27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Samatta gumzo Afrika

SAMATANA ZAINAB IDDY, DAR ES SALAAM

SALAMU za pongezi zimezidi kumiminwa kwa mshambuliaji raia wa Tanzania, Mbwana Samatta, ambaye juzi alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani.

Samatta ambaye anahusishwa kujiunga na KRC Genk ya Ubelgiji akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ameishtua dunia baada ya kuweka historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kutwaa tuzo hiyo.

Katika tuzo hizo zilizofanyika mjini Abuja, Nigeria, Samatta alimbwaga kipa wa TP Mazembe, Robert Kidiaba, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na mshambuliaji raia wa Algeria anayekipiga kwa mkopo Etoile du Sahel ya Tunisia akitokea Al Sadd ya Qatar, Baghdad Boundjah.

Samatta aliyeambatana na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Selestine Mwesigwa nchini Nigeria, alikuwa na mchango mkubwa katika klabu yake ya TP Mazembe kwa kuiwezesha kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika mwaka jana.

Mshambuliaji huyo wa Taifa Stars aliifungia klabu yake ya TP Mazembe mabao saba sawa na mshambuliaji wa El Merreikh ya Sudan, Bakri Al-Madina na kuibuka kinara wa mabao.

Pierre-Emerick Aubameyang, raia wa Gabon anayekipiga Borussia Dortmund ya Ujerumani alitangazwa Mwanasoka Bora wa Afrika 2015 na kuzima ndoto za kiungo wa Manchester City ya England na raia wa Ivory Coast, Yaya Toure, kutwaa tuzo hiyo kwa mwaka wa tano mfululizo.

Nafasi ya tatu katika tuzo ya Mwanasoka Bora Afrika ilimwendea mshambuliaji wa Swansea City ya England raia wa Ghana, Andre Ayew.

Washindi wa tuzo mbalimbali za mwaka kwenye mabano ni Victor Osimhen (chipukizi bora), Herve Renard (kocha bora), Bakary Gassama (refa bora), Ivory Coast (timu bora ya taifa), TP Mazembe (klabu bora), Cameroon (timu bora ya taifa ya wanawake), Oghenekaro Etebo (kipaji cha mwaka) na Gaelle Enganamouit (mwanasoka bora wa kike).

Samatta aliyezaliwa Januari 7, 1992, jijini Dar es Salaam, aliwahi kuichezea klabu ya African Lyon katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2008-2010 na kujiunga na Simba 2010-2011 na baadaye kujiunga na TP Mazembe inayomilikiwa na tajiri, Moise Katumbi.

Licha ya Samatta kutwaa tuzo hiyo, baadhi ya mitandao mbalimbali duniani imekuwa ikimtambulisha nyota huyo kuwa ni raia wa Botswana, Tunisia na DRC Congo.

Salamu za Rais Magufuli

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, amemtumia salamu za pongezi Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, kufuatia mchezaji Mbwana Samatta wa timu ya taifa kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza barani Afrika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, Rais Magufuli amemtaka Waziri Nape amfikishie Samatta salamu zake za pongezi.

Rais amesema tuzo hiyo imemjengea heshima na kuleta sifa kwa Mbwana Samatta mwenyewe, wanasoka wa hapa nchini na Tanzania kwa ujumla katika medali ya soka kimataifa.

Aidha, Rais Magufuli amewasihi wachezaji wote wa soka na wadau wa mchezo huo kuongeza juhudi za kuuendeleza mchezo huo ili upige hatua zaidi kimaendeleo.

Salamu za Rais wa TFF

Naye Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Jamal Malinzi, amempongeza Samatta kwa ushindi huo wa kihistoria ukimfanya kuwa mchezaji wa kwanza kwa Ukanda wa Afrika Mashariki kushinda tuzo kubwa barani Afrika.

Pamoja na kushinda tuzo hiyo, Samatta pia amejumuishwa katika kikosi bora cha wachezaji wa Afrika kwa mwaka 2015 sambamba na Robert Kidiaba (Congo DR), Sergie Aurier (Ivory Coast), Aymen Abdenmor (Tunisia), Mohamed Meftah (Algeria), Sadio Mane (Senegal), Yaya Toure (Ivory Coast), Yacine Ibrahim (Algeria), Andrew Ayew (Ghana), Pierre-Emercik Aubameyang (Gabon) na Baghdad Bounedjah (Algeria).

Mshambuliaji huyo aliyeambatana na Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine, walitarajiwa kuwasili nchini jana saa 8 usiku kwa Shirika la Ndege la Ethiopia.

 Kocha wa Yanga

Kocha mkuu wa Yanga, Mholanzi Hans Van Pluijm, naye amempongeza Samatta kwa kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani.

“Napenda kumpongeza Samatta kwa kutwaa tuzo, hii inaweza kuwahamasisha wachezaji wengine wa ndani kubadili mwelekeo wao na kuwa na mawazo ya uchezaji wa kimataifa.

“Hii itawezesha wachezaji wengi wa Tanzania kupata mafanikio, si tu kwa manufaa yao binafsi lakini pia kwa timu yao ya taifa hususani michuano ya kimataifa,” alisema Pluijm.

Salamu za Kibadeni

Kocha mkuu wa JKT Ruvu, Abdallah ‘King’ Kibadeni, amesema mafanikio anayoyapata mchezaji wa kimataifa wa Tanzania anayecheza klabu ya TP Mazembe ni mfano wa kuigwa kwa wachezaji wengine wa Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Kibadeni ambaye pia ni mkurugenzi wa ufundi wa timu ya soka la Tanzania, Taifa Stars, amesema mafanikio ya Samatta ni heshima kwa soka la Tanzania.

“Ni muda wa wachezaji wengine kwa Tanzania kuwa na uchungu pamoja na wivu wa mafanikio kwa Samatta, hivi sasa wapo wachezaji wengi waliocheza soka kwa muda mrefu lakini hawakufika hatua aliyoifikia.

“Kikubwa kilichomuinua Samatta ni kujitambua yeye ni nani, anafanya nini kwa wakati upi, lakini pia heshima na kukubali kukosolewa ni vitu vilivyochangia kutimiza ndoto zake, jambo ambalo kwa wachezaji wengine ni tofauti hivyo ni muda wa wengine kuiga kutoka kwake,” alisema Kibadeni.

Wafaransa wamfuata Samatta Dar

Katika hatua nyingine, Klabu ya Nantes inayoshiriki Ligi Kuu nchini Ufaransa, imetuma wajumbe wake nchini kuzungumza na Samatta.

Taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana kutoka kwa mtu wa karibu na mchezaji huyo, zinasema kuwa  ujumbe huo unatarajiwa kukutana na mchezaji pamoja na meneja wake, Jamali Kisongo kwa ajili  ya kumalizana kila kitu na pande hizo.

Klabu hiyo ya Ufaransa ina nia ya kupata saini ya Samatta katika dirisha dogo la usajili ambalo limeshafunguliwa barani Ulaya tangu Januari Mosi mwaka huu.

Kwa mujibu wa mwakilishi wa Samatta, Nantes inataka kila kitu kimalizike kabla ya Januari 20.

Nantes inamtaka Samatta kwa ajili ya kufufua safu yake ya ushambuliaji ambayo imekuwa butu ikifunga mabao 14 msimu huu ambayo ni idadi ndogo zaidi ukiondoa timu ya mwisho kwenye msimamo, Troyes.

Timu hiyo inashika nafasi ya 13 katika msimamo wa ligi hiyo wenye timu 20 baada ya kucheza mechi 19 na kujikusanyia pointi 24.

Mwanasoka Bora wa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani

2015      Mbwana Samatta (Tanzania – TP Mazembe)

2014      Firmin Ndombe Mubele (DR Congo – Vita Club)

2013      Mohamed Aboutrika (Misri – Al-Ahly)

2012      Mohamed Aboutrika (Misri – Al-Ahly)

2011      Oussama Darragi (Tunisia – Espérance)

2010      Ahmed Hassan (Misri – Al-Ahly)

2009      Tresor Mputu (DR Congo – TP Mazembe)

2008      Mohamed Aboutrika (Misri – Al-Ahly)

2007      Amine Chermiti (Tunisia – Etoile du Sahel)

2006      Mohamed Aboutrika (Misri – Al-Ahly)

2005      Mohamed Barakat (Misri – Al-Ahly)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles