SERIKALI KULETA BIMA YA AFYA KWA KIFURUSHI

0
806

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, amesema Serikali ipo katika mkakati wa kuanzisha bima ya afya ya kifurushi kumwezesha mwananchi kujihudumia kadiri ya uwezo wake.

Amesema hiyo ni kwa sababu bima ya afya iliyopo sasa si rafiki kwa wananchi wengi, hali inayofanya baadhi yao, hususan familia duni, kushindwa kujiunga na huduma hizo muhimu za matibabu.

Kauli hiyo aliitoa juzi Dar es Salaam, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Kigamboni, ikiwa siku ya mwisho  ya kuhitimisha ziara yake ya kukagua shughuli za maendeleo jimboni kwake.

Dk. Ngugulile ambaye pa ni Mbunge wa Kigamboni, alisema Serikali ya Awamu ya Tano imetenga bajeti kubwa ya afya kuliko wakati wowote kwa lengo la kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na uhakika wa matibabu mazuri na salama.

“Kama ilivyo mitandao ya simu, na katika bima ya afya tutakuja na vifurushi tofauti tofauti na hapa kila mwananchi atajihudumia kulingana na uwezo wake, lengo letu ni kumfikia kila mmoja,” alisema Dk. Ndugulile.

Akizungumzia vifaa vya kujifungulia kwa wajawazito, alisema Serikali imegharamia vifaa vyote kwa wanaokwenda hospitali kujifungua na vitagawiwa bure vikiwa kwenye mabegi maalumu yenye nembo ya MSD.

Akitoa ufafanuzi wa malalamiko ya wananchi kuhusu kuzuiwa kwa miili ya wanaofariki katika hospitali za Serikali, Dk. Ndugulile alipiga marufuku kwa hospitali zote kuzuia miili ya marehemu ambayo ndugu zao wameshindwa kugharamia gharama za kuitunza.

Aliwataka ndugu wenye matatizo kuwasiliana na uongozi wa hospitali ili miili hiyo kuruhusiwa kwa utaratibu mzuri.

“Jukumu la Wizara ya Afya ni kuhakikisha wananchi wanapata matibabu ya uhakika na pale inapotokea ndugu wameshindwa kulipia gharama za maiti, ni vema wakafuata utaratibu wa kusaidiwa na hili lifanyike kwa kufuata utaratibu,” alisema Dk. Ndugulile.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here