27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

‘Serikali ipunguze masharti kwa walimu kutoka nje’

NA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM

SERIKALI imeombwa kupunguza masharti ya vibali vya walimu wa kigeni   kwa kuwa yamekuwa yakisababisha wenye shule binafsi kutoza ada kubwa kufidia gharama hizo ambazo ni zaidi ya Sh milioni saba.

Akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyuo na Shule Binafsi Tanzania (TAMONGSCO), Mzinde Mzava, alisema endapo Serikali itapunguza masharti itawasaidia kuwapata walimu kwa gharama nafuu na gharama za ada zitapungua.

“Tunamuomba waziri mwenye dhamana ya elimu, Profesa Joyce Ndalichako na timu yake, wafikirie hili la vibali vya walimu wageni kutoka nje kwa sababu  itatusaidia hata sisi kuwapata walimu wenye fani mbalimbali na kupunguza gharama za ada,”alisema Mzava.

Alisema wanalazimika kutafuta walimu kutoka nje kwa kuwa   hawana mgao wa walimu wanaotoka kwenye vyuo mbalimbali vya serikali   nchini.

“Hapa nchini kuna upungufu wa walimu wa sayansi  27,000 hivyo hata huko shule za serikali nako wana upungufu wa walimu…endapo serikali itapunguza masharti sote tutanufaika katika hilo,” alisema Mzava.

Pia alisema Serikali imekuwa na changamoto ya uhaba wa walimu wa shule za watoto wadogo wenye stashahada hivyo wao hulazimika kuagiza walimu kutoka nchi kama Kenya ambako kuna walimu wengi wa aina hiyo.

“Kwa hapa Tanzania walimu wa watoto wadogo ambao wanafika hadi chuo kikuu wameanza mwaka jana kuhitimu, hivyo inatulazimu nasi kuagiza nje ya nchi ili tupate elimu bora yenye kukidhi matakwa ya soko la dunia,” alisema Mzava.

Naye Makamu Mwenyekiti wa TAMONGSCO, Emmanuel Rwegenyeza, alisema elimu bora ni lazima igharamiwe kwa vile ina ushindani mkubwa katika soko la ajira.

Rwegenyeza alisema upo mchakato na serikali wa kupata ada elekezi na baada ya hapo nao watatoa msimamo wao.

“ Tunaendelea na mchakato wa pamoja na serikali…tunategemea serikali itapanga ada ya kuanzia na mwisho ni shilingi ngapi kwa shule binafsi na ndipo sisi tukapotoa msimamo wetu kama tunaridhika nayo au la…,”alisema Rwegenyeza.

Alisema shule hizo hazipo kwa ajili ya kuwaumiza wananchi kwa kutoza ada kubwa lakini kinachoangaliwa  ni gharama za uendeshaji na ubora wa elimu inayotolewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles