Serikali ipige marufuku wanafunzi kushiriki mikesha ya Mwenge

0
865

Na ELIYA MBONEA, ARUSHA

Taarifa za kulawitiwa kwa wanafunzi 17 wa shule za sekondari Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wakati wa mkesha wa mbio za Mwenge wa Uhuru zimezua taharuki kwa wazazi.

Ni jambo la kushangaza na kusikitisha sherehe za mkesha huo kuwa chanzo cha watoto hao kufanyiwa ukatili huo.

Naweza kukiri hapa kupitia maandishi yangu kwamba nimeshiriki baadhi ya misafara ya kukimbiza Mwenge kimkoa na kuona namna wananchi katika kijiji au eneo husika ambako huwa unalala jinsi wanavyokuwa huru nyakati za usiku.

Ukifanikiwa kupita eneo ulipolala Mwenge wa Uhuru si ajabu kukuta vitu kama mipira ya kiume (kondom), zilizotumika zikiwa zimezagaa hovyo ama vichochoroni au maeneo ya wazi.

Sasa basi, kwa mazingira hayo tu madogo ambayo binafsi nimewahi kuyashuhudia ni wazi kwamba vitendo vya kulawitiwa wanafunzi au watoto ni rahisi kufanywa na wenye nia ovu wanaotumia mkesha huo kutimiza malengo yao.

Wazo langu katika tukio hili la kulawitiwa wanafunzi naamini sasa litaamsha hisia au mtazamo tofauti kuhusu mikesha ya Mwenge wa Uhuru na ushiriki wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Kwamba umefika wakati sasa wa kupiga marufuku ushiriki wa wanafunzi katika mikesha ya Mwenge kwani umeonekana kuwa kichocheo cha kufanyika vitendo vya ukatili kwa watoto waliopo shuleni.

Na kwa vile tayari mamlaka za Serikali zimeitaarifu jamii kuwa wapo baadhi ya watu wanaoshikiliwa kutokana na tuhuma hizo, sheria zichukue mkondo wake ikiwa ni pamoja na kufanya uchunguzi wa kina katika tukio hilo.

Si uchunguzi tu bali waende mbele zaidi kuwafuatilia watoto waliofanyiwa vitendo hivyo ili kubaini ukweli zaidi wa jambo hilo na kupima afya zao kama wamepata maambukizi ya Ukimwi au magonjwa mengine ya zinaa.

Vyombo vya dola vihakikishe walioshiriki wote wanachukuliwa hatua na kufikishwa mahakamani.

Nasisitiza haya kwa kutambua kwamba kesi za aina hii zimekuwa na changamoto kubwa ya ushahidi kutokana na kuvurugika kwa mazingira ya ushahidi hasa wazazi kutaka masuala yaishie ngazi ya kifamilia.

Ni imani yangu Serikali ya Mkoa wa Kilimanjaro itasimamia jambo hilo na kutoa fundisho kwa watu wengine wenye tabia za kutumia sherehe na mikesha ya Mwenge kuharibu ndoto za watoto, hasa wa kike.

 

Mwisho.

 

 

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here