23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

SABABU  YA NETANYAHU KUZURU KENYA MARA YA PILI

JOSEPH HIZA, DAR ES SALAAM


KWA mara ya tatu ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na nusu Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amezuru barani Afrika, mara mbili akifanya nchini Kenya.

Mwelekeo huo mpya kwa Taifa hilo la Mashariki ya Kati umeibua maswali miongoni mwa wachambuzi wa mambo baadhi wakijiuliza maslahi anayotafuta  Afrika na hasa Kenya.

Awali sera za Israel zilikuwa zikilipuuza Bara hili, mikakati maalumu ikielekezwa badala yake Asia, Ulaya na Marekani ili kupata uungwaji mkono katika mgogoro wake wa kihistoria na Palestina pamoja na Waarabu eneo hilo.

Lakini pia wakati uhusiano ulipofufuka baina ya Afrika-Israeli uliishia zaidi katika sekta ya ulinzi na kijeshi; kununua au msaada wa silaha, kupata mafunzo ya kitaalamu na mbinu za kijeshi hasa kwa tawala zenye mwelekeo wa kikandamizi barani Afrika.

Wakati masuala ya ulinzi yakiendelea hadi leo hii, Netanyahu analenga kupanua uhusiano hadi katika maeneo mengine hasa biashara na diplomasia.

Kwa mfano kampuni ya  Israel, Energiya Global imejitosa kujenga miradi yenye thamani ya dola bilioni moja ya umeme wa jua Afrika, ikianzia na mradi wa dola milioni 20 kwenye uwanja mkuu wa ndege nchini Liberia.

Na mwaka 2015, Israel ilijenga mradi wa umeme wa jua nchini Rwanda ambao kwa sasa unazalisha asilimia tano ya umeme wote wa taifa hilo la Afrika Mashariki.

Hali kadhalika, ziara za Netanyahu barani Afrika ni kutafuta kuungwa mkono kwa taifa lake ndani ya Umoja wa Mataifa (UN) na vyombo vingine vya kimataifa katika nyakati hizi, ambazo washirika wake  zamani wa magharibi ukiondoa Marekani wanaanza kuitenga.

Miongoni mwao ni Uingereza na Ufaransa, ambazo siku hizi zinapinga wazi sera za Israel katika mgogoro wake Mashariki ya Kati kiasi cha kuunga mkono uanachama wa Palestina katika chombo kama UNESCO, kitu ambacho hakikuwepo huko nyuma.

Viongozi wa Afrika kwa miaka mingi tangu wakati wa Vita ile ya Siku Sita wamekuwa wakiipinga Israel ndani ya UN kuhusu Palestina, ikichangiwa na wingi wa Waslamu katika bara hili pamoja na kuguswa na kinachowakumba Wapalestina, ikikumbushia madhila waliyokuwa wakipata Waafrika zama zile za ukoloni.

Mwaka  2016,  Senegal, ikiwa mmoja wa wanachama wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la UN ilikuwa mfadhili mwenza wa azimio la UN lililotamka kuwa sera ya Israel ya ujenzi wa makazi ya walowezi katika eneo la Yerusalem Mashariki na Ukingo wa Magharibi ni haramu na inakiuka sheria za kimataifa.

Netanyahu aliwaghadhibikia wote waliofadhili azimio hilo ikiwamo Senegal, na mara moja akavunjilia mbali husiano zote za kidiplomasia na kiuchumi na taifa hilo la Afrika Magharibi.

Senegal, ambayo aslimia  92 ya watu wake ni Waislamu, kupitia wizara ya mambo ya nje ikajibu kidiplomasia zaidi: “Senegal inaunga mkono utafutaji suluhu wa haki na usawa katika mgogoro wa Palestina-Israeli.”

Netanyahu akaviambia vyombo vya habari kabla ya ziara ya kwanza Afrika mwaka jana, kuwa madhumuni ya ziara hiyo yalikuwa: “kuvunja wingi huu (mataifa yanayoipinga), wa chombo (Umoja wa Afrika) hiki kikubwa cha mataifa 54 ambacho ndicho msingi wa wingi unaoikwamisha Israel katika UN na vyombo vingine vya kimataifa.”

Netanyahu anaamini kuwa kuilainisha Umoja wa Afrika (AU) kupitia mikataba ya kibiashara, anaweza kupunguza kama si kuondoa kabisa upinzani inaopata Israel ndani ya UN kutokea Afrika.

Anaweza akawa sahihi kwani Senegal na Israel ziliweza kurejesha uhusiano wa kidiplomasia baada ya kujadiliana katika mkutano wa Jumuiya ya Uchumi Afrika Magharibi (ECOWAS) nchini Liberia.

Katika ziara ya karibuni nchini Kenya, dhumuni la ziara hiyo ya siku moja, Netanyahu alisema kabla ya kupanda ndege ni, “kupanua uhusiano wa Israel na Afrika, ikiwamo kuanzisha muunganiko na mataifa ambayo haina bado uhusiano wa kidiplomasia.”

Ikumbukwe pia ni Kenya ndiyo iliyofungua milango ya ziara za Netanyahu barani Afrika baada ya Rais Uhuru Kenyatta wakati akitafuta washirika wapya kufuatiwa kuwekewa kauzibe na Mataifa ya Magharibi alipoitembelea Israel Februari 2016, kitu kilichomfanya Netanyahu aseme ‘hakika Afrika-Israel inawezekana.’

Netanyahu alisisitiza kabla ya ziara ya karibuni kuwa kipaumbele chake kipya cha kwanza ni kuzindua uhusiano na Afrika. “balozi nne za Israel zimeshafunguliwa kipindi cha miaka miwili na nina matumaini mwingine wa tano utafunguliwa siku si nyingi. Na huu ni mwanzo tu,”alijigamba

Aidha akizungumza katika mkutano wa chama chake cha Likud siku moja kabla ya ziara hii, Netanyahu alisikika akijigamba kufanikiwa kutengeneza uhusiano na Mataifa ya Afrika baada ya miaka mingi ya kususwa, akiwakumbushia wajumbe pamoja na wabunge kuwa hii inakuwa ziara yake ya tatu barani humu kipindi cha mwaka mmoja na nusu.

Kabla ya ziara yake ya pili iliyomfikisha kwenye mkutano na ECOWAS nchini Liberia, mapema Julai 2016, Netanyahu alikuwa Waziri Mkuu wa Kwanza wa Israeli katika kipindi cha miongo kadhaa kutembelea Bara la Afrika, wakati alipozuru mataifa manne ya Afrika Mashariki Uganda, Kenya, Rwanda na Ethiopia.

Kwanini yawe mataifa hayo? Uganda, ni Taifa alilolitembelea miaka 10 nyuma, kwa mwaliko wa Rais Yoweri Museveni, akiwa bado hajawa Waziri Mkuu na hivyo kuwa na uhusiano mzuri naye.

Alialikwa kipindi hicho wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya uvamizi wa Entebbe, unaokumbushia namna makomando wa Israel walipowaokoa mateka zaidi ya 100 wa Taifa hilo, katika tukio ambalo kaka yake Netanyahu kama tutakavyoona baadaye katika makala haya aliuawa. Aidha Uganda ni Taifa lililo tayari kupokea wahamiaji wanaoomba hifadhi nchini Israel kwa makubaliano ya malipo.

Rwanda kwa upande wake mbali ya sababu ya kushamiri kwa uhusiano wa kibiashara, Netanyahu alienda kuweka sawa suala kama la Uganda la kupokea wahamiaji 10,000 waliokwama kupata hifadhi Israel kwa makubaliano ya malipo.

Upande wa Ethiopia ina uhusiano wa kihistoria na kidini na Israel, mbali ya Kitabu kitakatifu cha Biblia, kile cha Ethiopia, Kebra Nagast kina simulizi za namna Malkia Sheba wa Ethiopia alivyomtembelea Mfalme Solomon wa Israeli kwa madhumuni ya kibiashara.

Leo hii Waethiopia 140,000 wanaishi Israel na kutokana na historia hiyo, mataifa haya yana uhusiano mwema huku Ethiopia ikiitegemea Israel kwa misaada ya kijeshi kupambana na majirani zake wa Kiarabu.

Na hili la kwanini Kenya tutaliona baadaye katika makala haya, lakini kwa ujumla mataifa hayo yalikuwa kianzio cha mkakati wake wa kujenga ushawishi wa Israel inayofahamika kwa ubora wa teknolojia katika sekta mbalimbali, ziara ambayo kama tulivyoona ilitanguliwa na ile ya Kenyatta nchini Israel.

Katika miaka ya 1960, uhusiano baina ya Afrika-Israeli ulikuwa mzuri na Israel ilikuwa na balozi 32 katika mataifa mbalimbali ya Afrika.

Hata hivyo, haraka haraka mambo yakageuka kuwa chungu kufuatia Vita ya Siku Sita mwaka 1967 na ile ya Yom Kippur mwaka 1973 baina ya Israel na ushirika wa Mataifa ya Kiarabu.

Katika kipindi hicho, uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ukichagizwa zaidi na Misri iliyohusika katika vita hizo, uliziagiza nchi wanachama kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Israel.

Mataifa yote kasoro Malawi, Lesotho na Swaziland yalitii agizo hilo, ingawa baadhi shingo upande.

Msimamo huo dhidi ya Israel ulibakia hivyo hadi katika miaka ya 1990 wakati mataifa mengi yalipoanza kurejesha uhusiano.

Nguvu msukumo iliyo nyuma ya mataifa ya Afrika kulegeza misimamo yao kwa Israel kwa kiasi kikubwa imelenga maslahi ya kibiashara na kijeshi.

Bado kuna mataifa makubwa Afrika yenye nguvu na ushawishi yanayoweza kukwamisha nia ya Netanyahu na miongoni mwao ni  Nigeria ambayo haikushiriki mkutano wa ECOWAS nchini Libya na hadi sasa haijatoa taarifa rasmi juu ya uamuzi wake huo.

Afya ya Rais wake Muhammad Buhari inaweza ikawa sababu lakini iwapo ndiyo sera ya Nigeria, Netanyahu ana kazi ya kufanya kutopuuza ukubwa wa ushawishi wa Taifa hilo ndani ya ECOWAS, maana huwezi kukitaja chombo hicho bila Nigeria.

Lakini pia wakati Mataifa ya Afrika yakivunja uhusiano wa kidiplomasia na Israel miaka ile, kama tulivyoona baadhi yalifanya shingo upande.

Wakati Tanzania, chini ya Mwalimu Julius Nyerere ikiwa miongoni mwa mataifa yaliyokuwa na msimamo mkali dhidi ya Israel, hali hiyo haikuwa hivyo kwa jirani yake Kenya.

Hilo halikuwa ajabu kwa vile Kenya ilikuwa mshirika mkubwa wa Magharibi, mataifa ya kibepari yaliyokuwa yakiipa kiburi Israel, hivyo ilihesabu kuwa inapoteza mshirika mzuri kwake kimaslahi.

Licha ya kwamba inapozungumza majukwaani, Kenya iliionesha ukali kwa Israel, lakini baba wa Rais wa sasa Uhuru Kenyatta, Mwasisi wa Kenya huru, Mzee Jomo Kenyatta alikuwa na urafiki mzuri na binafsi na Golda Meir, Waziri Mkuu wa nne wa Israeli.

Lakini pia wakati ikiwa imetangaza kuvunja uhusiano na Israel, Kenya ikaanzisha uhusiano wa siri na Palestina, ikitarajia kunufaika kutoka kwa Waarabu.

Mita chache tu kutoka makazi rasmi ya Mwambata wa Ubalozi wa Uingereza huko Spring Valley, Nairobi, Chama cha Ukombozi Palestina (PLO) chini ya Marehemu Yasser Arafat, mwaka 1974 kiliruhusiwa kufungua ofisi ya siri eneo hilo.

“Ni watu wachache waliojua kuhusu nyumba hii,” anakumbushia aliyekuwa Naibu Kamishina wa Polisi nyakati za utawala wa Jomo Kenyatta na Daniel arap Moi. “Ililindwa na polisi waliovalia kiraia.”

Ndani ya ofisi, maofisa wa PLO waliendesha ofisi zao bila kujulikana na wala bughudha zozote.

Walikaribishwa Kenya baada ya Taifa hilo kulazimika kusitisha uhusiano wake na Israel kufuatia vita ya Yom Kippur iliyopiganwa na mataifa ya Kiarabu yaliyoongozwa na Misri na Syria – katika Jangwa la Sinai na vilima vya Golan kupinga uvamizi wa Israel, tangu ile vita maarufu ya Siku Sita ya 1967.

Vita ilisababisha mgogoro wa mafuta baada ya Jumuiya ya Mataifa ya Kiarabu Yazalishayo Mafuta (OAPEC) kutangaza vikwazo vya nishati hiyo, vilivyoshuhudia bei ikipaa kutoka dola tatu kwa pipa hadi 12 kwa pipa na kusababisha uchumi wa Kenya kuvurugika vibaya.

Kenya ilikuwa na matumaini kuwa kwa kufungua ofisi ya PLO na kuvunja uhusiano na Israel, ingepata upendeleo maalumu wa kiuchumi kutoka dunia ya Kiarabu, lakini hilo halikutokea.

Ofisi ya Nairobi ilikuwa ikishirikiana na ile ya Tanzania. Mara kwa mara ilitoa machapisho kwa kushirikiana na kundi lingine la Solidarity with Palestinian lililoweka kambi nchini Tanzania, ambayo kipindi hicho ilifahamika duniani kwa kutoa hifadhi kwa makundi mengi ya harakati za ukombozi.

Lakini pia pamoja na ubalozi wa Israeli pale Lower Hill, Nairobi kufungwa, Kenya haikutaka kupoteza uhusiano huo hivi hivi ikifahamu umuhimu wa Israel kwake siku za usoni.

Kundi teule la mawaziri wa Kenyatta lilipewa jukumu la kuendelea kuwasiliana na Tel Aviv na kuwafahamisha namna wasivyofurahishwa na azimio la OAU dhidi ya Israel.

Wakati uhusiano wa siri ukiendelea, Oktoba 1975, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Munyua Waiyaki aliandika barua ya siri kwenda kwa mwenzake wa Israeli, Yigal Allon.

Alimtaka mwenzake huyo, Israel itumie ushawishi wake kuiomba Marekani kuipatia Kenya ndege za kivita ili kumzuia Rais wa Uganda, Idi Amin aliyetishia kulimega eneo la Magharibi mwa Naivasha — ambalo awali lilikuwa sehemu ya Uganda.

Kenyatta alikuwa na hofu kutomhimili  Amin kutokana na usasa wa zana zake za kivita kulinganisha na Kenya, ambayo ndege zake za kivita zilichakaa.

Waiyaki aliligeukia Taifa hilo la Kiyahudi, ambalo pia lilitoa mafunzo kwa makachero wake waandamizi, makomando na kikosi cha ulinzi cha Rais baada ya kushindwa kwa Mataifa ya Kiarabu kusimama upande wa Kenya katika uhasama wake na Amin na Somalia ya Siad Bare.

Ombi la Kenya lilikubaliwa miezi mitano baadaye baada ya Ubalozi wa Israel kuiandikia Washington ikigusia  kuhatarika kwa ‘maslahi ya Marekani’ eneo hilo linalozidi kujengeka ushawishi wa Urusi na China.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Henry Kissinger alimtaka Rais Gerald Ford kuikubalia Kenya kukabili tisho la silaha za Urusi nchini Uganda na Somalia.

Lakini pia ulikuwa uvamizi wa Entebbe uliorahisisha mambo kwa kuifanya Marekani  ione Kenya kuwa mshirika muhimu sana kwake katika kuukabili Ukomunisti eneo hilo na kwa Israel mshirika wake pia.

Katika hilo Mzee Jomo Kenyatta aliweza kuionesha Marekani, ambayo awali ilisitisha misaada kwa Kenya kuwa tisho la Amin lilivyokuwa kweli.

Kufikia wakati Kissinger aliporudi nyumbani baada ya ziara yake nchini Kenya Aprili 1976, Kenyatta aliiruhusu ardhi ya Kenya kutumika kujaza mafuta kwa makomando wa Israeli, ambao walikuwa katika operesheni ya kwenda kuwaokoa abiria waliotekwa wakiwa ndani ya ndege ya Shirika la Ndege la Ufaransa, ambapo Idi Amin alikuwa upande wa watekaji.

Kissinger, ambaye aliripoti Marekani kuwa Mzee Jomo afya yake haikuwa nzuri akitumia dozi, aliitaka Kenya iihusishe OAU ili Taifa hilo lisionekane linaingilia masuala ya eneo hilo.

Lakini Mzee Kenyatta alikataa kata kuihusisha OAU kwa vyovyote vile, akikumbuka namna chombo hicho kilivyo tofauti na mshirika wake wa siri Israel.

Hatimaye Wamarekani walikuja mpenda sana Kenyatta kwa ushiriki wa Kenya kuisaidia Israel kwenda Uganda kuwaokoa mateka.

Ikumbukwe hizo zilikuwa siku za giza nchini Uganda, wakati Dikteta Idi Amin Dada, alipokuwa upande wa magaidi walioiteka Air France kwenda Uwanja wa Ndege wa Entebbe, ambako walikuona ni salama kwao kutokana na uwepo wa Amin.

Ikiwa njiani kutoka Tel Aviv kwenda Paris ndege hiyo chapa AF139, ilitekwa mjini Athens, Ugiriki Juni 27, 1976 na kuelekezwa Uganda ikiwa na abiria 248 na wafanyakazi 12.

Watekaji ambao ni Wapalestina na Wajerumani wawili kutoka kundi la Bader Meinhof Red Army walikuwa wakishinikiza kuachiwa kwa wapiganaji wa Palestina wanaoshikiliwa Israel na katika mataifa mengine.

Watekaji waliokaribishwa na Idi Amin kisha wakatengenisha utaifa, huku 148 wa mataifa mengine wakiachiwa huku wale wa Kiyahudi karibu 100 na wafanyakazi Wafaransa wakiendelea kuzuiliwa.

Watekaji walitishia kuwaua mmoja baada ya mwingine iwapo matakwa yao hayatatimizwa, hali ambayo iliifanya Israel kuitisha kikao cha dharura cha baraza la mawaziri na wanausalama ambapo makomando wakateuliwa kuifanya kazi kuwaokoa Wayahudi wenzao.

Kenya ilishiriki kikamilifu kutoa msaada wa kilojistiki, ikitoa anga na ardhi, hali iliyosababisha kuuawa kwa Waziri wa zamani wa Kenya, Bruce McKenzie, ambaye ndege yake ililipuliwa Mei 24, 1978.

Operesheni ya kuwaokoa mateka Julai 4, 1976 ilifanikiwa lakini iliigharimu familia ya Netanyahu maana mtu pekee miongoni mwa makomandoo wa Israel aliyeuawa alikuwa Luteni Kanali Yonatan Netanyahu, kaka wa Benjamin Netanyahu.

Amin akiwa amekasirika akalipa kisasi kwa kumuua mateka wa Israel Dora Bloch, aliyekuwa akitibiwa Hospitali ya Mulago na kuzidisha vitisho vya kuivamia Kenya, ambayo ilikana vikali kuisaidia Israel.

Barua kutoka Kissinger ya Julai 3, 1976 ilisema: “Nimesikia na kuridhika operesheni ya uokoaji wa ndege ya Air France iliyotekwa mapema wiki hii. Nataka Rais (Ford) ufahamu kuwa Kenya ikihitaji msaada siku chache zijazo, Marekani lazima itoe ushirikiano wa kutosha.”

Siku nne baadaye barua ya  Kissinger ikamfahamisha Mzee Kenyatta kupatiwa ndege za kivita chapa P-3 zikiwa katika manowari USS Beary mjini  Mombasa Julai 12 na manowari hiyo itakaa hapo kwa siku tatu ili kumtisha Amin.

Ili kumtisha Amin, Kissinger alikubali kutuma manowari na ndege maalumu za kuichunguza Uganda na kuweka kambi Mombasa.

Kumuonesha Amin kuwa Kenya ilikuwa imekamilika kwa zana nzito za kivita, Marekani pia ikakubali kutoa zana nyingine zaidi maalumu kuzionesha wakati wa Sikukuu ya Jamhuri 1976. Kama ilivyotarajiwa, mkakati wa Mzee Kenyatta ulifanikiwa kwani Amin alitishika kweli kweli, akafuta mipango ya kuivamia Kenya.

Hivyo ndivyo, Israel ilivyoweza kumfanya Mzee Kenyatta apumue dhidi ya vitisho vya Amin, ambaye badala yake akaenda kuivamia Tanzania zile pande za Kagera miaka miwili baadaye.

Wakati Kenya ilipovamiwa na wanamgambo wenye silaha Septemba 21, 2013 kwenye Kituo cha Biashara cha Westgate mjini Nairobi, Kenya, ni Israel iliyojitokeza kwa hali na mali kuisaidia kijeshi.

Nyendo hizo za tangu zamani zinaonesha kwanini Kenya ina urafiki maalumu na Israel huku pia eneo hilo likiwa la kimkakati kutokana na uwepo wa mashirika mengi ya kimataifa.

Lakini pia Netanyahu kwa kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Kenyatta mjini Nairobi, aliweza kuua ndege wawili kwa jiwe moja, akikutana na kuzungumza na viongozi wakuu  wa mataifa zaidi ya 10 wa Afrika katika harakati za kuboresha uhusiano na Bara hili.

Mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles