31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Saratani mlango wa kizazi hatari zaidi kwa waathirika VVU

Na Derick Milton

-Simiyu

SHIRIKA la Afya Duniani linasema kuwa saratani ya mlango wa kizazi ni moja kati ya magonjwa yanayosababisha vifo vya wanawake kwa wingi katika nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwamo.

Utafiti wa mwaka jana, uliofanywa na kituo cha habari cha saratani ya mlango wa  kizazi Tanzania (HPV Information Centre), unabainisha kuwa wanawake 9,772 wengi wao wakiwa na umri wa kuanzia miaka 40-64 waligundulika kuwa na saratani ya mlango wa kizazi hapa nchini.

Kila mwaka inakadiriwa kuwa wanawake 6,695 wengi wao wakiwa na umri wa miaka 15-44 wanapoteza maisha kutokana na saratani hiyo ikiwa ni asilimia 22.4 ya waathirika wote nchini.

Wataalumu wa masuala ya afya wanasema saratani ya mlango wa  kizazi hutokea katika chembechembe za shingo ya kizazi, ambayo ni sehemu ya chini ya mji wa mimba (uterus).

Takwimu za Kituo cha Kudhibiti Maradhi Duniani (CDC), za mwaka 2008 zinaonesha kuwa katika kila wanawake watatu, wawili kati yao wanashambuliwa na saratani ya aina hii duniani.

Hapa nchini, inakadiriwa kuwa zaidi ya wanawake milioni 14 walio katika umri wa kuzaa kuanzia miaka 18 hadi 25 wapo hatarini kupata saratani ya shingo ya kizazi.

Hatari kwa wanaoishi na VVU

Watalaamu wa afya wanasema watu walioko kwenye hatari zaidi ya kupoteza maisha kwa haraka endapo watapata saratani hii ni wale wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Lina Ngowi, ni mtaalamu wa huduma za afya ya mama, baba na mtoto, anasema watu wanaoishi na VVU wako hatarini zaidi kutokana na kinga zao kuwa chini kuweza kupambana na ugonjwa huo.

Anasema ikiwa mtu huyo atashambuliwa na wadudu wanaosababisha ugonjwa huo (Humanpapilloma Virus) na wakati huo kinga zake zipo chini, uwezekano wa kuathirika zaidi ni mkubwa.

“Mtu ambaye anaishi na Virusi vya Ukimwi tunatambua kuwa kama hatumii dawa za kurefusha maisha (ARVs) basi mwili wake uko katika hatari zaidi ya kushambuliwa na magojwa mengi, saratani hii ikiwamo,” anasema Ngowi.

Anaongeza: “Ikiwa wadudu hao watamshambulia na kupata saratani ya mlango wa kizazi, watapata nafasi kubwa na kumletea madhara makubwa zaidi hadi kumsababishia kifo kutokana na kutokuwapo kwa kinga.”

Anasema VVU vinasababisha kuondoa kinga zote za mwili, hata kinga za saratani ya mlango wa kizazi, hali ambayo inachangia wadudu wa saratani hiyo kushambulia kwa urahisi.

Anasema watu wengi ambao wanaishi na VVU hasa maeneo ya vijijini wanapoteza maisha kwa kushambuliwa na saratani hiyo kutokana na kutokutumia dawa za ARVs kwa usahihi.

“Watu wengi wanaoishi na VVU maeneo ya vijijini hawatumii vizuri dawa za ARVs, kitendo hicho kinasababisha kinga zao kuwa chini na kuruhusu wadudu wa saratani hii kushambulia kwa urahisi.

Jinsi inavyoambukizwa

Ripoti za utafiti wa  kisayansi zinaeleza kuwa asilimia 99 ya saratani za shingo ya kizazi hutokana na maambukizi ya virusi vya ‘Human Papillomavirus’  au HPV vilivyoko katika jamii  ya papilloma.

Baadhi ya virusi hivi vyenye aina zaidi ya 100 huambukizwa kwa njia ya kujamiiana ambapo huwapata zaidi wale wanaoshiriki tendo la ngono katika umri mdogo, au chini ya miaka 18.

Mwenda Saidi ni Daktari wa magonjwa mbalimbali, anasema kutembea na wanaume au wanawake wengi na kufanya nao ngono zembe ni moja ya visababishi vikubwa vya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi.

“Ikiwa leo utafanya ngono na mwanamume huyu, kesho ukafanya na mwingine, siku inayofuata mwingine, uwezekano wa kuugua saratani hii huwa ni mkubwa, kwa sababu kati yao huwezi kujua nani mwenye vimelea au wadudu wanaoambukiza,” anasema Dk. Said.

Utumiaji wa sigara, tumbaku na ugoro vinatajwa pia kuwa moja ya visababishi vikubwa vya ugonjwa huo, ambapo baadhi ya wanawake huvitumia kuweka katika sehemu zao za siri.

Ngowi anasema wamekutana na wanawake wengi wanaofanya hivyo kwa kuweka ugoro na tumbaku kwenye sehemu zao za siri wakiaminishwa na waganga wa jadi kuwa wataongeza upendo kwa waume zao.

“Ukweli ni kwamba kufanya hivyo kuhatarisha maisha yao kwa kupata na ugonjwa huu, ukiweka vitu hivi ni rahisi kushambuliwa na wadudu wa saratani hii,” anaeleza Ngowi.

Mbali na sababi hizo, hata kuzaa bila ya mpangilio (mfulululizo), ni moja ya kisababishi kinachoweza kumfanya mwanamke kupata saratani hiyo.

Anasema mwanamke ambaye anazaa bila ya mpango, mlango wake wa kizazi unaweza kuchoka na kuruhusu kwa urahisi kupitia kwa wadudu wanaoambukiza saratani hiyo.

Dalili

Dalili za saratani ya mlango wa kizazi ni nyingi, lakini kubwa zaidi ni kutokwa na damu ukeni baada ya tendo la ndoa na kutokwa na majimaji au uchafu wenye harufu kali ukeni.

Dk. Said anasema ikiwa mwanamke atatokwa na damu baada ya tendo la ndoa, basi atakuwa yuko kwenye dalili za kupata ugonjwa huo.

Dalili nyingine ni kuhisi maumivu chini ya kitovu na kupungua kwa kasi kwa uzito wa mwili.

Matibabu

Serikali na wadau mbalimbali wa afya wameendelea kuboresha huduma za afya ili kupambana na ugonjwa huu unaosababisha vifo kwa wanawake.

Watalaamu wanasema ikiwa mgonjwa atawahi kituo cha huduma ya afya baada ya kuona dalili za ugonjwa huo, upo uwezekano mkubwa wa kupata matibabu na kupona.

“Huduma zinazotolewa bure ni zile za awali, kabla ya ugonjwa haujawa sugu, na zinatolewa bure na wengi wanaotibiwa huwa wanapona,” anasema.

Moja ya wadau ambao wamekuwa wakishirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu ni Shirika la Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) linalojihusisha na mapambano dhidi ya VVU/ Ukimwi.

Dafrosa Charles ni Mratibu wa Shirika hilo, mkoani Simiyu, anasema AGPAHI kwa kushirikiana na serikali wamekuwa wakitoa huduma ya uchunguzi wa ugonjwa huo pamoja na tiba ya awali  katika vituo nane vya kutolea huduma za afya mkoa mzima.

“Tunatoa huduma hizi katika hospitali ya teule ya Mkoa, vituo vya afya vya Muungano, Nguliati (Bariadi), Malampaka na Nkoma (Itilima), Nasa  na Lukungu (Busega) kituo cha afya Mwandoya (Meatu) na hospitali za wilaya za Maswa na Meatu,” anasema Charles.

Anasema katika Mkoa wa Simiyu jumla ya wanawake 11,334 toka mwaka 2017 hadi sasa wamefikiwa na huduma za uchunguzi wa saratani hiyo, kati yao wanawake 515 waligundulika na maambukizo ya awali kisha kutibiwa.

Mratibu huyo anasema licha ya kuendelea kutoa huduma hiyo kwa kusaidiana na serikali, wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi ikiwamo upungufu wa watumishi katika vituo vinavyotoa huduma ya ugonjwa huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles