24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

SARAKASI ZA DEMOKRASIA NA UTAWALA BORA AFRIKA

Na BALINAGWE MWAMBUNGU


BARA la Afrika inaelekea kurejea katika mfumo wa chama kimoja, kwani viongozi wengi wa sasa wanafanya ukandamizaji wa sauti huru na za vyama vya upinzani.

Hii inatokana na ukweli kwamba nchi zinajinasibu kwa maneno tu kwamba zinaendesha utawala wa kidemokrasia, huku ziking’ang’ania na kuzidi kujichimbia katika mfumo wa zamani wa utawala wa chama kimoja.

Baadhi ya wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema kwamba nchi hizo, ingawaje zinaendesha uchaguzi ambao viongozi wanasema ni za kidemokrasia, lakini ukweli ni kwamba uchaguzi huo ni za ujanja ujanja na sehemu nyingine ni za mabavu, huendesha uchaguzi zilizojaa vitisho.

Tanzania ni mojawapo ya nchi ambazo zina chama tawala chenye nguvu (dominant). Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni mfano halisi na dalili zote zinaonesha kwamba kinafanya kila kiwezavyo, kujiimarisha na kufanya mbinu chafu za kudhoofisha upinzani. Bado CCM ni chama dola na kinataka kiendelee kutawala bila kubughudhiwa au kunyooshewa kidole.

CCM kinajiita ni Chama Cha Mapinduzi, lakini uhalisia kinafuata mfumo wa utawala wa kinguvu kutoka juu. Chama ambacho kiko tayari kufanya jambo lolote ili kiendelee kukamata hatamu za utawala, ni chama hatari kwa ustawi wa demokrasia na utengamano wa nchi.

Hivi karibuni kutakuwa na uchaguzi wa madiwani katika baadhi ya mikoa, kinataka  kishike hatamu kuanzia Serikali za Mitaa, vitongoni, miji na majiji nchi nzima!

Katika Afrika kuna vyama tawala vyenye nguvu na vingine ni vyama rafiki wa CCM—FRELIMO  cha Mozambiki, ZANU-PF cha Zimbabwe, ANC cha Afrika Kusini, MPLA cha Angola, SWAPO cha Namibia.

Lakini kuna vyama vingine kama Botswana Democratic Party, Gabon Democratic Party, Democratic Party cha Equatorial Guines, Patriotic Salvation Movement cha Chad.

Vyama vingine vyenye nguvu ni Congolese Party of Labour (Congo Brazaville), Cameroon People’s Democratic Party, National Congress (Sudan), Justice and Development Party (Morocco) na National Liberation Front (Algeria).

Vyama vingine ni Rwanda Patriotic Front, National Resistance Movement (Uganda), Sudanese People’s Liberation Army (Sudan Kusini).

Rally for Guinea People, Party for the Independence of Guinea and Cape Verde (PAIGC), Union for the Republic (Togo), People’s Front for Democracy and Justice (Eritrea), Ethiopia People’s Revolutionary Democratic Front na Gabonese Democratic Party. Kuna chama kinaitwa Alliance of the Presidential Majority cha DR Congo.

Vyama vingi kati ya hivi, vina kila dalili ya udikteta uliovishwa joho la Mapinduzi (vingine viliingia madarakani kwa nguvu ya mtutu wa bunduki) lakini vimejivika gwanda la demokrasia huku.

Ukiangalia historia ya baadhi ya vyama hivyo, vilipigania uhuru au viliziondoa kwa nguvu tawala zilizokuwapo, vikajipambanua kwamba vinalenga kujenga demokrasia na kusimamia haki, lakini sasa vinafufua mfumo mfu wa chama kimoja.

Vyama hivyo vimekuwa vinafanya mbinu chafu zenye lengo la kuunyamazisha umma, kuiminya demokrasia na kukandamiza haki za msingi za binadamu. Sehemu nyingine viongozi wapinzani kutupwa gerezani kwa visingizio mbalimbali.

Kuna ushahidi kuwa katika nchi nyingine, mahakama haifanyi kazi kwa misingi ya kisheria, mabunge ni butu na vyombo vya habari vimenyamazishwa isipokuwa vile vinaimba ‘wimbo ni upendao.’

Baadhi ya viongozi wa vyombo vya habari au waandishi wa habari wanaochokonoa yaliyoko chini ya zulia, ama wako kifungoni au wanaishi uhamishoni.

Ni kawaida katika nchi zinazoongozwa na vyama vya Mapinduzi na kidemokrasia, huwa vinafanya chaguzi za kuzuga (window dressing) na kuingilia utendaji wa tume za uchaguzi.

Nigeria, Ghana, Zambia, Malawi angalau zimeonesha mfano kwamba inawezekana kubadili uongozi wa nchi kwa njia ya sanduku la kura. Gambia inaongozwa na Muungano wa vyama vya siasa baada ya kukivunja nguvu chama tawala cha Yahya Jameh, Alliance for Patriotic Reorientaion and Construction ambacho kilikuwa madarakani kwa miaka 22.

Lakini pia kuna vilivyopigania uhuru ambavyo vimepoteza nguvu, Kenya African National Union (KANU), viongozi wake wamejiunga katika mkusanyiko wa vyama maslahi uitwao Jubilee.

United National Independence Party (UNIP) cha Dk. Kanneth Kaunda wa Zambia, Chama cha Malawi Congress Party, cha Dk. Kamuzu Banda na Uganda  People’s Congress (UPC) cha Dk. Milton Obote, ni kama vimepotea katika ramani za siasa, vimepoteza mvuto kwa wananchi.
Kwa hiyo, vyama vya upinzani katika Afrika na hasa hapa Tanzania, vinapaswa kutambua kwamba Umoja ni Nguvu na ili viweze kuleta mabadiliko ya kweli, vinapaswa kuunda umoja, bila hivyo, havitaweza kutwaa madaraka.

Ujuzi umeonesha kwamba vyama tawala hushinda uchaguzi kwa kubebwa ama na Katiba mbaya, vyombo vya dola na mahakama. Lakini wengine wanasema Katiba nzuri pekee haitoshi kama wanaopewa madaraka na kuapa kuilinda Katiba, wakishapata madaraka, wanakengeuka wanaiweka Katiba pembeni.

Kenya ambayo ilitoa mfano bora wa Katiba na heshima ya mahakama, imerudi nyuma baada ya wabunge wa Jubilee kwa kuangalia maslahi yao, wametumia wingi wao katika Bunge na kupitisha sheria mbaya inayohusiana na uchaguzi.

Hadi hapo itakapojengeka mifumo mizuri ya Utawala Bora, ikiwa ni pamoja na kuheshimu nguzo kuu tatu za utawala, Afrika haitaweza kuwa na Serikali zinazojali maslahi

ya wananchi, kuheshimu haki zao na kuimarisha utawala wa sheria.

Nchi zenye vyama vya siasa vya kidemokrasia kwa majina, viko mbali sana na misingi ya demokrasia. Vingine vinajiita kuwa ni vyama vya Kimapinduzi, lakini kiitikadi ni vyama vya kihafidhina.

Viongozi wa vyama tawala wanasimama majukwaani na kusema wapinzani wana uchu wa madaraka, lakini ni wao ambao wamekuwa ving’ang’anizi wa madaraka.

Katiba zimeweka vipindi vya kukaa madarakani, ikiwa ni pamoja na kutaja ukomo wa umri wa mtu kugombea urais, lakini wenye uchu wa madaraka, hubadili Katiba na kutaka kuwa Rais wa maisha. Hii inatokana na uoga kwamba uongozi wa chama kingine utawaadhibu viongozi waliofanya madudu, wezi na wabadhirifu wa rasilimali na mali ya umma.

Waafrika inaonekana kuwa ni waoga, wanaogopa kutoa madaraka kwa vyama ambavyo havijawahi kuongoza nchi. Wanasiasa wengi wanaamini katika usemi wa ‘jini likujualo halikuli likakwisha.’

Afrika itatokaje kwenye mduara huu wa vyama vyenye nguvu kuwadanganya wananchi kwamba ndivyo vyenye mamlaka ya kuwaweka viongozi madarakani.

Watu wengi wanaamini kwamba vyombo vya habari ndivyo vyenye dhima ya kuwajuza nani anafanya nini na wapi. Nani ni mkweli na nani ana maslahi mapana ya nchi. Lakini nafasi ya vyombo vya habari kama ‘mbwa mlinzi’ si tu kwamba mbwa huyo amefungwa mnyororo, pia amezibwa mdomo asiweze kubweka.

Serikali za Kiafrika hazipendi kuanikwa, wanahabari wanaoandika habari za uchunguzi, wanakutana na vikwazo vingi, hutishwa na mara nyingine kuuawa.

Ni jukumu la vyombo vya habari kuchunguza tuhuma za rushwa au makosa ya kiutendaji na udhaifu katika kufanya uamuzi. Lakini S Serikali za Kiafrika hazipendi kuanikwa.

Viongozi wanaamini kwamba kuandikwa mabaya na udhaifu mara kwa mara, sawa na kuichimba Serikali na inaweza kuleta madhara kwa nchi.

Ipo dhana kwamba baada ya uchaguzi, vyama pinzani viache malumbano ya kisiasa na kuungana katika kuzisaidia Serikali kutekeleza majukumu yake.

Lakini wenye kupenyeza dhana hii wanasahau kwamba vyama pinzani ni kama timu shindani za mpira. Timu moja ikikosea, inapoteza ushindi. Vikiacha kuikosoa Serikali, itasinzia.

Dhima ya upinzani ni kuwafanya viongozi wa Serikali kutobweteka, kuwa makini katika uamuzi wao na utendaji. Kiongozi akikosea, anaelezwa kosa lake mara moja na ikibidi anawajibishwa.

Bila kuwapo upinzani makini, Serikali inakuwa goigoi, inafanya vile inavyotaka hata kama inakiuka misingi ya uwepo wake na wajibu wake kwa wananchi. Hii ndio maana ya siasa za ushindani.

Serikali za Kiafrika zingependa sana upinzani uliodorora, unaosinzia, ili wananchi wasiambiwe upungufu wake. Mara nyingine viongozi wa upinzani, kwa mfano Uganda na Zimbabwe, wamekuwa wanasumbuliwa sana ili wasiwe na muda wa kutulia na kupanga mikakati na mbinu za kuikosoa Serikali.

Mambo kama haya yanaonesha udhaifu wa watawala katika kujibu hoja za wapinzani, badala yake wanatumia nguvu. Kiongozi mzuri ni msikivu, anasikiliza na kuzifanyia kazi taarifa na hoja za wapinzani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles