31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Saa za waliochota Sh bil 321 IPTL zahesabika

Abdulrahman Kinana
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kila aliyehusika katika kashfa ya uchotwaji wa Sh bilioni 321 katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), abebe msalaba wake bila kujali cheo chake na kwamba muda wa kulindana umekwisha.

Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye walipokuwa wakihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Ilulu mkoani Lindi.

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais asiyekuwa na wizara maalumu, Profesa Mark Mwandosya, alisema ni vema watu wanaotajwa katika kashfa hiyo wakae pembeni ili kutoitia doa serikali na chama tawala.

Profesa Mwandosya alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambao pia ni wanachama wa CCM.

“Kwa sasa hivi vikao vya chama na serikali vinaendelea, ni lazima ripoti iwasilishwe bungeni, mambo yawe hadharani ili mbivu na mbichi zijulikane.

“Kwa maoni yangu, naamini kabisa kuwa ni vema wale wote wanaotajwa kwenye hili suala la IPTL, wakakaa kando ili kuepuka kukipaka chama na serikali matope,” alisema Profesa Mwandosya.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amemtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, na Katibu Mkuu wake, Eliachim Maswi pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema wajiuzulu kutokana na kutajwa katika kashfa hiyo.

Katika mkutano huo, Nape  alisema  watakaobanika kuhusika katika kashfa hiyo, wanapaswa kuwajibishwa bila kujali nafasi  zao.

“Katika hili naomba niseme kila  ambaye atabainika kuhusika  achukuliwe hatua, kila mtu  abebe msalaba wake mwenyewe. Hatutakubali  kuona watu waliohusika katika sakata hilo wanaachwa, lazima  wachukuliwe hatua.

“CCM tunaheshimu miiko ya  uongozi na maadili, hivyo hili  la Escrow lazima waliohusika  wachukuliwe hatua,”alisisitiza  Nape.

Kwa upande wake Kinana alisema muda wa viongozi  ndani ya chama hicho kulindana  umekwisha na uvumilivu sasa  basi.

Kinana ambaye hakuzungumzia  kabisa sakata la Escrow, alitumia nafasi hiyo kuwaambia  wananchi. “Si sawa mwizi  kumlinda mwizi, haiwezekani mtu  anaharibu halafu anaachwa.

“Muda wa kulindana haupo tena  ndani ya CCM. Uvumilivu umefika  mwisho. Muda wa kubebana na  kuvumuliana sasa  umekwisha,”alisisitiza Kinana.

Alisema  CCM  haiko tayari  kuendelea kulindana na kubebana  wakati mambo yanaharibika  huku  akisisitiza kazi ya chama hicho  ni kuisimamia Serikali.

CUF

Nacho Chama cha Wananchi (CUF), kimemtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Nishati na madini, Profesa Sospeter Muhongo na wengine wanaotajwa katika kashfa hiyo kujiuzulu wenyewe vinginevyo rais atengue uteuzi wao.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba alisema  viongozi wengine wanaopaswa kuwajibika ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali(AG),Jaji Frederick Werema na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi.

Alisema licha ya hatua hiyo, pia akaunti zote za benki zinazotajwa kupitisha fedha za Escrow ni vyema zikafungwa na fedha zirudishwe serikalini.

Profesa Lipumba pia alitaka mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering, James Lugemalila iliyokuwa na asilimia 30 za hisa IPT na mmiliki wa Kampuni ya Pan Africa Power Solutions Ltd (PAP), Harbinder Singh Sethi, aliyenunua kampuni hiyo ya kufua umeme, wafikishwe mahakamani.

Alisema chama hicho kimefikia uamuzi huo baada ya kuona ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG).

“Tanesco walipaswa kurejeshewa sh bilioni 321 zilizolipwa kwa ITPL kati ya mwaka 2002 na 2012, kwa hiyo fedha zote za akaunti ya escrow jumla ya Sh bilioni 306 ni mali ya tanesco na bado wanaidai IPTL bilioni 15.

“Kutokana na hali hiyo, watuhumiwa hao wanapaswa kufikishwa mahakamani kutokana na kufanya ufisadi mkubwa wa namna hiyo wakati wananchi wanaishi katika mazingira magumu,”alisema Profesa Lipumba.

Alisema katika ripoti hiyo pia imeonyesha kuwa kampuni ya PAP haikununua kihalali asilimia 70 ya hisa za kampuni ya Merchmar ya nchini Malaysia  katika IPTL kwa sababu zilikua zimezuiwa na mahakama.

“PAP hawana hati halisi za hisa hizo, pia ilifanya udanganyifu katika malipo ya kodi kwa kutoa nyaraka za uongo kuwa walinunua hisa kwa sh milioni 6 badala ya dola milioni 20, hali iliyoikosesha serikali mapato ya Sh bilioni 8.7.

“Kosa hilo pia linawahusu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kanda ya Ilala ambao walihusika katika kupokea kodi ya mauzo hayo,”alisema.

Prof. Muhongo

Katika hatua nyingine, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema hajiuzulu ng’o.

Akizungumza na MTANZANIA  jijini Dar es Salaam juzi, Profesa Muhongo alisema uamuzi wa kujiuzulu unaweza kusababisha rasilimali za wananchi kuibwa zaidi.

“Siwezi kujiuzulu kwa ajili ya kauli za watu…nafanya kazi kwa maslahi ya wananchi, kama kuna watu wanadhani nitajiuzulu ili nitengeneze mianya ya kula rushwa, wamejidanganya… sijiuzulu ng’o,”alisema.

Alisema hafanyi kazi kwa ajili ya kusikiliza maneno ya watu, bali kutetea rasilimali za wananchi, hivyo hawezi kuhusishwa na mambo yasiyomuhusu.

“Hata ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonyesha wazi sijala hata shilingi kumi, na siwezi kufanya hivyo kwa sababu nawatumikia wananchi kwa nia na moyo mmoja. Wanaotaka ning’oke wana mambo yao binafsi, narudia tena kusema sing’oki.

“Sijatenda kosa baya lolote, wezi, walarushwa na wababaishaji wananiogopa na kunihofia,” alisema.

Alisema mara nyingi vyombo vya habari vimekuwa vikimtuhumu bila ya kuwa na ushahidi.

“Sitaki kutetewa, bali wanapaswa kuandika habari zenye ukweli ambazo zimefanyiwa utafiti kabla ya kutoa hukumu,” alisema.

Pinda ausia serikali

Naye Waziri Mkuu Mizengo Pinda, amesema ili kuweza kuridhisha nyoyo za Watanzania katika kashfa ya IPTL, ni lazima Serikali ijipange ili kuweza kutoa majibu yatakayoridhisha  kuhusiana na suala la IPTL.

Amesema kwa kipindi cha sasa Taifa linapita katika wakati mbaya na mgumu wa lala salama kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Kauli hiyo aliitoa jana mjini Dodoma alipokuwa akitoa hotuba ya kumweka wakfu Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Kati wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Dickson Chilongani, ambapo alisema hivi sasa kumekuwa na kampeni za kuchafuana mbele ya jamii.

“Baba Askofu kipindi hiki ni kibaya tunasema lala salama, kubwa ni Serikali kutoa maelezo yatakayotuaminisha kwa wananchi. Ila uadilifu mkubwa unahitajika serikalini kwa sababu kuna mapesa.

“…Kipindi hiki ni cha lala salama kwa hiyo watu wengine wamekuwa wakichafua wengine kwa ajili ya kutaka kupata madaraka ya nchi,” alisema Pinda.

Habari hii imeandaliwa na  Patricia Kimelemeta, Shabani Matutu na Ramadhan Hassan, Dodoma

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Mawaziri wa CCM si wakweli kwa sababu tangu Kafulila alipotoa taarifa ya wizi wa fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow walimpinga kwa dhati kabisa, lakini baada ya kuona ukweli umeenea kwa wananchi wanaanza unafiki wa kusema tusilindane. Tunawajua CCM sera zao ni za kulindana kwa makosa ya kuwadhurumu wananchi, hata waliosema CCM ni Chukua Chako Mapema wako sahihi maana tunaona matendo yao

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles