33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yabariki Tanesco kuzikatia umeme taasisi zake

Susan Uhinga, Handeni



Serikali imesema Shirika la Umeme nchini (Tanesco), liendelee kukata umeme kwa wateja sugu wanaodaiwa malimbikizo ya Ankara zao za hata kama ni taasisi nyeti za serikali.

Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani ameyasema hayo kutokana na maombi maalumu yaliyotolewa na Mkuu wa Gereza la Handeni Miraj Katumbili na Meneja wa Mradi wa Maji wa HTM, Yohana Mgaza, waliotaka umeme usikatwe katika ofisi zao na wizara wakati zikitafuta ufumbuzi wa kulipa malimbikizo ya madeni yao.

Mrakibu Mwandamizi wa jeshi la Magereza SSP Katumbili, alisema mara nyingi umeme unapokatwa katika gereza hilo wanakuwa na wakati mgumu kutokana na aina ya watu wanaofungwa kwa makosa mbalimbali, hivyo wangeomba wasikatiwe.

Kwa upande wake Mgaza, alisema mradi wao wa maji wa HTM licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali, wanakiri kwamba Tanesco wanawadai zaidi ya Sh milioni 900 ambazo Wizara ya Maji imeanza kulipa lakini wamekuwa wakikatiwa umeme mara kwa mara.

“Mheshimiwa Waziri sisi ni wateja wakubwa wa Tanesco, tunawahudumia wananchi kwa maana tunatoa huduma, ni kweli tunadaiwa zaidi ya Sh milioni 900, wizara yetu imejitahidi kulipa kiasi cha Sh milioni 500 lakini bado tunakatiwa umeme wananchi hawapati maji,” amesema Mgaza.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe, akichangia suala hilo alisema anasikitishwa na Ofisi ya Tanesco Mkoa wa Tanga, namna wanavyoshindwa kukaa pamoja kutafuta suluhisho la kudumu la kutatua tatizo hilo ambalo kimsingi kwa vile wizara imeanza kulipa linazungumzika.

“Wizara ilishaanza kuonesha jitihada za kumaliza deni lakini wanakata umeme na wananchi wanakosa huduma hii muhimu, nimeongea na ofisi ya mkoa kumaliza tatizo hili, nimelalamika kwenye kikao ch RCC nikitaka wakutane walimalize, lakini hadi leo Tanesco hawataki kukaa pamoja,” amesema Mkuu huyo wa Wilaya.

Akifafanua hilo Dk. Kalemani aliwapongeza kwa kuonesha jitihada za kulipa lakini akasisitiza madeni hayo lazima yalipwe kwa kuwa Shirika hilo na lenyewe limekuwa na madeni mbalimbali ya zaidi ya Sh bilioni 700 huku lenyewe likidai kwa wateja wake kiasi cha Sh bilioni 200.

“Ni kweli tunajua wananchi wanaumia lakini mnapolipa Ankara hizi inasaidia kuliwezesha shirika kuwasaidia wananchi kwa kuwasambazia nishati ya umeme,” amesema Waziri na kumwagiza Meneja wa Tanesco Mkoa wa Tanga, Julius Sabu, kuwafuata viongozi wa HTM kumaliza suala lao mapema iwezekanavyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles