24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

SEKTA MISITU NCHINI INAKOSA MATUMIZI SAHIHI  

Na LEONARD MANG’OHA


MOJA ya ajenda zinazotawala mijadala ya mikutano mbalimbali ya kikanda na kimataifa ni pamoja na suala la mabadiliko ya tabianchi, hususan tishio la ukame linaloikabili dunia kwa kasi katika kipindi cha miaka ya karibuni.

Madhara ya ukame yameanza kujitokeza kwa kasi kubwa katika maeneo mbalimbali ya dunia, huku Bara la Afrika likionekana kuwa mwathirika mkuu wa janga hili, ambapo ukame mkubwa umeshuhudiwa katika mataifa kama vile Kenya na Ethiopia, kiasi cha watu kulazimika kuyahama makazi yao, huku mifugo ikifa kwa kukosa malisho.

Chanzo kikuu cha madhara haya, pamoja na mambo mengine, ni shughuli za kibinadamu kama vile uchomaji mkaa na ufyekaji misitu kwa shughuli za kilimo.

Nimepata nafasi ya kumuuliza Mkuu wa Shule ya Misitu ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Mtaalamu wa Masuala ya Misitu, Profesa John Kessy, ikiwa kuna namna ambayo inaweza kusaidia kuokoa misitu na kuwa fursa ya kiuchumi kwa wananchi, badala ya wendawazimu wa kuteketeza misitu kwa lengo la kujipatia kipato.

Anasema jambo linalopaswa kufahamika ni kwamba misitu ni chanzo cha kiuchumi kama vyanzo vingine na imekuwa ikichangia katika pato la taifa (GDP) asilimia nne.

Anasema ziko aina mbili za misitu ambayo ni ile iliyo katika maeneo ya uhifadhi ambayo hairuhusiwi kutumika kwa shughuli za kibinadamu na huhifadhiwa kwa kusudi la kuhifadhi vyanzo vya maji na mambo mengine, sambamba na ile isiyo ya uhifadhi.

Anasema misitu inaweza kuwapa kipato cha kutosha wananchi kwa kulima misitu binafsi nje ya misitu ya hifadhi ambayo wanaweza kuiuza kwa matumizi mbalimbali ya shughuli za kibinadamu.

Anataja mahitaji ya nguzo za umeme na shughuli nyingine kama moja ya masoko ambayo wananchi wanaweza kuuza miti yao.

Anasema kwa sasa kuna aina ya miti ya kisasa inayokua haraka na kufikia kuvunwa kwa kipindi cha miaka sita pekee, ikiwa tayari na uwezo wa kutoa magogo yenye uwezo wa kuzalisha nguzo za umeme.

“Kinachotakiwa ni wananchi kushirikishwa katika usimamizi wa misitu kwa kuanzisha misitu shirikishi na wao waweze kuanzisha misitu yao wenyewe nje ya misitu ya hifadhi.

“Kwa mfano, Mafinga (Iringa) wananchi wana misitu yao, watu waeleweshwe namna ya kuhifadhi na kuoneshwa njia mbadala ya kuweza kupata mazao mbalimbali yanayotokana na misitu,” anasema Profesa Kessy.

Anaeleza kuwa, kupitia kilimo cha misitu, wananchi wanaweza kuendelea na shughuli za kilimo cha mazao ya muda mfupi, kama vile viazi, mazao ya jamii ya mikunde na mengine yoyote yanayoweza kustawi katika mazingira hayo.

Anasema kitaalamu inashauriwa mwanzoni mkulima anaweza kuchanganya misitu na mazao mingine na hii hufanyika hadi baada ya miaka mitatu tangu kupandwa kwa miche ya misitu kipindi ambacho kwa kawaida miti inakuwa na kiasi kidogo cha majani.

“Kwa sababu misitu ni zao la muda mrefu, ni lazima mkulima aendelee na kupata kipato kupitia shughuli za uzalishaji wa mazao madogo madogo ya kilimo, ambayo yatasaidia pia kuitunza misitu kwa kuiweka katika hali ya usafi.”

Anasema mfumo huu kitaalamu hufahamika kama ‘Taungya-system’, ambayo humtaka mkulima kuendelea kupata faida katika eneo linalokuza msitu kabla ya msitu kuwa mkubwa.

Anasema shughuli nyingine inayoweza kufanyika katika misitu ni ufugaji wa nyuki, ambao utamwezesha mkulima kuvuna mazao ya mdudu huyo, ikiwamo asali ambayo imekuwa miongoni mwa shughuli kuu za kiuchumi katika baadhi ya jamii nchini.

Mfumo mwingine ni ule unaofahamika kama ‘agro-forest’ ambao huhusisha shughuli za kilimo cha mazao na misitu.

Nchini Gabon, sekta ya misitu ilichangia asilimia 4.7 ya pato la taifa mwaka 2009, ikiwa imepanda kutoka asilimia 2.5 mwaka 2004, mchango unaokwenda sambamba na uhifadhi madhubuti wa mazingira na uhifadhi wa misitu, huku uwekezaji binafsi katika sekta hiyo ukielezwa kufikia dola za Marekani bilioni 1.5.

Katika ripoti ya mwaka 2015, inaonesha kuwa sekta ya misitu nchini Scotland huchangia kiasi cha Euro bilioni moja katika pato la nchi hiyo kila mwaka, huku ikiajiri zaidi ya watu 25,000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles