24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Sababu tisa zang’oa mawaziri 15

Na NORA DAMIAN

-DAR ES SALAAM

NDANI ya miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli, mawaziri na naibu mawaziri 15 wameondolewa katika nafasi zao kwa sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo. 

Idadi hiyo ilifikiwa jana baada ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda.

Uteuzi huo ulitenguliwa kufuatia malalamiko yaliyoelekezwa katika wizara yake na wafanyabiashara waliokutana na Rais Ikulu, Dar es Salaam juzi.

Viwanda na Biashara ni miongoni mwa wizara tano ambazo mawaziri wake wamekuwa wakitumbuliwa ama kubadilishwa. 

Wizara nyingine ni Maji na Umwagiliaji, Kilimo, Madini na Mambo ya Ndani ya Nchi.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, imeeleza kuwa Rais Magufuli amemteua aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa kuchukua nafasi ya Kakunda.

Katika mkutano wa juzi uliokutanisha wafanyabiashara kutoka wilaya zote nchini, baadhi yao waliinyoshea kidole Wizara ya Viwanda huku wengine wakidai kuwa hawamfahamu hata waziri wake.

Pia wafanyabiashara walilalamikia tabia ya baadhi ya watendaji wa wizara hiyo kufunga viwanda kutokana na madai mbalimbali yakiwemo ya kodi na ushuru. 

Mara kwa mara Rais Magufuli amekuwa akionesha kukerwa na utendaji wa baadhi ya wizara na kusema kuwa ataendelea kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri pale patakapokuwa na uhitaji wa kufanya hivyo.

Licha ya kwamba mara nyingi taarifa za Ikulu hazitaji sababu ya mawaziri kutumbuliwa, uchambuzi wa Mtanzania Jumapili umeonesha kuwa baadhi waliondolewa kutokana na kamati za Bunge kuwataja kuhusika na makosa mbalimbali walipokuwa katika nafasi zao miaka ya nyuma.

MAWAZIRI WALIOTOSWA

Mei 20, 2016, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga aliondolewa katika nafasi yake kwa tuhuma za kuingia bungeni akiwa amelewa.

Mei 23, 2017, Nape Nnauye (Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo) alitumbuliwa siku moja baada ya kupokea ripoti kutoka kwa kamati aliyokuwa ameiunda kuchunguza sakata la kuvamiwa kwa Ofisi za Clouds Media Group.

Mei 24, 2017, Rais Magufuli pia alitengua uteuzi wa Profesa Sospeter Muhongo aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini kufuatia sakata la mchanga wa madini (makinikia) wa Kampuni ya Acacia.

Januari 19 mwaka jana, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Walemavu aliyekuwa akishughulikia walemavu, Dk. Abdallah Possi na kumteua kuwa balozi.

Septemba 7 mwaka jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene, aliandika barua ya kujiuzulu wadhifa huo baada ya kutajwa katika ripoti ya uchunguzi wa biashara ya madini ya Tanzanite na almasi iliyoonesha namna Serikali ilivyopoteza matrilioni ya fedha kutokana na sababu mbalimbali.

Hatua hiyo ilikuja muda mfupi baada ya Rais Magufuli kuwataka viongozi wote ambao wametajwa katika ripoti hiyo wakae pembeni kupisha uchunguzi ambao utakuwa huru na wa haki.

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani naye alijiuzulu baada ya kutuhumiwa kutotekeleza majukumu yake kikamilifu alipokuwa akifanya kazi Shirika la Madini la Taifa (Stamico) lenye dhamana ya kusimamia madini.

Pia Oktoba 7 mwaka jana, wakati alipofanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri kwa kuongeza idadi ya wizara, alitengua uteuzi wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe huku nafasi yake ikichukuliwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla.

Katika mabadiliko hayo, Mhandisi Ramol Makani naye aliachwa na nafasi yake ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii ilichukuliwa na Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga.

Mwingine ni Anastazia Wambura aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Juliana Shonza.

Julai mwaka jana, Rais Magufuli alifanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri na kumtupa nje aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba huku nafasi yake ikichukuliwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Kangi Lugola.

Rais Magufuli alisema Mwigulu alishindwa kushughulikia azimio la Bunge kuhusu suala la kufunga mashine za kielektroniki za utambuzi wa alama za vidole (AFIS) katika vituo 108 vya polisi, mradi uliofanywa na Kampuni ya Lugumi kwa gharama ya Sh bilioni 37. 

Septemba mwaka jana, Rais Magufuli pia alitengua uteuzi wa Dk. Susan Kolimba aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kumteua Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Damas Ndumbaro kuchukua nafasi hiyo.

Wengine ni Charles Mwijage (Wizara ya Viwanda) na Dk.  Charles Tizeba (Wizara ya Kilimo) ambao waliondolewa Novemba mwaka jana kwa kushindwa kushughulikia suala la bei ya korosho, kahawa, pareto na ufufuaji wa Kiwanda cha Chai Mponde kilichopo mkoani Tanga na kile cha Buko mkoani Lindi.

Rais Magufuli alieleza hadharani kuwa hakuona taarifa yoyote ya Waziri wa Viwanda au Kilimo kukemea sekta binafsi.

Alisema kiwanda cha chai kilikaa bila kufanya kazi kwa miaka minane hadi alipomtuma Waziri Mkuu kwenda kutatua tatizo na kwamba Kiwanda cha Mponde na cha Lindi havikurudishwa na wizara na hata mchakato wake mawaziri husika hawakuujua.

Mwingine aliyeondolewa ni Gerson Lwenge aliyekuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji.  

KUBADILI MAWAZIRI

Novemba mwaka jana, Rais Magufuli alisema ataendelea kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri pale patakapokuwa na uhitaji wa kufanya hivyo.

Alisema kuwa amekuwa akilazimika kumtuma waziri mkuu na wakati mwingine kumpigia simu hata saa 8 usiku akimtaka awakumbushe mawaziri wake kazi za uwaziri ni utumwa, hivyo lazima wawe watumwa wa watu masikini.

“Kazi hii ni ngumu na ni utumwa, mimi sitashangaa, hata nikibaki na mmoja wala sitajali. Kubadilisha ni ‘very simple’, wabunge wako 300 nafanya ‘rotation’ tu ili kusudi nipate matokeo,” alisema Rais Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles