23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali kuyaunganisha mashirika, taasisi za umma

Na NORA DAMIAN, DAR ES SALAAM

Msajili wa Hazina, Athuman Mbuttuka, amesema baadhi ya mashirika na taasisi za umma yataendelea kuunganishwa kuongeza ubora na ufanisi.

Hadi sasa kuna mashirika na taasisi za serikali 235 na makampuni 36 ambayo serikali ina hisa chache.

Akizungumza jana wakati wa uwekaji saini mikataba ya utendaji kazi kwa mashirika na taasisi 80, alisema wanaendelea kufanya tathmini za utendaji kazi wa mashirika 53.

“Tayari matokeo yameanza kuonekana na hata hatua zilizochukuliwa na mheshimiwa rais hivi karibuni za kuvunja baadhi ya bodi zinatokana na tathmini yetu.

“Si lazima kuzifuta (akimaanisha taasisi) zingine zitaunganishwa kuongeza ubora na ufanisi na tayari tumeanza kufanya hivyo kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii,” alisema Mbuttuka.

Alisema taasisi na mashirika 80 yaliyosaini mkataba huo yatafanyiwa tathmini ya utendaji kazi mwakani na kuzitaka bodi kuwajibika kwa kuweka malengo na shabaha kwani ndio kigezo kitakachotumika kupima ufanisi wao.

Kwa mujibu wa Msajili huyo, mkataba huo umeweka mkazo katika maeneo manne ambayo ni kuimarisha utawala bora, usimamizi wa raslimali fedha na utendaji, usimamizi wa watumishi na huduma kwa wateja.

Zoezi hilo linafanya idadi ya taasisi ambazo msajili wa hazina amesaini nazo makubaliano kufikia 185 tangu aanze utaratibu huo mwaka 2014/2015.

Awali Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk. Khatib Kazungu, aliyataka mashirika ya umma kujiendesha kwa faida badala ya kutegemea ruzuku za serikali kwa asilimia 100.

Alisema zoezi la uwekaji saini linafuatia waraka wa Katibu Mkuu Kiongozi wa Julai 13 mwaka huu ambaye alielekeza taasisi zote za umma na idara za serikali kuingia mikataba ya utendaji kazi.

Hata hivyo alisema baadhi ya taasisi bado hazizingatii matumizi bora ya fedha za umma na kusababisha kuwa na gharama kubwa za uendeshaji na kuikosesha serikali mapato.

“Tunazo taarifa za matumizi mabaya ya fedha kwa baadhi ya taasisi kama kulipana posho zisizo za lazima ambazo hazizingatii miongozo inayotolewa na serikali.

“Ni muhimu kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha kwa kuzingatia sheria na utawala bora,” alisema Dk. Kazungu.

Alizitaka taasisi hizo kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kutoanzisha miradi isiyokuwa na tija ili fedha zitakazookolewa zielekezwe katika miradi ya maendeleo na kuchangia mfuko mkuu wa hazina.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles