25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Samuel Sitta azikwa kitaifa Urambo

Familia ya aliyekuwa Spika mstaafu wa Bunge la 9, Samuel Sitta, wakiomboleza wakati jeneza lenye mwili wake likishushwa kaburini wakati wa mazishi yaliyofanyika eneo la Majengo, Urambo mkoani Tabora jana.
Familia ya aliyekuwa Spika mstaafu wa Bunge la 9, Samuel Sitta, wakiomboleza wakati jeneza lenye mwili wake likishushwa kaburini wakati wa mazishi yaliyofanyika eneo la Majengo, Urambo mkoani Tabora jana.

Na MURUGWA THOMAS-URAMBO

ALIYEKUWA Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samuel Sitta, amezikwa kwenye makaburi ya Ullasa, wilayani Urambo, mkoani Tabora, huku Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akitokwa machozi wakati akielezea alivyopokelewa naye alipokuwa mkuu wa wilaya hiyo.

Kiongozi mwingine aliyebubujikwa na machozi ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, ambaye alitumia muda mwingi kumfariji mjane wa marehemu, huku akisema kuwa sasa Mama Margaret Sitta amekuwa mke wa Bwana Yesu.

Katika maziko hayo, ibada ya misa imeongozwa na Askofu Mkuu, Dk. Alex Malasusa wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Waziri Mkuu Majaliwa alibubujikwa na machozi wakati akitoa salamu za rambirambi za Serikali na kueleza kuwa wakati akiwa mkuu wa wilaya ya Urambo chini ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete, alipokewa na Samuel Sitta.

Sauti ya Waziri Mkuu Majaliwa ilianza kupooza na mara baada ya kueleza kuwa “Sitta amechangia mimi kuingia Serikalini,” alianza kutokwa na machozi.

Alisema wakati huo walikuwa wakikutana mara kwa mara na Sitta na kuzungumza masuala mabalimbali na kumuusia kutoingilia migogoro ya mtu kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kumfanya kufika mbali na kuwa kiongozi bora.

“Marehemu Sitta nilikuwa nikikutana naye ghorofani (nyumbani kwa Sitta) na kujadiliana naye mambo mbalimbali na mara zote alinisisitiza kutoingilia mambo au migogoro ya mtu na mtu, kwani ndiyo njia ya kufanikiwa na kuwa kiongozi bora, lakini pia alinieleza nikiwa kiongozi na nikabahatika kutatua mgogoro nisipendelee yeyote, aliniasa kuchapa kazi, kwani ndicho kigezo cha kuwa kiongozi mzuri,” alisema.

Alimtaja Sitta kama mpenda amani, muwazi na wakati wote alipenda kusema ukweli na kuhimiza maendeleo kwa watu wote, bila kujali itikadi za dini na vyama vyao.

Naye Spika wa Bunge, Job Ndugai, akitoa salamu zake alisema jukumu alilowaachia marehemu Sitta ni kusukuma maendeleo ya watu wa Wilaya ya Urambo ambako ametoka ili kumuenzi, lakini aliahidi kuthamini mchango wake alioutoa kwa Bunge.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, ambaye aliongea kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alimuelezea Sitta kama kiongozi jasiri, mpole na mnyenyekevu.

Alisema kutokana na ujasiri aliokuwa nao marehemu Sitta wakati wa uhai wake, aliweza kupanda mbegu ndani ya CCM ambayo uzao wake unatoa matunda sasa, akimaanisha yeye na vijana wengine walioshika nyadhifa za juu Serikalini.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, ambaye aliwakilisha kambi rasmi ya upinzani Bungeni, alisema kumuenzi Sitta ni kuambatana na kukamilisha mchakato wa katiba mpya, ambao marehemu aliusimamia.

Mbowe alitumia nafasi hiyo kuwaomba viongozi, wananchi na watendaji wote wa Serikali kuwa wanyenyekevu wakati wa utendaji kazi zao na kuwa hofu kama ilivyokuwa wakati wa kuomboleza.

“Utaona leo hata Polisi ambao tumekuwa tukikwaruzana nao askari wake wanaonekana wakiwa watulivu na wasikivu msibani hapa, msiba huu uwe funzo kwetu sote kujenga mahusiano mema na tuijenge nchi hii,” alisema.

Maziko hayo yalihudhuriwa pia na Naibu Spika Tulia Ackson, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Mchemba, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na naibu wake, Dk. Hamis Kigwangala, Spika Mstaafu wa Kwanza wa Bunge la Afrika, Gertrude Mongella pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mohamed Aboud.

Mbali ya hao, wengine waliohudhuria ni Profesa Ibrahim Lipumba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida, aliyekuwa mbunge wa Kahama, James Lembeli pamoja na viongozi kutoka mikoa ya Kigoma na Shinyanga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles