27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI IANGALIE UPYA MUDA WA KUFUNGA SHOO USIKU

SERIKALI ilikataza muziki kupigwa usiku. Ilitoa sababu kadhaa. Zote zilikuwa na maana. Kumbi nyingi za starehe zimejengwa kati kati ya makazi ya watu.

Kupiga muziki usiku mnene ni kuleta bugdha kwa wakazi hasa wale ambao wanakuwa wamelala, wagonjwa, watoto na wazee. Nakubaliana na hilo ila pamoja na ukweli huo kuna mambo kadhaa ambayo serikali kupitia idara zake inabidi kuyatafakari upya.

Kwanza, inabidi kwa pamoja tukubali kuwa muziki hasa wa Dansi unapigwa karibu kila siku na huwa ni mida ya usiku. Wanamuziki wa Dansi wanategemea kupiga muziki mara tatu ama nne kwa wiki ili waweze kuendesha maisha yao.

Katika hili bila shaka sote tunakubaliana na ukweli huo ukweli huo, kukataza muziki kupigwa usiku maana yake unazuia ajira za hawa wanamuziki. Hivyo kupelekea familia na wategemezi wao wawe katika hali ngumu.

Pili, tukubali siyo chaguo na wanamuziki kupiga muziki katika kumbi ambazo hazina vizuio sauti kutoka nje ( Sound Proof). Ila wanalazimika kufanya hivyo kutokana na mazingira na aina ya kumbi zilizopo Tanzania.

Kwa namna hiyo, serikali inapaswa kuona haja ya kushirikiana na wanamuziki ili kujribu kutatua tatizo hilo.

Kuna wajibu serikali inapaswa kuuchukua kwa ajili ya kuwasaidia hawa wanamuziki. Wamiliki wa kumbi za muziki wana uwezo kuzitumia kumbi hizo kwa matumizi mengine na maisha yakaendelea.

Vipi kwa hawa wanamuziki ambao kwao kwenda katika kumbi hizo usiku kupiga nyimbo ndiyo msingi wa kuendesha maisha yao?

Nimekutana na wanamuziki wengi wa Dansi wakilia hali ngumu. Wanadai sasa ile mirija halisi ya kuwaingizia vipato vyao halali kwa mujibu wa sheria za nchi ‘imefungwa’. Wala hawakosei. Ni kweli kabisa.

Kwa namna fulani serikali kukataza kupiga muziki usiku bila kushauriana nao kuangalia watawasaidia vipi, ni kama kuwakatili.

Wakati huu tukitafakari namna ya kuurudisha muziki wa Dansi katika hadhi na sifa zake, tufikiri pia namna ya kuwasaidia wanamuziki hawa kujikwamua katika lindi hili la umasikini uliokithiri kwa sababu ya ‘kuzuiwa’ kufanya shughuli zao za muziki kama ilivyo zoeleka.

Wanamuziki hawa hawawezi kuwa wabunifu kama wakiwa wanakabiliwa na njaa. Inabidi tutafute mbinu za kuwafanya waendelee kufanya kazi yao kwa ufanisi ili wajiingizie vipato nasi tuweze kupata tungo nzuri zenye kusisimua kama ilivyowahi kuwa zamani.

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ndiyo, mlezi wa sanaa na wasanii. Wizara hii haitakiwi kuwacha wanamuziki wakibaki kama yatima wakati wana chombo cha kuwasaidia.

Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (Chamudata) washirikiane na  Muheshimiwa Mwakyembe ili wajue namna gani wanaweza kuwasaidia wanamuziki hawa wanaokosa mapato kisa kumepigwa marufuku muziki kupigwa usiku.

Pia ikumbukwe kuna faida kubwa sana juu ya hawa watu kutafutiwa fursa ya kupiga muziki wao kama ilivyokuwa awali. Miongoni mwa faida hizo ni kuongezeka kwa shughuli za kuwaingizia watu kipato.

Tukumbuke, watu wanapokwenda katika muziki, wengine hutumia taxi, bodaboda na bajaji. Hivyo kuna msisimko mkubwa sana wa kiuchumi kama hawa watu wakitafutiwa namna yao bora ya kupiga muziki.

Naamini serikali hii sikivu chini ya wizara ya mchapakazi Mwakyembe itafanya jambo kuwasaidia wanamuziki wetu wa Dansi.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles