, kati ya hizo, zaidi ya Sh bilioni mbili kwa ajili ya wakandarasi na wahandisi washauri,” alisema.

Alisema pamoja na kulipa kiasi hicho cha madeni, Serikali inaendelea na mkakati huo kwa wote wanaoidai kutoka ndani na nje ya nchi, hivyo kwa wakati huu, wote wanaoidai wanastahili kujivunia kuhusu madai yao kwa kuwa Serikali imeamua kufuta mzigo huo.

Dk. Abbasi alisema hatua nyingine nzuri iliyofikiwa na Serikali ni kuuza korosho zote zilizokuwa kwenye maghala, baada ya kuingilia kati mfumo kandamizi wa mauzo ya zao hilo uliokuwa ukiwaumiza wakulima kwa kushusha bei na kuamua kununua korosho yao yote na kwa bei nzuri.

Alisema hadi kufikia Septemba 30, mwaka huu, Serikali imeshauza korosho zote kwa wanunuzi 21 wa ndani na nje ya nchi, na tani zaidi ya 4,595.90 zitabanguliwa nchini.

Dk. Abbasi alisema zaidi ya tani 211, 587 zimeshauzwa nje ya nchi na kati ya hizo, 107,187 zitasafirishwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam na 104,400 zitapitia Bandari ya Mtwara.

“Hadi sasa zaidi ya tani 98,860 zimekwishachukuliwa na kusafirishwa nje ya nchi kupitia Bandari za Mtwara na Dar es Salaam, hii ni sawa na asilimia 41 ya korosho zote na zoezi la kuondoa korosho iliyobaki kupelekwa kwa wanunuzi linatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 21, mwaka huu,” alisema.

Alisema Serikali iliamua kutumia zaidi ya Sh bilioni 720 kununua korosho yote, karibu tani 225,105 (ikijumuisha tani 2,139 zilizoingia kwenye maghala awali) kwa kutoa bei nzuri ya hadi Sh 3,300 badala ya Sh 1,500 kwa kilo waliyokuwa walaliwe wakulima.

Akizungumzia miradi mikubwa, Dk. Abbasi alisema Serikali inaendelea na kasi yake ya utekelezaji wa miradi mikubwa yenye manufaa kwa taifa na wananchi kwa kiwango kinachoridhisha.

Alisema mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao ni wa kihistoria kwa ajili ya kufua umeme wa maji,  utakaozalisha megawati 2,115 utakaogharimu Sh trilioni 6.5, unaendelea vizuri na tayari Serikali imeshatoa Sh trilioni 1. 

Dk. Abbas alisema miradi mingine inayoendelea kwa kasi ni ile ya maji kwa maeneo yote nchini, ambayo inagusa moja kwa moja maisha ya watu.

Alisema mwaka 2015, Serikali ya awamu ya tano iliweka lengo la kufikisha maji vijijini kwa asilimia 85 na mijini asilimia 95 ifikapo mwaka 2020 na sasa wataalamu wako kazini kuhakikisha lengo hilo linafikiwa ifikapo mwakani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles