28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

SAKATA LA MCHANGA: MAPYA YAIBUKA IKULU

Rais Dk. John Magufuli akizungumza na Mwenyekiti wa Barrick Gold Corporation ya Canada, Profesa John L. Thornton. PICHA NA JUMANNE JUMA

 

ARODIA PETER Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambaye ni mmiliki mkubwa wa Kampuni ya Acacia Mining Limited, Profesa John Thornton wamekubaliana kuunda timu mbili za majadiliano.

Timu hizo zitahusisha Serikali ya Tanzania na wawakilishi wa Kampuni ya Barrick kutoka Canada na Marekani na watafanya majadiliano ambayo yatahusu namna ya kufikia mwafaka katika suala la kusafirisha mchanga wa dhahabu (makinikia) nje ya nchi kwa faida ya pande zote mbili.

Mwenyekiti huyo wa Barrick amekuja nchini siku chache baada ya ripoti ya kamati ya pili iliyoundwa na Rais Dk. Magufuli kusema Kampuni ya Acacia ni hewa kwa sababu haina usajili wowote nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa pamoja na sauti ya video ya Rais Dk Magufuli iliyosambazwa jana, timu hizo zitakutana ndani ya wiki moja hadi mbili kuanzia sasa.

Akiweka wazi mazungumzo yake na bosi huyo wa Barrick, Rais Dk. Magufuli alisema baada ya ripoti ya pili kusomwa, Balozi wa Canada hapa nchini, Ian Myles aliomba kuonana naye pamoja na mwenyekiti huyo wa Barrick.

Alisema katika mazungumzo hayo Profesa Thornton alimweleza Rais Magufuli kuwa amesikia ripoti hiyo na kwamba wao ndio wenye hisa kubwa kuliko Kampuni ya Acacia kwani wana hisa asilimia 64.

“Profesa Thornton amenieleza kwamba wao ndio wana hisa kubwa asilimia 64 na wale wengine waliobaki ndio wana hisa hizo zilizobaki, kwa hiyo ikitokea matatizo yoyote katika migodi hii wao ndio wanaathirika zaidi.

“Tukamwambia kama wewe ndio mwenye hisa ya asilimia 64 unasemaje, uamuzi wetu ndiyo huo kwamba sisi lazima tupate haki yetu kwa sababu tumenyonywa mno tumechezewa mno.

“Akasema yuko tayari kuingia kwenye mazungumzo na ataleta timu yake kutoka Canada na Marekani kwa sababu yeye anaishi Canada na Marekani. Hivyo na sisi tutakuwa na timu yetu, bahati nzuri tulikuwa na Profesa Palamagamba Kabudi (Waziri wa Katiba na Sheria).

“Timu hiyo itapitia mapendekezo yote na amekubali chochote ambacho kitakuwa kimekubalika watalipa.

“Akasema ni bahati mbaya wanatubu kwa haya yaliyotokea, nikamwuliza jina lako ni nani akasema ni John na mimi nikamwambia langu ni John kwa hiyo hapo tutaishi kwenye makubaliano.

“Kwa hiyo amesema kwa wiki moja au mbili tutakapowahitaji waje waingie kwenye mazungumzo na ametoa mfano kuwa amehusika hivyo hivyo katika nchi ya Dominica ambako nako walikuwa wanachimba dhahabu, viongozi wa kule wakasema wanaibiwa ikabidi waingie kwenye mazungumzo watengeneze mkataba mwingine.

“Pia akaniambia kwamba walifanya hivyo Saudi Arabia nako walikuwa wanadhulumiwa Serikali ya kule ikawa wazi na baada ya makubaliano sasa wana hisa asilimia 50  kwa 50.”alisema Dk. Magufuli na kuongeza.

“Hivyo akasema yaliyofanyika Dominica na Saudi Arabia hayana ugumu kufanyika Tanzania. Ameshangaa kwamba inawezekana wale wengine walikuwa wanadanganywa na wale wenye hisa ndogo na akasema sisi tuzungumze na Barrick si mtu mwingine na mimi nikawaambia hatuwezi kuzungumza na Acacia kwa sababu hawana leseni,”alisema Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine, taarifa ya Msigwa alisema  pamoja na Profesa Thornton kukubali kulipa fedha zinazodaiwa, pia amekubali kushirikiana na Tanzania kujenga mtambo wa kuchenjua dhahabu (smelter) hapa nchini.

Wakati akiwasilisha ripoti ya pili ya uchunguzi wa mchanga wa dhahabu Jumatatu wiki hii, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Nehemiah Osoro alisema licha ya Acacia kutosajiliwa, kampuni hiyo pia haina hati ya utambuzi (certificate of compliance) kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni, Sura ya 212.

“Kamati pia imebaini kuwa Kampuni ya Acacia Mining Plc, ambayo inajinasibisha kuwa mmiliki wa makampuni ya Bulyanhulu Gold Mines Ltd, North Mara Gold Mine Ltd na Pangea Minerals Ltd, haikuwahi kuwasilisha nyaraka wala taarifa yoyote kuonesha kuwa kampuni hiyo ni mmiliki wa makampuni hayo wala kuwa na hisa katika makampuni hayo.

“Kwa kuwa Acacia Mining Plc haina usajili wala utambuzi wa kisheria nchini Tanzania, haina sifa ya kupata leseni, kuchimba wala kufanya biashara ya madini nchini Tanzania,”alisema Profesa Osoro.

Aidha kamati hiyo ilisema kuna udanganyifu katika uuzaji na usafirishaji wa makinikia nje ya nchi ambako husafirishwa kwa madai ya kwenda kuchenjuliwa, lakini ukweli ni kwamba husafirishwa yakiwa tayari yameshauzwa.

Kamati pia ilibainisha kuwa kampuni za Bulyanhulu na Pangea ndizo wazalishaji na wauzaji wa makinikia nje ya nchi.

Taarifa ya kamati ilisema makinikia hayo hupelekwa nchi za China, Japan na Ujerumani, yakiwa kwenye makontena yenye urefu wa futi 20 na wastani wa tani 20 kila moja.

Acacia na taarifa

Taarifa iliyopatikana katika tovuti ya Kampuni ya Acacia jana mchana ilisema imeona taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais Ikulu baada ya kikao kati ya Rais Dk. John Magufuli na Profesa John Thornton Mwenyekiti Mtendaji wa Barrick Gold Corporation (“Barrick”), ambaye ni mwanahisa mkubwa wa Acacia.

Taarifa hiyo ilisema, Barrick na Serikali ya Tanzania wamekubaliana kuingia kwenye mazungumzo ili kufikia mwafaka kwenye suala la katazo la kusafirisha makanikia nje nchi pamoja na namna ambavyo Acacia inaweza kufanya kazi Tanzania kwa siku za usoni.

“Tutatoa taarifa zaidi kupitia mkutano wetu tutakaoufanya kwa njia ya mtandao Alhamisi Juni 15  (leo) saa 3 asubuhi kwa saa za Uingereza,” inasomeka taarifa hiyo kwenye tovuti yake jana.

Takukuru na watuhumiwa

Pamoja na hilo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imeanza kuwahoji watu wote waliotajwa katika ripoti ya pili ya kuchunguza mchanga wa madini ya dhahabu (makinikia).

Takukuru imeanza uchunguzi huo kutokana na agizo la Rais Dk. Magufuli wakati akipokea ripoti hiyo ya Profesa Osoro Juni 13 mwaka huu.

Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli alivitaka vyombo vya dola kuanza uchunguzi mara moja kwa kuwahoji watu wote waliotajwa kuhusika kwa namna moja au nyingine katika kuandaa mikataba ya madini nchini.

Waliotajwa katika ripoti hiyo ni pamoja na waliowahi kuwa wanasheria wakuu wa Serikali, Andrew Chenge, Johnson Mwanyika, na manaibu wanasheria wakuu, Felix Mrema na Sazi Salula pamoja na wakuu wa idara ya mikataba; Maria Kejo na Julius Malaba.

Wengine ni waliokuwa mawaziri akiwamo Dk. Abdallah Kigoda (marehemu), Daniel Yona, Nazir Karamagi, William Ngeleja na Profesa Sospeter Muhongo.

Wengine waliotajwa ni waliokuwa makamishna wa madini; Kamishna Paulo Masanja, Dk. Dalaly Kafumu na Kaimu Kamishna, Ally Samaje.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Msemaji wa Takukuru, Mussa Misalaba alisema tayari wameanza kuwahoji watuhumiwa hao.

“Sisi hatuchelewi, tumekwishaanza kuwahoji, tangu Rais Magufuli alipotutaka kufanya hivyo.

“Nani ameanza kuhojiwa siwezi kusema kwa sasa, taasisi hii inaongozwa kwa maadili na sheria ambavyo vinatubana kutaja majina ya watu tunaowahoji kwani tunaweza kutibua mambo na kuvuruga uchunguzi wetu.

Kuhusu uwezo wa taasisi hiyo kufanyia uchunguzi kwa watu ambao wengine ni wazito na maarufu, alisema taasisi hiyo inao wataalamu walio na weledi wa kutosha hivyo hakuna kitakachowashinda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles