27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Sensa ya Watu inavyoakisi maendeleo ya Taifa

Na BAKARI KIMWANGA-DAR ES SALAAM

KWA mara ya mwisho Tanzania ilifanya Sensa ya Watu na Makazi Agosti 26, mwaka 2012 ambapo matokeo yake yalionesha idadi ya Watanzania kufikia milioni 45.

Katika historia ya nchi yetu, Sensa hiyo ilikuwa ni ya tano kufanyika tangu Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 na kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 26, 1964.

Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988 na 2002. Kumbukumbu zinaonesha kuwa kwa upande wa Tanzania Bara wakati wa ukoloni zilifanyika Sensa mwaka 1910, 1931, 1948 na 1957. Kwa upande wa Zanzibar wakati wa ukoloni na utawala wa Sultan kulifanyika Sensa mara moja mwaka 1958.

Dhumuni kubwa la Sensa ya Watu na Makazi ni kujua idadi ya watu, mahali walipo, jinsia zao, umri wao, elimu, shughuli wazifanyazo, vipato vyao, upatikanaji wa huduma mbalimbali pamoja na makazi. 

Taarifa hizo hutumiwa na Serikali kupanga mipango ya maendeleo, kutengeneza programu mbalimbali na kubuni miradi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. 

Aidha, huisaidia Serikali kupanga na kupeleka huduma za kiuchumi na kijamii kwa wananchi kwa kuzingatia mahitaji halisi ya maeneo yao wanayoishi kwa mujibu wa idadi yao na mgawanyiko wao kijinsia, kiumri na huduma zinazohitajika. 

Hivyo basi, idadi halisi isipojulikana kuna hatari ya wananchi kukosa huduma wanazohitaji kwa kiwango kinachostahili. Vilevile, takwimu hizi hutumiwa na Serikali katika kufikia uamuzi wa kugawa majimbo ya uchaguzi na maeneo ya utawala kama vile mikoa, wilaya, kata, vijiji na vitongoji vipya.

Katika matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, ambayo yalizinduliwa na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, ambapo alionyesha kwamba Tanzania sasa ina watu 44,929,002, kati yao 43,625,434 wakiwa wa Tanzania Bara na 1,303,568 Zanzibar.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa Tanzania ina kasi kubwa ya ongezeko la watu, ambapo hadi kufikia mwaka mwaka 2016 Taifa litakuwa na jumla ya watu milioni 51na kufikia Sensa ya mwaka 2022 idadi ya watu naweza kufikia milioni 55 au zaidi.

Hata hivyo idadi hiyo inaweza kuonekana kuwa haina tatizo kwa nchi kama Tanzania, lakini ni mzigo kwa taifa, jamii na kwa uchumi.

Kutokana na kasi hiyo ya ongezeko la watu hapana budi kuwa na mikakati madhubuti na mipango mipya ya maendeleo kuanzia sasa.

Ikiwamo kupanga uzazi, vinginevyo hali ya maisha itazidi kushuka na ushindani katika rasilimali chache tulizonazo utazidi kuwa mkubwa.

NBS yajipanga kwa Sensa 2022

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk. Albina Chuwa(kushoto) akiangalia ramani kupitia teknolojia ya kisasa.

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk. Albina Chuwa, anasema matumizi ya teknolojia za kisasa yataleta ufanisi mkubwa katika sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, hivyo kuipatia nchi takwimu za uhakika zaidi na kwa wakati kuliko sensa zilizopita.

Ameyasema hayo hivi karibuni alipotembelea wilayani Kondoa kukagua maendeleo na ubora wa kazi katika hatua ya awali ya utengaji wa maeneo Mtaa wa Mnarani, ikiwa ni sehemu ya matayarisho ya Sensa ya mwaka 2022.

“Lengo letu ni kufanya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa ufanisi mkubwa na nimekuja hapa kukagua na kutathmini ubora wa kazi ya kutenga maeneo katika wilaya yenu,” anasema Dk. Chuwa.

Dk. Chuwa alionyeshwa namna maeneo hayo yanavyopimwa na kuwekewa mipaka pamoja na namna taarifa zinavyohifadhiwa katika kishikwambi (tablet) ambazo zitatumika wakati wa kuhesabu watu tofauti na sensa zilizopita ambazo wadadisi walikuwa wakitumia ramani zilizochorwa kwenye karatasi.

Watu waliosahaulika 2012

Katika sensa ya mwaka 2012 kiwango cha watu waliosahaulika kuhesabiwa kilikuwa asilimia tano, ambacho hata hivyo ni cha chini ikilinganishwa na nchi nyingine barani Afrika.

“Tunataka kile kiwango cha asilimia tano cha waliosahauliwa kuhesabiwa mwaka 2012 kiondoke katika sensa ijayo ili tupate takwimu halisi na kuongeza ufanisi katika upangaji wa mipango yetu ya maendeleo,” anasema Dk. Chuwa.

Mkuu wa Kitengo cha Mifumo ya Taarifa za Kijiografia katika Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Benedict Mugambi, anasema kwa kutumia kishikwambi, mdadisi atafanya kazi yake ya kuhesabu watu katika eneo lake tu na hataweza kuingia eneo la mwenzake.

“Mdadisi akitoka nje ya eneo lake, kishikwambwi kitamuonyesha alama kuwa anaingia eneo silo, lakini zaidi dodoso halitaweza kufunguka, hivyo hataweza kufanya kazi,” anaeleza Mugambi.

Kiongozi wa timu hiyo, Mrasimu Ramani Jerve Gasto wa NBS, anasema kwamba hadi sasa vijiji vyote 84 katika Halmashauri ya Kondoa Vijijini tayari vimetengewa maeneo ya kuhesabia watu na taarifa zote muhimu zimeshachukuliwa na kuweka katika ramani.

Umuhimu wa Takwimu 

Takwimu zinaonesha uchumi wa Tanzania hauko katika hali mbaya sana katika miaka ya karibuni, lakini kupanda kwa bei za vyakula, idadi ya watu wasio na ajira, kupungua kwa kiwango cha rushwa jambo ambalo limechochea kasi ya ujenzi wa miradi ya maendeleo ya kimkakati.

Matokeo ya mipango ya maendeleo ya jamii ambayo wanasiasa hudai mara kwa mara kuwa imekuwa ya mafanikio, hasa katika sekta za elimu na afya, imekuwa ikipata mafanikio kwa kuongezeka zaidi ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita.

Katika hali hiyo ni wajibu wa kila raia kushiriki katika tafiti mbalimbali ambazo huendeshwa na Serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwani ukusanyaji huo wa Takwimu husisha maisha ya wananchi moja kwa moja.

Kama ilivyokuwa kwa Sensa zilizotangulia, madhumuni makubwa ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 iliweza kujua idadi ya watu, mahali walipo, jinsia zao, umri wao, elimu, shughuli wazifanyazo, vipato vyao, upatikanaji wa huduma mbalimbali pamoja na makazi. 

Taarifa hizi hutumiwa na Serikali kupanga mipango ya maendeleo, kutengeneza programu mbalimbali na kubuni miradi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. 

Aidha, huisaidia Serikali kupanga na kupeleka huduma za kiuchumi na kijamii kwa wananchi kwa kuzingatia mahitaji halisi ya maeneo yao wanayoishi kwa mujibu wa idadi yao na mgawanyiko wao kijinsia, kiumri na huduma zinazohitajika. 

Hivyo basi, idadi halisi isipojulikana kuna hatari ya wananchi kukosa huduma wanazohitaji kwa kiwango kinachostahili. 

Vilevile, takwimu hizi hutumiwa na Serikali katika kufikia uamuzi wa kugawa majimbo ya uchaguzi na maeneo ya utawala kama vile mikoa, wilaya, kata, vijiji na vitongoji vipya.

Pamoja na umuhimu huo wa jumla wa Sensa kwa maendeleo ya nchi, ina umuhimu wa aina yake ambapo taarifa zake zitatumika kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2020/2021  ambao umelenga kutekeleza maeneo ya kipaumbele ikiwa ni pamoja na kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu kwa kuweka mkazo katika upatikanaji wa huduma bora za jamii ikiwemo elimu, maji, afya, umeme na barabara.

Maeneo mengine ni ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda kwa kuimarisha sekta ya kilimo kwa kujenga viwanda vitakavyotumia malighafi inayopatikana nchini, kuimarisha mashirika ya viwanda na kuanzisha na kuendeleza maeneo ya viwanda.

Utafiti wa umaskini

Kutokana na Sensa ya Watu na Makazi, Ofisi ya Taifa ya Takwimu hufanya tafiti mbalimbali ikiwamo kuangalia hali ya umaskini wa mapato.

Kwa mujibu wa  ripoti ya Matokeo ya Viashiria Muhimu vya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Mwaka 2017/2018, Ofisi ya Taifa ya Takwimu imekuwa kwenye mkakati madhubuti kwa kushirikiana na taasisi za kitafiti kuchunguza sababu za hali ya umasikini katika baadhi ya maeneo nchini.

Akizungumza hilo, Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa, alisema ripoti iliyotolewa inaonesha picha ya umasikini ilivyo bila ya uchambuzi unaoonesha sababu za hali kuwa hivyo.

“Tuna mpango wa kushirikiana na taasisi za kitafiti nchini kama REPOA kuangalia sababu za hali ya umasikini katika katika ngazi za chini ili kujifunza kama ambavyo tulivyowahi kufanya huko nyuma,”anasema Mtakwimu Mkuu.

Kwa mujibu wa Utafiti huo, umasikini wa mahitaji ya msingi umepungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2011-12 hadi asilimia 26.4 mwaka 2017/18 huku umasikini wa chakula ukionesha kupungua kutoka asilimia 9.7 hadi asilimia 8.0 katika kipindi hicho hicho.

Kauli ya Benki ya Dunia 

Mwakilishi wa Benki ya Dunia hapa nchini, Betty Talbert, anawataka wadau kuwa kutambua kwamba pamoja na kuwa kazi ya kutayarisha ripoti ni vema kushirikiana na NBS kufanya uchambuzi kanzidata ya utafiti mbalimbali ikiwamo ya hali ya umaskini.

“Kanzidata ya utafiti huu ina utajiri mkubwa wa taarifa za kitakwimu ambazo zikifanyiwa uchambuzi wa kina zitaleta manufaa makubwa kwa Tanzania na wadau wengine hivyo shime jitokezeni kusaidia uchambuzi wa kazidata hiyo,” anasema Talbert

Alibainisha kuwa miongoni mwa taarifa ambazo zitatokana na kanzidata ya utafiti huo ni pamoja na ripoti ya umasikini wa watoto ambao itatolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalioshughulikia Watoto (UNICEF) na taarifa maalum kuhusu matumizi ya muda katika kazi zisizo na malipo ambayo itatolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Wanawake-UN Women.

Mwakilishi huyo wa Benki ya Dunia anaipongeza NBS kwa kasi iliyoonesha katika utayarishaji wa ripoti za utafiti huu na kwamba imekuwa ni mfano kwa wengine kuiga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles