25.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali ya JPM inavyowaza miaka mitano ijayo (4)

JUMA  lililopita niliendelea na uchambuzi wa Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wa miaka mitano, nikachambua sura yote ya tano. Niliahidi kuwa leo tena nitaendelea na uchambuzi huo nikijielekeza katika sura mbili za mwisho, sura ya sita na sura ya saba ambazo kwa pamoja zinazungumzia mkakati wa utekelezaji na mwisho ni mkakati wa tathimini na ufuatiliaji wa Serikali kuhusu mpango huo.

Sura ya Sita ni moja ya sehemu muhimu ya mpango huo wa Maendeleo wa Pili wa Taifa wa miaka mitamo ambayo inaainisha Mkakati wa Utekelezaji.

Sura hii ina vipengele 9 vikijumuisha utangulizi, changamoto za msingi katika ufanisi wa utekelezaji, mabadiliko yatakayofanywa na Serikali wakati wa utekelezaji, mabadiliko mahususi kwa ajili ya miradi ya kipaumbele, urasimishaji wa mabadiliko yenyewe, ushiriki wa ufanisi wa Serikali au dola, ugatuzi wa madaraka na mfumo wa maendeleo ya kiuchumi kwenye ngazi za chini, pamoja na muundo wa utekelezaji.

Tayari katika mfululizo wa makala za uchambuzi huu nimeshaeleza udhaifu na changamoto zinazoukabili mpango huu wa Maendeleo ya Taifa. Kwa maoni yangu mpango bado haujaweza kuonesha ni namna gani kama Taifa tunaweza kutimiza ndoto ya kuwa Taifa la viwanda.

Kuwa Taifa la viwanda unahitaji umeme wa kutosha na wa uhakika, bado kama Taifa katika eneo hili tunasuasua na hatuna uhakika wa umeme, jambo linalofanya uzalishaji katika viwanda vilivyopo uwe na gharama kubwa ambazo zote anabebeshwa mlaji wa mwisho wa bidhaa kutoka kwenye viwanda hivyo.

Tulitarajia, mkakati wa utekelezaji useme ni kwa namna gani suala la umeme litashughulikiwa ili kuhakikisha umeme unakuwa wa uhakika, umeme unapatikana vijijini kama ishara ya kuondoa umasikini kwa wananchi wa kawaida. Mpango umeainisha changamoto moja kuwa katika utekelezaji ambayo haitoshi kutokana na changamoto za utekelezaji wa mpango huo kuwa nyingi kama hii ya ukosefu wa umeme wa uhakika.

Serikali katika mpango huu wazo lao kuhusu changamoto wameainisha kuwa na uwezo mdogo wa kitaasisi katika kufanikisha mpango na kutafuta vyanzo vya mapato vya kutosha ili kuufanikisha mpango. Pia Serikali imebainisha kuwa kuna tatizo la utawala bora ambalo linaweza kuwa kizuizi cha kufanikisha mpango huu.

Nakubaliana na haya mawazo ya Serikali kuhusu uwezo mdogo wa kitaasisi kusimamia na kuongeza mapato ya kugharimia mpango, isipokuwa changamoto hizi pekee hazitoshi kuonesha kuwa mpango unaweza usifanikiwe.

Katika changamoto ya uwezo wa kitaasisi na utawala bora, Serikali imenyumbulisha matatizo saba ambayo kwa pamoja yanatoa sura halisi ni nini Serikali inakiita uwezo mdogo wa kitaasisi na ufanisi hafifu wa utawala bora.

Matatizo hayo ni pamoja na idhaifu wa sera kutowiana, athari za rushwa, udhaifu katika kupanga vipaumbele, uwezo mdogo wa kutafuta rasilimali, kukosekana kwa ugatuzi wa madaraka kwa baadhi ya sehemu na kushindwa kushusha vipaumbele vya Taifa katika ngazi za chini, udhaifu wa mfumo wa ufuatiliaji na tathimini pamoja na kushindwa kufanya uamuzi kwa wakati.

Pamoja na hayo, nilitarajia kuona maelezo ya Serikali ndani ya mpango huo ikisema ni mbinu zipi zitatumika kukabiliana na changamoto hizo za uwezo mdogo wa kitaasisi na ufanisi duni katika utawala bora. M

pango badala ya kuainisha mbinu umetaja masuala kwa ujumla ujumla tu, kuwa utekelezaji utaangalia namna ya kuondoa udhaifu bila kusema namna hizo ni zipi ili wadau na Serikali yenyewe ijipime endapo mbinu hizo ni mwafaka au la? Hii ndio mikakati, mbinu zikikosekana basi kunakuwa hakuna mkakati wa utekelezaji zaidi ya maelezo tu. Huu nao ni udhaifu mkubwa ambao moja kwa moja unatoa taswira ya kushindwa kwa mpango huu kabla utekelezaji wake haujaanza, hii ni hatari kwa ustawi wa Taifa.

Serikali ya Awamu ya Tano tayari imeshaanza kuukanyaga na kutouzingatia mpango huu jambo ambalo linaashiria mpango mzima kutofanikiwa. Ukisoma mikakati ya utekelezaji katika ushiriki wa Serikali, (ukurasa wa 84) Serikali imepanga kuwekeza katika demokrasia.

Sehemu  ya mkakati wake unasema kwa “investing in the electoral process and expand the freedom of expression, transparency and access to information” yaani ikimaanisha kuwekeza katika mchakato wa uchaguzi, kupanua uhuru wa kujieleza, uwazi na kupatikana kwa taarifa.

Serikali imeshindwa kuwekeza katika uwazi wa Bunge kwa kuipatia TBC bilioni 4 ili waweze kurusha “live” matangazo ya Bunge, uko wapi uwazi wa Serikali ya Awamu ya Tano? Serikali imeendelea kuitumia Sheria ya Makosa ya Mtandao (Cyber Crime Act) ambapo vijana kadhaa wamefunguliwa mashitaka mahakamani kutokana na kunyimwa uhuru wa kujieleza kupitia mitandao ya kijamii.

Bado Serikali imeshindwa kuhakikisha Muswada wa kupata habari unatungwa kuwa sheria bora. Hii ni mifano michache ambayo inaonesha matendo ya Serikali ya Awamu ya Tano kukinzana na huu mpango wa Maendeleo wa miaka mitano.

Kwa upande mwingine sura ya saba ndio ya mwisho katika mpango huu na imeanisha maeneo matano. Eneo la kwanza ni utangulizi, muundo wa tathmini na ufuatiliaji, mkakati wa tathmini na ufuatiliaji, mambo ambayo yanadhaniwa kuibuka wakati wa ufuatiliaji na tathimini na mwisho ni jeduwali la matokeo ya mpango.

Sura hii ya saba na ya mwisho ni ya kitalaamu zaidi, inajaribu kuonesha mbinu za ufuatiliaji na tathimini ambazo Serikali itazitumia.

Licha ya wizara, idara na wakala wa Serikali na mamlaka za Serikali za Mitaa kuwa na mifumo ya tathmini na ufuatiaji imeonekana kuwa hakuna mfumo mmoja wa kitaifa wa ufuatiliaji na tathimini na imependekezwa mfumo huo uundwe. Kwa kuwa mpango huu uliandaliwa na wataalamu wa Serikali, moja ya jambo kubwa linalodhaniwa kuibuka wakati wa ufuatiliaji na tathimini ni uwepo wa utashi wa kisiasa katika utekelezaji wa mpango mzima.

Yapo masuala mengine manne yanayodhaniwa kuibuka wakati wa kazi ya  tathmini na ufuatiliaji ikiwamo uwezo na uamuzi wa Serikali kutenga bajeti ya kutosha na kutoa fedha zitakazowezesha kazi yote ya tathmini na ufuatiliaji kufanyika kwa ufanisi na weledi unaotarajiwa.

Nimalizie uchambuzi wangu kwa moja ya nukuu za Mwalimu wangu wa masuala ya mipango, akisema kuwa “Mpango kwenye makaratasi, unakuwa ni mpango tu na utaendelea kubakia kuwa mpango mpaka utekelezaji wake utakapoanza”. Nakubaliana na  mawazo ya Mwalimu wangu kuwa pamoja na udhaifu mkubwa nilioubaini katika uchambuzi wangu wa mpango huu, kwa kuwa ndio mpango pekee, sharti utekelezwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles