27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Samia akumbuka machungu uchaguzi 2015

Elizabeth Hombo – Dar es Salaam

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka wanachama wa CCM kutorudia makosa waliyoyafanya katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kwa kujipiga wenyewe na baadhi ya majimbo kuchukuliwa na upinzani.

Vilevile amewaonya wanachama wa chama hicho walioanza kujipitisha katika majimbo mbalimbali kutengeneza mazingira ya kupitishwa kuwania nafasi ya ubunge.

Samia ambaye pia ni mlezi wa CCM kwa Mkoa wa Dar es Salaam, aliyasema hayo jana katika maadhimisho ya miaka 43 ya kuzaliwa chama hicho tawala kwa mkoa huo.

Maadhimisho hayo katika Mkoa wa Dar es Salaam yalifanyika ikiwa ni mwendelezo wa maadhimisho yanayofanyika katika mikoa mbalimbali nchini.

“Katika uchaguzi uliopita hatukupigwa, lakini tulijipiga wenyewe kwa sababu ya tamaa zetu, sasa kwa uchaguzi wa mwaka huu kila mmoja akae kwenye mstari wake ili ile fimbo isitupige tena,” alisema Samia.

Kuhusu walioanza kujipitisha majimboni, alisema CCM ina taratibu zake za kusimamia uchaguzi na kwamba muda ukifika wote wataruhusiwa kutangaza nia na kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali.

“Nimepata fununu na nina majina ya baadhi ya watu wameanza kujipitisha huko majimboni na tayari wameanza kutoa takrima, chama kina jicho kali na tayari kimewaona.

“Kama wewe ni mchezaji mzuri subiri filimbi ipigwe halafu uingie uwanjani kucheza, sio unaanza kucheza peke yako, filimbi ikipigwa mpira unakukuta uko golini, unatia. Sasa ninawaomba mfuate kanuni na taratibu za chama.

“Na anayecheza rafu tutamuona na tayari tumewaona watu wameanza kujipeleka majimboni mapema, kuna wabunge wa eneo husika na wameanza kazi yao kwa muda mrefu sasa, unapoanza kujipitisha sio sawa,” alisema Samia.

Katika hatua nyingine, Samia ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, aliwaonya viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama hicho wanaoshiriki kuwasimamisha wanachama kinyume na taratibu za chama hicho tawala.

“Viongozi wa ngazi mbalimbali mnashiriki kuwasimamisha uanachama kwa chuki kwa vile tu wameona ni tishio akigombea nafasi fulani, namna ya kuchukuliana hatua ipo kwenye kanuni.

“Na nilikuwa mkali kwa kamati ya siasa kwamba wasitupunguzie mtaji wa watu mapema kwa sababu kila mnayemfukuza ana ndugu, jamaa na marafiki watakwenda kumuunga mkono huko.

“Uchaguzi uliopita ndio fimbo tulijipiga wenyewe watu wakakatwa tu ovyo, wakanuna wakaenda upande wa pili.

“Chuki baina yetu ndio iliyosababisha tukajipiga wenyewe 2015, watu mlichukiana, mkazushiana mambo ambayo hata hayapo na unakuta huyo anayekatwa ndio mzuri kuliko yule anayeachwa,” alisema Samia.

Alisema siku zote anayetoa nafasi ya uongozi ni Mwenyezi Mungu na mtu hata akimzuia mwenzake hatafanikiwa.

“Tupendane na twendeni kwenye Uchaguzi Mkuu tukiwa wamoja na kufarakana miongoni mwetu ni chanzo cha kuwapa ushindi upinzani,” alisema Samia.

Alisisitiza kuwa mtu anayefaa kugombea apewe nafasi badala ya kuondolewa sifa au kuvuliwa uanachama ili mradi asipate nafasi kwa sababu tayari viongozi wana watu wao.

“Unakuta mtu anafaa kugombea, lakini anaandikiwa sifa mbovu halafu anaenguliwa, mwenendo huu hautupeleki kuzuri,” alisema Samia.

Pia alizungumzia kuhusu uandikishaji wa daftari la wapigakura ambao kwa Mkoa wa Dar es Salaam unaanza leo, akiwataka viongozi wa chama hicho kuhakikisha katika maeneo yao watu wanakwenda kujiandikisha.

“Kila mtu ahakikishe katika eneo lake watu wamekwenda kujiandikisha, tuhimizane katika mitaa yetu na kuwaelimisha wanachama wetu,” alisema Samia.

CCM DAR KUMCHUKULIA FOMU JPM  

Awali Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba alisema mkoa huo utatoa Sh milioni 1 kwa Rais Dk. John Magufuli kuchukulia fomu ya kugombea urais.

Mwanasiasa huyo mkongwe na aliyepata kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, alisema chama hicho hakina cha kumlipa Rais Magufuli kwa sababu ameufanyia mambo makubwa Mkoa wa Dar es Salaam.

“CCM Mkoa wa Dar es Salaam tunatangaza kwamba mgombea wetu ni Rais Magufuli. Tutatoa Sh milioni 1 kwa ajili ya kumchukulia fomu ya urais.

“Makamu wa Rais, tunakuomba utufikishie salamu hizi kwa Rais Magufuli kwamba asihangaike na fedha ya kuchukulia fomu, sisi tutatoa,” alisema Kamba.

Alisema wanamshukuru Rais Magufuli kwa kuuletea Mkoa wa Dar es Salaam maendeleo makubwa ambayo yataufanya kuwa kitovu cha biashara hapa nchini.

Aidha, alisema chama hicho kitatoa Sh milioni 100 kuimarisha mashina ya chama hicho.

“Fedha hizo Sh milioni 100 ziko tayari na zitaanza kutolewa baada ya utaratibu unaoandaliwa kukamilika,” alisema Kamba.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliwataka wanachama wa CCM na wananchi wa mkoa huo kujitokeza leo katika uandikishaji wa daftari la wapigakura.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles