RWASA AJITOA MUUNGANO WA UPINZANI BURUNDI

0
657

Bujumbura, BURUNDI


Mwanasiasa mkongwe nchini Burundi, Agathon Rwasa, amejiengua katika muungano wa vyama vya upinzani nchini humo na anatarajia kusajili chama chake kipya cha siasa.

Baada ya kujiengua ameshakutana na watu wanachama wake zaidi ya 500 kutoka mikoa tofauti kwa majadiliano na mapendekezo mbalimbali kwa mujibu wa sheria ili waweze kusajili chama chao wizara ya mambo ya ndani wanachotaka kukiita National Liberty Front Amizero y’Abarundi.

Kwa sasa Rwasa ni Makamu Spika wa Bunge akiwakilisha muungano wa vyama vya upinzani wa Amizero y’abarundi.

Muungano huo katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2015 ulishika nafasi ya pili ukitanguliwa na chama tawala (CNDD FDD) cha Rais Pierre Nkurunziza.

Rwasa, amesema itawalazimu wanasiasa wa upinzani kujidhatiti katika vyama vyao ili wafikie malengo kwenye uchaguzi ujao.

Vile vile amewataka wafuasi wake wawe watulivu, wavumilivu na wachangie hali na mali kwa kipindi hiki hadi itapofikia uchaguzi mkuu miaka miwili ijayo.

Rwasa, amewahi kuishi uhamishoni katika nchi jirani ya Tanzania kwa takribani miaka 20 alipotoroka uongozi wa watutsi wachache. Mazungumzo ya Amani ya Arusha yaliwawezesha wana siasa wa kabila kubwa la wahutu kurejea nyumbani.

Agathon Rwasa, alitoroka tena machi mwaka 2010 wakati (CNDD FDD) ikiongoza. Baadae alirejea Burundi 2013.

Alijiunga na bunge baada ya uchaguzi wa 2015 ulio susiwa na upinzani. Iwapo chama chake kitasajiliwa, anasadikiwa kuwa mpinzani mkubwa kuliko wengine dhidi ya chama tawala cha (CNDD FDD).

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here