Ronaldo ataibeba Juventus Ligi ya Mabingwa wiki hii?

0
1090

NA BADI MCHOMOLO

HATUA ya mwisho ya 16 bora ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, inatarajiwa kufikia mwisho wiki hii huku timu nane zikitarajia kuyaaga mashindano hayo wakati huo nne zingine zikiingia robo fainali.

Tayari wiki iliopita timu nne zilifanikiwa kutangulia hatua hiyo ya robo fainali, timu hizo ni Ajax, Tottenham, FC Porto na Man United, wakati huo Real Madrid, Borrusia Dortmund, AS Roma na PSG wakiyaaga mashindano hayo.

SPOTIKIKI wiki hii imekufanyia uchambuzi kuelekea michezo hiyo minne ya wiki hii kwa kuangalia nani ana nafasi ya kusonga hatua ya robo fainali kutokana na kile walichokifanya katika michezo yao ya awali kabla hii ya marudiano.

Man City vs Schalke 04

Kikosi cha Manchester City msimu huu kipo kwenye kiwango cha hali ya juu hasa kwenye michuano ya Ligi Kuu England kama ilivyo msimu uliopita.

Ushindani mkubwa upo kwenye michuano hii ya Ligi ya Mabingwa kutokana na timu zinazokutana kutozoeana kama ilivyo kwenye Ligi Kuu.

Kesho Man City watakuwa kwenye uwanja wa nyumbani Etihad wakiwakaribisha wapinzani wao Schalke 04, mchezo huo hautokuwa rahisi japokuwa Man City wapo nyumbani na ni bora msimu huu chini ya kocha wake Pep Guardiola.

Mchezo wa awali Schalke 04 walikuwa kwenye uwanja wa nyumbani lakini walikubali kichapo cha mabao 3-2, hivyo wana kibarua kizito kuanzia mabao 2-0 bila ya kuwaruhusu Man City wapate bao jambo ambalo linaonekana kuwa ngumu kutokana na ubora wa safu ya ushambuliaji na kiungo.

Kwa kuwa Man City kesho watakuwa kwenye uwanja wa nyumbani watahakikisha wanashinda mchezo huo ili kujihakikishia wanaingia hatua ya robo fainali na kuungana na Waingereza wenzao Tottenham ambao wametangulia hatua hiyo.

Juventus Vs Atletico Madrid

Huu ni moja kati ya mchezo ambao utateka hisia za watu wengi kutokana na ushindani wa timu hizo na ubora wake.

Mchezo uliopita Atletico wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani waliweza kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wapinzani hao ambao walikuwa na nyota wao Cristiano Ronaldo.

Macho ya wengi kesho ni kuona Ronaldo atafanya nini kwenye mchezo huo ataweza kukifanya ili kuweza kuinusuru na kuingia robo fainali.

Kinacho wabeba Atletico Madrid ni mifumo ya kocha wao Diego Simon pamoja na umoja wa wachezaji wake wakiwa uwanjani.

Kitu ambacho atakifanya kocha huyo ni kuhakikisha walinzi wake José Giménez, Diego Godín, Juanfran na Filipe Luis wanakuwa katika ubora wao kwa ajili ya kumzuia Ronaldo na wenzake.

Wakati huo Ronaldo anataka kuonesha kwamba alikuwa muhimu kwenye kikosi cha Real Madrid kwa misimu mitatu mfululizo iliopita na sasa timu hiyo imeshindwa kufanya vizuri mara baada ya yeye kundoka, hivyo mchezo huo utakuwa na ushindani wa hali ya juu. 

Bayern Munich Vs Liverpool 

Mchezo uliopita Liverpool wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani hawakuweza kuonesha makali yao japokuwa walitengeneza nafasi nyingi, hivyo mchezo huo ulimalizika kwa timu hizo kutoshana nguvu bila ya nyavu kutikisika.

Mchezo huo ambao utapigwa kesho kutwa, timu yoyote ina nafasi ya kufanya vizuri, lakini Bayern Munich ambao wana uzoefu wa michuano hiyo wanapewa nafasi kubwa kwa kuwa wapo kwenye uwanja wa nyumbani.

Liverpool msimu uliopita walikuwa kwenye kiwango cha hali ya juu na waliweza kufika fainali lakini wakashindwa kufanya vizuri mbele ya Madrid, hivyo msimu huu wanatafuta tena nafasi hiyo, lakini wanaonekana kuwa na wakati mgumu kwenye mchezo huo wa marudiano kwa kuwa walishindwa kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani Anfield.

Barcelona Vs Lyon 

Huu ni mchezo mwingine ambao utapigwa kesho kutwa, huku Barcelona wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani wa Camp Nou.

Baada ya kutoka bila ya kufungana katika mchezo wa awali, Barcelona wanataka kumaliza nguvu zao kwenye uwanja wa nyumbani huku wakiamini mshambuliaji wao Lionel Messi ambaye yupo kwenye kiwango kizuri msimu huu anaweza kuamua matokeo.

Barcelona ina kikosi ambacho kimekamilika, hivyo itakuwa ngumu kuwaruhusu wapinzani wao wakatamba kwenye uwanja huo, lakini chochote kinaweza kutokea kwa kuwa soka ni mchezo wa makosa.

Vinara hao wa Ligi Kuu nchini Hispania, wanataka kuonesha kuwa wao ni bora mara baada ya wapinzani wao Real Madrid kuondolewa, hatokuwa mchezo rahisi kwa kuwa hakuna timu ndogo, kila timu inaamini inaweza kupata matokeo kikubwa ni kutumia nafasi zitakazotengenezwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here