30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

SEAMIC KUFUNGUA MAABARA MADINI NCHINI

Na Mwandishi Wetu

TANZANIA kujizatiti zaidi katika kushughulikia madini kwa kuwa na maabara ya kisasa kwa utafiti, utambuzi na uchunguzi wa madini.

Maabara ya teknolojia ya hali ya juu ya uchambuzi na uongezaji thamani madini ya vito iko mbioni kufunguliwa nchini na hivyo kuwezesha nchi kuwa na uwezo wa kutambua kile kinachopelekwa nje na wahusika mbalimbali na madini nchini.

Kwa mujibu wa maelezo ya Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe, maabara hiyo itarahisisha shughuli za utafiti, uchambuzi na uthaminishaji wa madini mbalimbali  yanayochimbwa barani Afrika.

Wazo na utekelezaji wa mradi huo umefika wakati mwafaka, wakati nchi inapambana na uhalifu na udanganyifu ulioshamiri katika sekta ya madini nchini, ikiwamo yale madini ya dhahabu na vito kama tanzanite na sapphire.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wiki jana, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 37 wa Mwaka  wa Kituo cha Madini Afrika, Profesa Mdoe  alisema ujenzi wa maabara hiyo unatokana na maazimio ya mkutano wa mwaka jana ambayo yalinuia kukiwezesha kituo hicho kujiendesha chenyewe.

“Katika malengo tuliyojiwekea mwaka jana ni kuongeza thamani ya madini, kufanya utafiti na kujiwezesha. Pia kusaidia nchi hizi katika kufanya uchambuzi wa madini mbalimbali na kuweka kazidata za kisayansi ambazo awali zilikuwa za kikanda, lakini kwa sasa ni za Afrika yote.

“Kwa mfano, ukitaka kujua kuna madini gani Tanzania unapata na hata ukitaka kujua ukanda fulani una madini ya aina gani na ni  kiasi gani utapata.

“Kwa hiyo malengo ya mwaka jana ni kukiwezesha chuo kijisimamie na kiweze kujiendesha kwa njia ya kuwa na miradi yake, kwa mfano wa kujenga maabara ya teknolojia ya hali ya juu. Na sasa inabidi tuone ujenzi umefikia wapi ili tukifungue,” alisema Profesa Mdoe.

SEAMIC kwa muda mrefu kimekuwa kituo cha kupima na kutoa cheti cha ithibati kwa ajili ya ‘certificate of origin” kwa madini ya vito, hasa Tanzanite na almasi kutoka Mwadui na hivyo kusaidia upatikanaji wa takwimu na kukubalika katika masoko ya kimataifa ya madini.

Awali Profesa Mdoe alisema kuwapo kwa Kituo cha Madini Afrika hapa nchini kumenufaisha pia wanafunzi wa vyuo vikuu wanaosomea jiolojia na uchakataji wa madini ambao wamekuwa wakikitumia kituo hicho kwa mazoezi ya masomo yao.

Alifafanua kuwa, nchi wanachama wanalipa ada ya dola elfu 62 kwa mwaka, hivyo kwa nchi mwanachama inayohitaji huduma za kituo hicho, inapunguziwa asilimia 40 ya gharama za kazi husika.

Naye Mkurugenzi wa Jiolojia kutoka Wizara ya Nishati na Madini ya Kenya, Shadrack Kimomo, alisema kituo hicho kimewasaidia kupika wataalamu wengi wa madini nchini mwake.

Alisema uwapo wa kituo hicho umesaidia  Serikali ya Kenya kujenga  kituo chake cha kuchambua madini ya vito na kinaendelea vizuri kwa kutoa huduma stahiki.

“Wataalamu wengi nchini kwetu wanategemea kituo hiki kwa kupata ujuzi zaidi, napenda kuweka wazi bila kituo hiki na sisi huko Kenya tusingeweza kujenga chetu,” alisema Kimomo.

Jijini Dar es Salaam kituo hicho kiko eneo la Kunduchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles