27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

SERA YA KUPIGA MARUFUKU KUOA ASIYE NA CHETI KIDATO CHA NNE IFUTE MASWALI HAYA

JANA gazeti dada la hili la MTANZANIA, lilimkariri Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Kakunda, akisema kuwa, Serikali inaandaa utaratibu katika sera mpya ya elimu kuzuia watoto wa kike kuolewa kabla hawajamaliza kidato cha nne.

Kwa mujibu wa Kakunda, baada ya sera hiyo kuanza kutumika, watoto wa kike watalazimika kuonyesha cheti cha kumaliza kidato cha nne (Leaving Certificate) ndipo wafungishwe ndoa.

Sisi MTANZANIA Jumamosi pamoja na kwamba tunaunga mkono juhudi zinavyofanywa na Serikali, taasisi zisizo za kiserikali na jamii kwa ujumla katika kuhakikisha mtoto wa kike analindwa na kupata haki za msingi, ikiwamo elimu, tunadhani sera ambayo ameizungumzia Kakunda kama itapita kwa maelezo hayo basi itakuwa ina nyufa nyingi.

Kama Serikali ina dhamira ya kuja na sera hiyo, tunadhani pia ni vyema ikaja na suluhisho kwa mtoto wa kike aliyefeli darasa la saba na hivyo kukosa sifa za kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza hadi cha nne katika  shule za serikali.

Tunasema hivyo kwa sababu ada katika shule binafsi za sekondari zinaeleweka kuwa ni kubwa na wazazi wengi wa Tanzania ni vigumu kuhimili.

Si hivyo tu, pia tunazo kumbukumbu zinazoonyesha kuwa, Serikali bado haina shule nyingi za sekondari ambazo zinaweza kuhudumia watoto wote wanaokwenda kidato cha kwanza hadi cha nne.

Kwa sababu hiyo, Serikali inapojiandaa kuja na sera hiyo ihakikishe inatazama hali halisi za maisha ya Watanzania ili kusiwepo kisingizio chochote cha mzazi au mlezi kushindwa kumpeleka mtoto shule au mtoto mwenyewe kushindwa kufika kidato cha nne.

Sera hiyo isipokuja na suluhisho hilo, ni wazi itakuwa haina tofauti na kauli iliyopata kutolewa na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria wakati huo, Dk. Harrison Mwakyembe.

Mwakyembe, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, alipiga marufuku ufungishaji ndoa za aina zote bila kuwa na cheti cha kuzaliwa, kabla ya kauli yake hiyo kutenguliwa na Rais Dk. John Magufuli.

Rais Magufuli alilazimika kutengua kauli hiyo akisema ameshangazwa na kauli ya Mwakyembe ya kupiga marufuku ufungishaji ndoa za aina zote bila kuwa na cheti cha kuzaliwa.

Rais Magufuli alisema kauli hiyo ya Dk. Mwakyembe kwamba Serikali imepiga marufuku ufungishaji ndoa za aina zote, iwe za kidini, kimila na kiserikali bila kuwa na cheti cha kuzaliwa kinachotolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), ilimshtua hivyo alilazimika kutoa ufafanuzi na kuifuta.

Katika ufafanuzi huo, Rais Magufuli, ambaye si mara ya kwanza kutofautiana au kutengua maagizo ya wasaidizi wake, alisema ingawa yeye si mwanasheria, lakini anafahamu sheria ya vizazi na vifo sura ya 108 iliweka masharti ya usajili wa lazima kati ya mwaka 2009, lakini hakukuwa na kipengele cha kuoa au kuolewa.

Katika hilo, alisema anachojua yeye ile sheria ya vifo na kuzaliwa sura namba 108, ambayo iliweka masharti kati ya mwaka 2009, masharti ya kwamba awe na compulsory registration (usajili wa lazima), katika masharti hayo hapakuwapo na kipengele cha kuoa au kuolewa.

Alisema katika sheria ya ndoa sura namba 29, hakuna mahali panapozungumza kwamba wakati wa kuoa lazima uwe umesajiliwa.

Kwa kumbukumbu kama hizo, tunadhani sera mpya ambayo inaandaliwa na Serikali itafuta makosa kama hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles