28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yahaha kukwamua fedha zilizofichwa Uswisi

Frederick Werema
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI inatafuta msaada kutoka nchini Uswisi ili kufanikisha zoezi la kuchunguza mali na fedha za Serikali zilizoporwa na kufichwa katika benki mbalimbali za nje ya nchi.

Hatua hii ya Serikali inakuja ikiwa ni miaka miwili tangu Bunge liitake Serikali kuchukua hatua dhidi ya suala hilo.

Hayo yamebainishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, ambapo alisema Serikali inafanya kazi na Kituo cha Kimataifa cha Urejeshaji Mali (ICAR) chenye makao makuu nchini Uswisi kuchunguza kesi kadhaa za ufisadi, hongo na rushwa.

“Hatuwezi kuanika majina ya watu kwa sababu kufanya hivyo ni kukwaza haki zao. Pili, iwapo tutaamua kuwataja, itakuaje iwapo tuhuma dhidi yao si za kweli? Na tatu, iwapo tutafichua majina yao, tutavuruga ushahidi wetu wenyewe,” alisema.

Mwaka 2012, Kamati ya Bunge iliyochunguza suala hilo iliitaka Serikali ichunguze ufisadi katika sekta ya umma na kuwabainisha wale ambao wameficha fedha katika akaunti za kigeni.

Pamoja na kelele za umma wakati taasisi ya Thomson Reuters Foundation iliporipoti suala hilo mwaka jana kuhusu uwapo wa akaunti za siri nchini Uswisi, kuliibuka jaribio la Bunge kutunga sheria itakayowabana wanasiasa wa Tanzania kuanika mali zao na kuweka ukomo wa akaunti zao za nje hata hivyo lilishindikana.

Wakati huo huo, kiwango cha fedha  ambazo Watanzania wameweka katika akaunti za Uswisi kimeendelea kupanda.

Kiwango hicho kilipanda kwa asilimia 42 kufikia Dola za Marekani milioni 304.2 mwaka 2013, kutoka dola milioni 213.4 mwaka 2012, kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu ya Uswisi.

Uswisi inaonekana kuwa kimbilio la matajiri kuweka fedha zao kutokana na uimara wa sarafu yake, unafuu wa kodi na utamaduni wa usiri katika benki za nchi hizo.

Taasisi ya Kimataifa ya Kukabiliana na Ufisadi (GFI) yenye makao makuu mjini Washington, Marekani ambayo huchunguza mtiririko wa fedha haramu, ilikadiria kuwa dola bilioni 4.5 zilitoroshwa kutoka Tanzania kipindi cha muongo mmoja uliopita.

Aidha, ilisema kiwango cha utoroshaji kwa mwaka 2011 kilifikia dola milioni 817, zikiwa ni takwimu za karibuni zaidi kupatikana kutoka dola milioni 551 mwaka 2002.

Hizo ni fedha pekee zilizopotezwa kwa njia ya kifisadi katika utumishi wa umma.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mahesabu ya Umma, Zitto Kabwe, alisema Oktoba mwaka jana alibainisha kuwa taifa linapoteza karibu dola bilioni 1.25 kwa mwaka katika mapato ya bajeti ikiwa sawa na asilimia tano ya pato lake la ndani, kupitia ukwepaji kodi za kampuni (corporate tax), rushwa, fedha ambazo zinahitajika kwa ajili ya huduma za afya, elimu na miundombinu.

ICAR husaidia maofisa kutoka nchi zinazoendelea kubainisha fedha za wizi, kushikilia na kurejesha mali zilizotokana na rushwa, fedha haramu na uhalifu mwingine kama huo.

Hata hivyo, taasisi hiyo haikuweka wazi iwapo inafanya kazi na Serikali ya Tanzania kushughulikia fedha zilizofichwa ng’ambo.

“Tunatoa msaada wa kiufundi kwa mashirika wakala wa sheria katika nchi mbalimbali duniani kupitia mafunzo, msaada unaohusiana na kesi, kuwa kiunganishi na mifumo ya mahakama ya kigeni pale inapobidi,” alisema Mkurugenzi wa ICAR, Gretta Zinkernagel kwa njia ya barua pepe.

Kituo hicho ni sehemu ya Taasisi ya Utawala Bora ya Basel, ambayo inaongozwa na Mark Pieth, anayeheshimika kwa kazi zake hasa ufanikishaji wa mkataba wa kimataifa dhidi ya rushwa duniani ujulikanao kama Mkataba wa Kupambana na Rushwa. Mkataba huo ulifikiwa wakati akiongoza Kitengo cha Kupambana na Rushwa katika Shirikisho la Maendeleo na Ushirikiano wa Kiuchumi (OECD).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles