26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

‘SATARANJI’ INATUCHELEWESHA KUFIKIA MALENGO

Humphrey Polepole
Humphrey Polepole

NA INNOCENT NGANYAGWA,

KUNA michezo rahisi inayoshabikiwa zaidi na Watanzania kwa kufuata mkumbo tu kama ilivyo kandanda inayohusudiwa zaidi, lakini michezo ya kuketi inayohusisha watu wawili, drafti, bao au karata inashabikiwa zaidi.

Ipo michezo mingine inayohitaji ufundi mkubwa isiyohusudiwa na wengi kutokana na kutumia fikra nyingi, michezo hiyo huwasaidia wanaoicheza kunoa akili na kuwapa wepesi wa kufikiri.

Sizungumzii michezo bali naitumia kwa muktadha wa hoja yangu nikinasibisha na mwenendo wetu kisiasa nchini, huhitaji kuwa mweledi kutambua ‘mwenendo tenge’ usiotusaidia kutimiza malengo ya ujumla, pengine unatimiza malengo machache kwa dhamira tusiyoitambua kwani hatufahamu mashiko yake.

 Sataranji ni jina la Kihindi la mchezo mgumu unaoitwa ‘Chess’ kwa Kiingereza unaochezwa na watu wawili, unaotumia kete zenye maumbo tofauti zenye nguvu ya mwelekeo mbadala kwenye ubao wa kuchezea. Ushindi katika mchezo huo hupatikana kwa kuua kete kuu (Mfalme), kwa kupunguza kete zinazoilinda lakini kila unapoikaba kete kuu ukikaribia kumaliza mchezo unawajibika kumtahadharisha mpinzani wako ukitamka ‘check!’

Ninanasibisha matukio mawili ya hivi karibuni ya ‘uteuzi’ na ‘utenguzi’ wa nafasi mbili mojawapo ikimhusisha mwanasiasa anayepanda chati, Humphrey Polepole, Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mwenye misimamo thabiti aliyejaliwa uwezo wa kujenga hoja bila kuudhi. Sina shaka na uwezo wake kiutendaji kwa kuwa mimi ni mmojawapo wa watu wanaomfahamu siku nyingi katika harakati nyingine kabla ya kuibukia kwenye siasa.

Namtumia kujenga hoja ya panga pangua kutoka ukuu wa wilaya mpya ya Ubungo hadi nafasi aliyopo sasa, katika zoezi endelevu la kupanga kikosi cha watimiza majukumu ingawa pia kujenga uzoefu kuna umuhimu wake ili malengo yafikiwe kwani mtu anayehamishwa wadhifa kila baada ya muda mfupi, hawezi kutimiza vipaumbele kwa kuwa kila mara anaanza upya.

 Najaribu kuishughulisha tafakuri yangu kwa ufahamu wangu mdogo kwamba ukijiandaa kushika uongozi, licha ya mfumo uliowekwa kukulazimisha kufuata utaratibu wa kuteua na kupanga safu yako, lakini una utashi binafsi wa maandalizi yanayozingatia muda mchakato (timeline) ndani ya kipindi husika (time frame), ili ukianza kusimika umalize kwa wakati na kujielekeza kutimiza malengo badala ya kupanga na kupangua kila kukicha.

Pengine tunahitaji kubadilisha mfumo wa ‘muda mpito’ wa kupokezana hatamu ili kuweka pengo la kupanga safu, kama tunavyoshuhudia kitakachotokea hivi karibuni nchini Marekani kwamba Rais mteule tayari ameshapanga safu yake ya Baraza la Mawaziri na akikabidhiwa rasmi majukumu kwa kuapishwa, anaanza kutimiza kinachobainishwa kwa nahau ya Kiingereza: “To hit the ground running!” Kwamba hakuna kupoteza muda wa kuanza kazi. Tofauti na sisi ambao hata kutangazwa kwa kikosi cha utawala mpya hugubikwa ‘promo’ na utabiri mwingi kutokana na mfumo wetu tuliojiwekea.

 Ndiyo maana muda mwingi unatumika kucheza ‘Sataranji’ ya kisiasa, kwamba hata baada ya kazi kuanza bado kuna utenguzi na uteuzi unaokengeusha dhima ya mwelekeo na kugeuza kunyofoa na kupachika watendaji kwenye nafasi zao kuwa kipaumbele, kinachopigiwa debe na kila mmoja hata vyombo vya habari bila kutimiza methali isemayo ivumayo haidumu.

Hata kwenye fani ya muziki wimbo ukichosha masikio na mtunzi hana tungo nyingine basi hufanya ‘toleo mbadala’ (remix) ili kukamata tena masikio ya wasikilizaji, lakini kwenye siasa zetu ‘nyimbo’ hazina ‘remix’ ingekuwa muziki, singo ya ‘Kutumbua’ ingeshakuwa na remix yake!

Sataranji nyingine inahusisha taaluma inaposigana na siasa ambayo ni fani kamili, lakini kitaaluma kuna baadhi ya maeneo yanakulazimu kusomea au kuwa na sifa tanzu za ziada ili kumudu nafasi unayokasimiwa ya uongozi.

Inanikumbusha enzi za Mwalimu Julius Nyerere kilipoanzishwa chuo cha chama Kivukoni ingawa kwa sasa ukikitaja unaonekana umepitwa na wakati kutokana na muktadha husika kama ambavyo utashangaza ukionekana umebeba kijitabu cha misingi ya TANU na kuhisiwa kuwa fikra zako haziko mujarab.

 Najaribu kujilinganisha na wenzetu ughaibuni waliotutangulia kimaendeleo, kwamba wataalamu wao wakitaka kubainisha waliyoyatafiti wanahitaji idhini ya mwenye wadhifa wa kisiasa ambaye hana taaluma husika? Inawezekana ni mfano mkubwa kulinganisha na sakata la ‘zika’ lililohusisha mwanataaluma na mwanasiasa, ingawa sidhamirii kulenga suala hilo bali ukimtengua Mwele Malecela, kwa kutimiza weledi wake na kumsimika mweledi mwingine hujapoteza kitu, lakini ni mwendelezo wa ‘Sataranji’ inayozidi kutuchelewesha na tayari tuko nje ya muda mchakato. Kitakachojiri?

Tumeshauanza mwaka wa pili wa awamu ya tano na kila aliye katika wadhifa wa kuchezesha ‘Sataranji’ ili aonekane anatimiza dhima anatuimbia tungo inayoitwa ‘Kutumbua’ iliyokosa toleo mbadala (remix), pengine methali ya ‘mlimila dole’ yaani asemaye bila kutenda au ‘maisha si mazoezi bali ni tumbuizo halisi’ hazina maana yoyote kwetu, kwa kuwa ni suala la kuwamba ngozi kuvutia kwetu ili ionekane dhima inatimizwa bila kujali kuwa siku hazigandi kutusubiri tujirekebishe!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles