29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

‘SCORPION’ AANZA KUJITETEA MAHAKAMANI

Na FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM 

SALUM Njwete maarufu kama ‘Scorpion’ (35) ameiomba Mahakama ya Wilaya ya Ilala kumwachia huru kwa madai kuwa hahusiki na unyang’anyi wa kutumia silaha na kumjeruhi, Said Mrisho.

Njwete aliwasilisha maombi hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Flora Haule, alipoanza kujitetea akiongozwa na wakili wake, Juma Nassoro.

Akitoa utetezi wake huo, Njwete ambaye alikiri kuwa mwalimu wa sanaa za mapigano na mshiriki kwenye tamthilia mbalimbali alidai siku ya tukio Septemba 6, mwaka jana akiwa kwenye maeneo yake ya kazi kuanzia eneo la reli hadi kwenye daraja jipya la chuma lililopo jirani na kituo cha daladala cha Buguruni Sheli, alisikia kelele za watu waliokuwa wakihamaki.

“Siku ya tukio nilikuwa nafanya msako kama ilivyo kawaida yangu kwenye maeneo yote inapofika usiku kuazia saa 2 hadi saa 5 usiku.

“Wakati nikiendelea nilisikia zogo na wakati nikiwa bado na taharuki niliona kundi kubwa la watu waliokuwa wanazozana.

“Nilisogea hadi maeneo ya Buguruni mataa, baada ya kufika hapo niliwaona baadhi ya vijana wanaoendesha bodaboda na kuwauliza juu ya kilichokuwa kikiendelea.

“Walinijibu kuwa kulikuwa na mwizi anapigwa, Kutokana na wingi wa watu nilishindwa kuingia katikati yao ikabidi nirudi hadi Kimboka kwa meneja wangu (Hussein).

“Nilimwambia juu ya tukio hilo akanijibu kuwa tayari alikuwa amesikia, kwani naye alikuwa akiangalia eneo hilo,” alidai Njwete.

Njwete aliendelea kudai kuwa waliendelea kushangaa tukio hilo na bosi wake na kwamba baada ya dakika 20 ilifika gari ya polisi ambayo iliwatawanya watu na kuondoka na mtu huyo aliyedaiwa kuwa ni mwizi.

“Baada ya polisi kuondoka na mtu huyo walirudi baada ya dakika 20 na kuwakamata baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa pale na kuondoka nao. Ilipofika saa 6:30 usiku niliondoka.

“Kesho yake baada ya kuwasili ndipo nikaambiwa kuwa yule mwizi aliyepigwa alitobolewa macho, ila baadhi ya watu walikuwa wanasimulia kuwa alikuwa ni mmoja wa viongozi wa genge la boda to boda ambalo lipo Tabata.

“Baada ya siku nne ndipo nilipoambiwa na bosi wangu kuwa nilikuwa nahitajika Kituo cha Polisi Buguruni,” alidai Scorpion.

Alidai yeye si mhalifu wala mwizi na hajawahi kupata kashfa zozote kama vile kugombana na watu, kuhusishwa na makosa ya jinai na kwamba jamii inamhitaji sana kwa elimu anayoitoa kupitia sanaa za maigizo.

“Pia jamii inanihitaji kwa ulinzi na kama mwalimu, hivyo naomba mahakama yako iniachie huru,” alidai Njwete.

Aliieleza mahakama kuwa aina ya uhalifu uliokuwa ukifanyika katika eneo la Buguruni ni pamoja na kuiba, kupora mali, pochi, simu na chochote ambacho mtu anakuwa amekishika mkononi.

“Uhalifu huu ulikuwa ukifanywa na magenge mengi yakiwamo Gorogota la Buguruni kwa Madenge, Sri Lanka la Vingunguti, Boda to Boda la Tabata na jingijne la Kabashida la Buguruni kwa Mnyamani. Hivyo, makundi haya yote yalikuwa yamejenga chuki na mimi baada ya kuona nawadhibiti,” alidai.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Novemba 22, mwaka huu itakapoendelea kusikilizwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles