24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

RUTO: NASA WANATUMA WATU KUTUOMBA ‘NUSU MKATE’

NAIROBI, KENYA

NAIBU Rais, William Ruto, ameusuta muungano wa upinzani wa National Super Alliance (NASA), akisema lengo lake la kutaka kususia marudio ya uchaguzi ujao wa urais ni kutaka kujumuishwa kwenye serikali ya mseto.

Hata hivyo, Ruto amesema endapo Jubilee itashinda uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Alhamisi Oktoba 26, 2017, hawatakubali Serikali ya ‘nusu mkate’.

“Hawa watu ukiwasikiliza, mchana wanasema hawataki serikali ya nusu mkate usiku wanatutafuta wakiiomba,” alisema Ruto akihutubia kwenye Kaunti ya Uasin-Gishu.

Nasa imekuwa ikisema iwapo matakwa yake hayataafikiwa kikamilifu, itabidi wasusie kushiriki uchaguzi.

NASA inasisitiza sharti la Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) irekebishwe ikiwatuhumu baadhi ya maafisa wake kusababisha uchaguzi wa Agosti 8 kutokuwa halali.

Afisa Mkuu Mtendaji Ezra Chiloba ni mmoja wa maafisa wanaotaka atimuliwe ofisini, na kwa sasa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Keriako Tobiko imeagiza sekretarieti ya IEBC kuchunguzwa.

Ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta ulifutwa Septemba Mosi na Mahakama ya Juu, baada ya Nasa kufungua kesi kupinga matokeo hayo kwa kile ilichosema uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu.

Jaji Mkuu David Maraga aliagiza IEBC inayoongozwa na Mwenyekiti Wafula Chebukati kuandaa uchaguzi mwingine kwa siku 60.

Chama cha Jubilee kimekuwa kikimshambulia Jaji Maraga kikidai alishirikiana na Nasa kubatilisha ushindi wa Rais Kenyatta.

Naibu Rais hata hivyo amesema Jubilee haitakubali kusubiri yeyote anayetafakari kushiriki au kutoshiriki uchaguzi huo.

“Hakuna muda wa kupoteza kukusubiri. Ukisema hutaki uchaguzi na iwe hivyo sisi tutaendelea na mipango,” alisema akiilenga Nasa.

Kwenye kampeni hiyo ya Jubilee Uasin-Gishu, Gavana wa kaunti hiyo Jackson Mandago alikuwepo.

“Wakati wa mchezo umeisha. Hatutakubali wananchi wagharamike tena pesa za kuandaa uchaguzi mwingine, kwa sababu ya watu wenye tamaa binafsi,” alisema Mandago akionekana kuisuta Nasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles