29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

 ‘SERIKALI ITOE MSAMAHA KODI TAULO ZA KIKE’

Na Aziza Masoud-Dar es Salaam


SERIKALI imeombwa kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni zinazoingiza na kusambaza taulo za kike, ili kuwasaidia wasichana kununua bidhaa hiyo kwa bei ya chini.

Akizungumza jijini jana wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuchangisha fedha za kununua taulo kwa ajili ya wanafunzi wasiopungua 1,500 wa shule za sekondari, Mkurugenzi wa Shirika la  Haki za Wanawake (HAWA), Joyce Kiria, alisema wasichana waliopo  shuleni wanapofika siku za kupata hedhi hulazimika kutumia taulo zisizo na ubora.

Kutokana na hali hiyo alisema wengi hujikuta wakipata maambukizi ya magonjwa huku wengine wakidhalilika kutokana na bidhaa hiyo kuuzwa kwa bei  ya juu kati ya Sh 2,500 mpaka Sh 5,000.

“Serikali ichukue jukumu la kuangalia kwa jicho la tatu suala la pedi (taulo za kike), ikiwezekana zitolewe hata kwa msamaha wa kodi ili zipatikane kwa bei  rahisi, maana wasichana wanadhalilika kwakukosa fedha za kununulia na hili ni suala la kimaumbile ambalo hawawezi kuyazuia,” alisema Joyce.

Alisema kuna baadhi ya watoto wa kike  wanashindwa kwenda shule wanapokuwa katika siku zao kwa sababu ya kukosa taulo na shule kukosa mazingira mazuri yakujihifadhi.

Akizungumzia kuhusu kampeni hiyo ambayo wanashirikiana na kituo cha runinga cha EATV, alisisitiza ugawaji wa taulo hizo za kike utawalenga zaidi wanafunzi wa shule za sekondari wenye  mahitaji ambao watapatikana baada ya kushirikisha mashirika mbalimbali wanayofanya utafiti kuhusu masuala hayo ili kujua maeneo yenye mahitaji.

Kilele chake itakuwa siku ya wanawake duniani Machi nane ya kila mwaka.

Kwa upande wa Ofisa Masoko wa EATV, Brendasia Kileo, alisema kampeni hiyo imelenga kuwasaidia wanafunzi ambapo takwimu zinaonyesha  wanafunzi wa kike hushindwa kuhudhuria masomo kwa siku 60 mpaka 70 kutokana na kukosa pedi.

“Hali hiyo husababisha watoto wa kike  kutofanya vizuri katika masomo, pia watoto huatarisha afya zao kwakutumia matambara kujisitiri wakati wa hedhi, kupitia kampeni hii ambayo itafikia kilele Mei nane, tutagawa taulo kwa wanafunzi wenye uhitaji,” alisema Kileo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles