Sekta ya ushereheshaji yatajwa kuchangia pato la taifa

0
588

Janeth Mushi, Arusha Sekta ya ushehereshaji nchini inatajwa kuwa miongoni mwa sekta yenye nafasi kubwa ya kuongeza pato la taifa na pia kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la ajira kwa vijana.

Hayo yalisemwa jana jijini hapa na Mbunge wa Viti Maalum,Mkoa wa Manyara, Ester Mahawe(CCM), akizungumza katika semina ya washereheshaji kutoka mikoa ya Kanda ya Kaskazini, iliyoandaliwa na Umoja wa Washereheshaji Mkoa wa Arusha(UWAA).

Amesema vijana hasa wenye vipaji mbalimbali ambao wakipatiwa elimu ya ujasiriamali wataweza kuondokana na tatizo la kutegemea ajira katika sekta iliyo rasmi hasa serikalini.

“Washereheshaji wana nafasi kubwa ya kuongeza pato la taifa kwa kutumia vipaji vyao badala ya kutegemea ajira, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya ujasiriamali, watu wakaanzisha biashara mbalimbali.

“Hili si kundi la kudharau ni kundi la kuheshimiwa, ni kundi kubwa lenye uwezo wa kuchangia pato la taifa kwa namna mbalimbali hata kwa kutoa elimu ya ujasiriamali kwani mnakutana na watu wengi kwa wakati mmoja wakati mkitekeleza majukumu yenu, tumieni vipaji vyenu vizuri,” amesema mbunge huyo.

Awali Mwenyekiti wa UWAA, Mohamed Msoffe, alisema lengo la semina hiyo ni kukumbushana weledi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, kufahamiana, kubadilishana uzoefu na kupewa elimu na masuala ya ugonjwa Ukimwi, ili na wao wakatumie majukwaa mbalimbali kuisaidia serikali kutoa elimu ya ugonjwa huo.

“Tuzidi kushirikiana, tusipigane vijembe wala majungu au kushusha gharama za utoaji huduma ili kuvutia wateja bali tujitahidi kufanya kazi kwa ubora na tumejiona tuna nafasi ya kuisaidia serikali kutoa elimu ya masuala ya Ukimwi, hivyo tutumie nafasi zetu kuelimisha jamii,” amesema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here