23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

RUFAA ZA MATIBABU NJE ‘STOP’

Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amewataka madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),  kutokutoa rufaa kwa mgonjwa yeyote ambaye anaweza kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.

Kauli hiyo ameitoa jijini Dar es Salaam jana wakati akizindua vyumba viwili vya upasuaji wa watoto wadogo, ambapo alisema hata kama kuna mwanasiasa anataka rufaa hali ya kuwa ugonjwa wake unaweza kutibiwa na madaktari hapa nchini wasifanye hivyo.

“Narudia tena, hata kama ni mimi au kiongozi yeyote asipewe rufaa kama ugonjwa wake unaweza kutibiwa hapa, mimi naweza kuja hapa nikawashinikiza mnipeleke nje, msikubali, simamieni taaluma yenu.

“Kama madaktari wamethibitisha mgonjwa anaweza kutibiwa hapa, hakuna haja ya kupelekwa nje,” alisema Ummy.

Licha ya agizo hilo, alisema Serikali itaendelea kuiwezesha Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) katika mikakati yake ya kutoa huduma bora za afya zikiwamo za ubingwa wa hali ya juu pamoja na upasuaji katika maeneo mbalimbali.

Msaada huo uliotolewa kwa hospitali hiyo una thamani ya Dola za Marekani 675,000 sawa na Sh bilioni 1.5 ambao ulikwenda sambamba na uzinduzi wa wodi ya watoto yenye vitanda 25.

Katika uzinduzi huo, Waziri Ummy, ameitaka Muhimbili kutokutoa rufaa kwa mgonjwa yeyote ambaye anaweza kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.

Vyumba hivyo vya upasuaji vimewekewa vifaa vya upasuaji kwa msaada wa mfuko wa Arch Wood Foundation ya Scotland.

“Napenda kuwashukuru kwa namna ya pekee wahisani wetu Sir. Ian Wood na mtoto wako, Garret Wood, ambao mlipoletewa wazo la kuisaidia Hospitali ya Taifa Muhimbili kupitia taasisi yenu ya Archie Wood Foundation, mlilipokea kwa mikono miwili na kulitekeleza.

“Nichukue nafasi hii kwa niaba ya Serikali chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli, kuwashukuru sana kwa msaada huu,” alisema Ummy.

Waziri ameutaka uongozi wa Muhimbili kuweka mpango mzuri wa matengenezo kinga ili kuhakikisha kila kifaa kinatunzwa na kutumika kwa lengo lililokusudiwa.

Naye Mkurugenzi wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru, alisema msaada uliotolewa na mfuko huo ni taa za kufanyia upasuaji, mashine za usingizi, mashine za kuzuia damu isiendelee kupotea wakati wa upasuaji, mashine ya kusafisha vifaa vya upasuaji na vifaa vyake, vitanda vya kufanyia upasuaji  na vifaa mbalimbali vya upasuaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles