27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

SAMMATA , NYOTA WALIOBEBA ROHO YA AFRIKA MASHARIKI AFCON 2019

NA SOSTHENES NYONI KWA MSAADA WA MTANDAO

MATAIFA manne ya Afrika mashariki yatashiriki fainali  zijazo za  mataifa ya Africa (Afcon), zitakazoanza kutimua vumbi nchini Misri, Juni 21 mwaka huu.

Mataifa hayo ni Uganda, iliyofuzu baada ya kuongoza kundi lake huku Kenya, Tanzania na Burundi zikifuzu baada ya kukamata nafasi ya pili.

Tofauti na mashindano yaliyopita, safari hii nchi zitakazoshiriki michuano hiyo ni 24, baada ya Shirikisho la Soka Afrika(Caf), kuongeza idadi kutoka16 ya awali.

Mara ya mwisho, Afrika Mashariki iliwakilishwa na Kenya na Rwanda, mashindano yaliyofanyika nchiniTunisia, mwaka 2004, ambapo ziliondolewa hatua ya makundi.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa nchi nne za  ukanda huo kushiriki Afcon kwa pamoja.

Kuelekea fainali hizo, MTANZANIA litakuletea nyota wa mataifa hayo manne ambao watabeba dhamana katika vikosi vya nchi zao Afcon.

Mbwana Samatta

Samatta(27), ni mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania na klabu ya Genk nchini Ubelgiji.

Samatta pia ni nahodha wa timu ya  Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

Kabla ya kujiunga na Genk, alikuwa katika kikosi cha timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC).

Akiwa na Mazembe, mwaka 2015 alitwaa Ligi ya Mabingwa Afrika, akifunga mabao saba na kuibuka mfungaji bora wa mashindano hayo.

Januari mwaka 2016, alikuwa mchezaji wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa mwaka wa Caf anayechezea ndani ya Afrika.

Sammata alitwaa tuzo hiyo, baada ya kumshinda, kipa Robert Kidiaba ambaye pia alikuwa akiidakia Mazembe.

Simon Msuva

Ni winga wa kimataifa wa Tanzania anayeichezea Difaa El Jadida ya Morocco

Msuva(26), aliwahi kuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom, msimu wa 2014-2015, akifunga mabao 17, akiwa na kikosi cha Yanga.

Aliibuka mfungaji bora kwa mara nyingine wa ligi hiyo, msimu wa 2016-2017, baada ya kupachika mabao 18.

Pia aliibuka  Mfungaji Bora wa michuano ya Kombe la Mapinduzi lililofanyika mwaka 2015, akifunga mabao manne.

Mwanzoni mwa mwaka wa 2017, aliingia mkataba kuichezea klabu ya Al Jadida ya nchini Morocco, ambapo amezidi kuwa moto katika upachikaji wa mabao. Anatarajia kuingoza Taifa Stars sambamba na Samatta.

Victor  Wanyama

Ni kiungo wa kimataifa wa Kenya anayekipiga Tottenham  inayoshiriki Ligi Kuu ya England.

Mbali na kuingoza timu ya Taifa ya Kenya inayojulikana kwa jina la utani Harambee Stars Afcon akiwa nahodha, ndiye Mkenya wa kwanza kufunga bao katika Ligi ya Mabingwa ya Ulaya, wakati huo akiichezea Celtic iliposhinda mabao 2-1 dhidi ya Barcelona, mwaka 2012.

Alijiunga na Ligi Kuu England, mwaka 2013, akiichezea  Southampton kwa dau la pauni milioni 12.5 na kumfanya awe mchezaji ghali zaidi kuwahi kuuzwa na klabu ya Scotland.

Wanyama ameichezea Harambee Stars  zaidi ya mechi 30.

Hivi karibuni, klabu yake ya Tottenham ilimaliza nafasi ya pili Ligi ya Mabingwa Ulaya, nyuma ya Liverpool iliyotwaa ubingwa.

Michael Olunga

Ni mchezaji wa kulipwa wa Kenya  anayeichezea klabu ya Kashiwa Reysol ya  Japan.

Olunga(25) alianza maisha yake ya soka  katika timu ya Liberty Academy iliyokua inashiriki madaraja ya chini nchini Kenya.

Aliifungia timu hiyo mabao 32, akiisaidia kumaliza msimu huo bila kufungwa.

Alijiunga na klabu ya Tusker kwa mkataba wa mwaka mmoja, kabla ya kusajiliwa na Thika United.

Baadaye alijiunga na mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya, Gor Mahia ambapo alimaliza msimu huo na mabao19 na kuisaidia timu hiyo kushinda taji la 15.

Februari 17,  2016, Olunga alijiunga na klabu ya Djurgadens IF,  kwa kandarasi ya miaka minne kabla ya mwaka 2017 Olunga kujiunga na klabu ya China ya  Guizhou Zhicheng.

Septemba 2017, Olunga alijiunga kwa mkopo klabu ya La Liga ya Girona.

Akiwa na klabu hiyo ya Hispania alifunga mabao matatu ‘Hat-trick’ katika mchezo dhidi ya Las Palmas.

Agosti 2018, alijiunga na  Kashiwa Reysol anayoichezea hadi sasa.

Emmanuel Okwi

Ni mshambuliaji wa kimataifa wa  Uganda na klabu ya  Simba inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Okwi(27), kabla ya kujiunga na Simba aliwahi kuitumikia  SC Villa ya nchini kwake Uganda.

Akiwa Simba aliivutia klabu ya Etoile du Sahel  ya Tunisia ambayo ilimsajili kwa  dau lililovunja rekodi ya Ligi Kuu  Tanzania Bara, Dola 300,000.

Disemba 2013, alirudi SC Villa ya Uganda baada ya kushindwana na Etoile kabla ya kujiunga na Yanga na kisha kurejea Simba.

Denis Onyango

Ni kipa wa kimataifa wa Uganda na klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Pia ni nahodha wa timu yake ya taifa Uganda ambayo  pia inafahamika kwa jina la utani Cranes.

Onyango(34),alianza maisha yake ya soka nchini Uganda kabla ya kuelekea  Ethiopia katika klabu ya Saint George na kisha Superport United, Mpumalanga Black Aces na Mamelodi Sundowns, zote za Afrika Kusini.

Akiichezea Mamelodi Sundowns, alishinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika  mwaka 2016 na kushiriki Kombe la Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) la klabu.

Amewahi  kuchaguliwa mchezaji bora wa mwaka wa Afrika.

Pia aliorodheshwa katika orodha ya makipa10 bora duniani mwaka 2016, iliyoandaliwa na Shirikisho la Kimataifa la Historia ya Soka na Takwimu (IFFHS).

Fiston Abdul Razak

Ni mchezaji wa kimataifa wa Burundi anayeichezea klabu ya JS Kabylie.

Razak(26), kabla ya kujiunga na JS Kabylie, alizichezea klabu za LLB Académic FC, Rayon Sports, CSMD Diables Noirs, Sofapaka F.C ya Kenya , Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini , Bloemfontein Celtic F.C, C.D. Primeiro de Agosto ya Angola na Al-Zawra’a SC.

Saido Berahino
Ni mchezaji nyota wa kimataifa wa  Burundi.

Mshambuliaji huyo amewahi kukipiga Stoke City, West Bromwich, Northampton Town, Brentford na Peterborough United za England.

Ni mchezaji muhimu katika kikosi cha Burundi ambacho pia kinafahamika kwa jina la utani Intamba murugamba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles