29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali ya Lebanon yaanguka

BEIRUT, LEBANON

WAZIRI Mkuu wa Lebanon, Saad Hariri amejiuzulu na hivyo kusababisha serikali kuanguka kutokana na  maandamano ya nchi nzima.

Katika maandamano hayo  yaliyodumu kwa zaidi ya wiki wananchi wanaipinga Serikali. 

Waandamanaji wamesema hatua hiyo haitoshi wanataka mabadiliko ya mfumo mzima wa kisiasa.

Tangazo la kujiuzulu Hariri kupitia televisheni, lilipokelewa kwa shangwe na waandamanaji ambao wamekuwa wakikusanyika tangu Oktoba 17. 

Hairri amesema amechukua uamuzi huo ili kukidhi matakwa ya raia walio wengi wanaotaka mabadiliko.

Kujizulu kwa Hariri ni ushindi kwa walioandamana, lakini Bunge litakabiliwa na kazi kubwa ya kuunda serikali mpya.

Mamia walikusanyika katika mji wa kaskazini wa Tripoli – ngome ya waziri mkuu wa madhehebu ya Sunni – na vile vile mji wa kusini wa Sidoni, inakotokea familia yake.

Waandamanaji wamesisitiza juu ya mabadiliko ya mfumo mzima wa serikali inayotawala kwa mgawanyiko wa kimadhehebu, huku wakisherehekea mwanzo wa utambulisho wa uraia wa kitaifa. 

Mmoja wa waandamanaji hao, Ayman Sharouf anasema bado hawajaridhika. 

“Kimsingi, tumeshinda sehemu tu ya ‘vita’, ikiwa tunaweza kusema hivyo. Tunahitaji mabadiliko, tumeanza na Serikali, lakini mabadiliko makubwa yatakuwa ya mfumo mzima. 

“Tutabaki kukaa hapa, ili kusema kwamba tunahitaji zaidi ya kile kilichotokea leo, tunahitaji mabadiliko ya mfumo mzima wa Lebanon, ” amesema Sharouf.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo alitoa wito kwa viongozi wa kisiasa wa Lebanon haraka kuunda serikali mpya. 

Pompeo amewaambia kuwa maandamano ya amani na umoja wa kitaifa kwa siku 13 zilizopita yametuma ujumbe wa wazi. 

“Watu wa Lebanon wanataka serikali inayofaa na nzuri, mageuzi ya uchumi, na kukomesha rushwa” alisisitiza.

Viongozi wa dunia wawatahadharisha wanasiasa Lebanon.

Wakati Ufaransa, mmoja wa washirika wa karibu wa Hariri na mshirika muhimu wa Lebanon katika mpango wa msaada wa kiutu wa dola bilioni 11, imeeleza hofu yake ya kwamba kujiuzulu kwa Hariri huenda ikaufanya mgogoro huo kuwa mbaya zaidi.

Ingawa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Lebanon Raya al-Hassan amesema kuondoka kwa Hariri ni muhimu sana ili kulinda utulivu.

Hariri wiki iliyopita alitangaza mageuzi ya kiuchumi ambayo yanalenga kufufua uchumi ambao umekaribia kuanguka kwa miezi kadhaa sasa, lakini hatua hiyo ilishindwa kumaliza hasira hizo za mitaani.

Viongozi wa kisiasa wa Lebanon wameonekana kushtushwa, wakati huo huo wakijaribu kuwaonyesha huruma waandamanaji wanaodai mabadiliko, pamoja na kuonya dhidi ya misukosuko itakayojitokeza iwapo taifa hilo litakabiliwa na ombwe la kisiasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles