31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

SERGIO AGUERO AVUNJIKA MBAVU MBILI

AMSTERDAM, UHOLANZI

MSHAMBULIAJI wa klabu ya Manchester City, Sergio Aguero, amepata ajali ya gari na kumsababishia kuvunjika mbavu mbili, hivyo atakuwa nje ya uwanja kwa miezi miwili.

Mchezaji huyo alikuwa mjini Amsterdam nchini Uholanzi kwa ajili ya tamasha la mwanamuziki kutoka nchini Colombia, Maluma, baada ya shoo Aguero alichukua taxi ambayo ilikuwa inampeleka uwanja wa ndege kwa ajili ya safari yake kuelekea jijini Manchester na ndipo akapata ajali hiyo.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29, amefunguka kwamba ajali hiyo ingekuwa mbaya zaidi lakini kilichomsaidia ni kufunga mkanda.

Hata hivyo, klabu ya Manchester City imethibitisha mchezaji wao huyo kupata ajali hiyo na tayari Aguero amewasili jijini Manchester kwa ajili ya matibabu zaidi.

“Klabu ya Manchester City inathibitisha kuwa mshambuliaji wake, Sergio Aguero, amepata ajali nchini Uholanzi, lakini anaendelea vizuri, tunaamini hatutakuwa na mchezaji huyo kwa wiki kadhaa.

“Kutokana na hali hiyo hatuwezi kuwa naye kwenye mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya mabingwa watetezi Chelsea, kwenye uwanja wa Stamford Bridge kesho (leo),” waliandika Man City.

Inasemekana kuwa mchezaji huyo alipewa mwaliko maalumu na msanii huyo wa nchini Colombia kutokana na urafiki wao, hivyo mapema siku ya Jumanne, Aguero alitumia ukurasa wake wa Instagram na kuposti picha akiwa na msanii huyo kwenye gari.

Hata hivyo, msanii huyo na yeye aliposti picha akiwa na Aguero wakati mchezaji huyo anasaini jezi yake ya Manchester City, akiitoa kama zawadi. “Ishi muda mrefu kwenye soka na kwenye urafiki wetu, asante sana kwa kumbukumbu yako,” aliandika Maluma.

Mchezaji huyo hadi sasa ana jumla ya mabao saba katika michuano yote aliyocheza msimu huu na bado bao moja kuvunja rekodi iliyowekwa na mshambuliaji wa zamani wa Man City, Eric Brook ya kuwa mfungaji bora wa kipindi chote.

Wachezaji mbalimbali na wadau wa soka duniani wameonesha kuguswa na ajali hiyo, hivyo kupitia mitandao ya kijamii wanamtumia salamu za pole na kumtakia kila la heri aweze kupona mapema na kurudi uwanjani.

Kwa sasa klabu ya Manchester City itakuwa na pengo la wachezaji wawili nyota ambao ni majeruhi, wiki iliyopita nyota wao beki wa kushoto, Benjamin Mendy, amedaiwa kuwa anaweza kukaa nje ya uwanja hadi mwisho wa msimu huu kutokana na majeruhi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles