33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yakosa bil 23/- mgodi wa Tancoal

Mwandishi wetu -Mbinga

MGODI wa makaa ya mawe wa Ngaka (Tancoal) ambao Serikali ni mbia, uliopo Kijiji cha Ngaka, Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, umeshindwa kulipa kodi ya Serikali zaidi ya Sh bilioni 23 tangu mwaka 2011.

Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme, wakati akitoa taarifa hiyo mgodini hapo baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki, kuutembelea.

Mndeme alisema kuwa waziri huyo alimweleza kuwa wawekezaji hao hawaonyeshi dalili njema ya uwekezaji wao kwani ni muda mrefu tangu Serikali itoe maelekezo kwao juu ya kulipa deni hilo, lakini hadi sasa wako kimya.

Alisema hata kwenye halmashauri mgodi huo umeshindwa kulipa fedha unazotakiwa kulipa na kwamba awali walikuwa wanalipa kodi kulingana na thamani ya madini badala ya kulipa kulingana na bei ya soko.

Mndeme alisema katika hatua ya kusikitisha, mgodi huo umeanza kupunguza wafanyakazi wakati moja ya faida za uwekezaji mahali popote ni ajira kwa wazawa na kwamba mkoa kwa kushirikiana na Wizara ya Madini unaendelea kufuatilia utaratibu wa ulipaji deni hilo.

“Awali wawekezaji hawa walidai wanashindwa kulipa deni hilo kutokana na kujiendesha bila faida, lakini cha kushangaza bado wanaendelea na kazi. Kama hawapati faida yoyote si wangekuwa wameondoka?” alisema Mndeme.

Akizungumzia suala hilo, Waziri Kairuki aliwataka wawekezaji kutokiuka sheria na taratibu za nchi na kuutaka uongozi wa mgodi huo kuwasilisha mpango wao wa malipo ya deni husika Wizara ya Madini ili kuondokana na migogoro isiyokuwa ya lazima.

Alisema amefadhaishwa na tatizo hilo kwani ukuaji wa uchumi wa nchi unategemea ukusanyaji wa kodi na kwamba kulipa kodi si hiari, ni matakwa ya kisheria.

“Lengo la Serikali si kukwamisha wawekezaji, bali ni kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kuondoa vikwazo, lakini na wawekezaji wana jukumu la kutimiza wajibu wao kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi.

 “Viongozi wote na watumishi wa Serikali wana deni kubwa la kuhakikisha sekta binafsi inasonga mbele kwani ndiyo mwajiri wao kama ambavyo Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli anavyosisitiza,” alisema Kairuki.

Kaimu Meneja wa mgodi huo, Edward Mwanga, alikiri kuwa kampuni yao inadaiwa na kwa sasa uongozi unajipanga kuangalia ni namna gani watalilipa deni hilo na kukanusha taarifa ya wao kupunguza wafanyakazi na kwamba ndiyo kwanza wamezisikia kwa mkuu wa mkoa.

Kairuki yuko kwenye ziara ya mikoa mitatu akianza na Ruvuma kwa kutembelea na kukagua viwanda, mashamba na migodi ya makaa ya mawe iliyopo mkoani hapa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles