30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

RIPOTI: UCHAFUZI WA MAZINGIRA UNAUA KULIKO VITA, NJAA

KWA miongo mingi uchafuzi na athari zake mbaya kwa afya za binadamu, mazingira na sayari kwa ujumla wake umeonekana kutoangaziwa katika ajenda za kiserikali na jumuiya ya kimataifa.

Lakini usisahau kuwa uchafuzi ni sababu kuu ya kimazingira zinazosababisha maradhi na vifo katika dunia ya leo.

Unahusika na vifo vya mapema karibu milioni tisa kwa mwaka, ikiwa ni sawa na asilimia 16 ya vifo vyote duniani, kwa mujibu wa utafiti mpya.

Utafiti huo uliohusisha watafiti zaidi ya 40 kutoka serikali na vyuo vikuu kote duniani kupitia Tume ya Uchafuzi na Afya ulifadhiliwa na Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Ulaya (EU) na Marekani.

“Hii ni kipande muhimu cha kazi kinachoangazia athari za uchafuzi wa kimazingira kwa vifo na maradhi,” anasema Dk. Maria Neira, Mkurugenzi wa Afya ya Umma na Mazingira wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

“Huu ni upotevu usiokubalika wa maisha na mwelekeo wa maendeleo ya binadamu,” anasema.

 

Idadi hiyo ni mara tatu zaidi ya vifo vilivyotokana na maradhi ya Ukimwi, Kifua Kikuu, uvutaji wa sigara na Malaria unapovijumuisha kwa pamoja.

Aidha, ni mara 15 zaidi ya vifo vilivyosababishwa na vita na aina nyingine ya machafuko katika maeneo mbalimbali duniani.

Ripoti inaonesha hakuna nchi ambayo haijaathirika na uchafuzi duniani isipokuwa tu viwango vya uathirika vinatofautiana.

Shughuli za binadamu ikiwamo viwanda, kukua kwa miji na utandawazi, yote ni kichocheo cha uchafuzi wa mazingira.

Ripoti hiyo kupitia uchambuzi wa takwimu zilizopo na mpya kutoka WHO na vyanzo vinginevyo pamoja na mambo mengine ilitathimini athari za kiafya na kiuchumi kwa aina tofauti ya uchafuzi.

Kwa mara ya kwanza ilihusisha pamoja na uchafuzi wa hewa, maji, ardhi na mahala pa kazi.

Katika nchi zilizoathirika zaidi na uchafuzi, maradhi yanayotokana na hali hiyo yanahusika na zaidi ya kifo kimoja kwa kila vifo vinne na husababisha athari kubwa za kiuchumi.

Aidha, kwa mujibu wa utafiti huo uliochapishwa katika Jarida la Tiba la Lancet, karibu nusu ya vifo vya jumla hutokea katika nchi mbili tu.

Kulingana na utafiti huo, moja ya kila sita ya vifo milioni tisa vya mapema kote duniani katika mwaka wa 2015, vinaweza kuhusishwa na magonjwa yanayosababishwa na sumu katika hewa au maji.

Ripoti hiyo ilibaini uchafuzi wa hewa ulikuwa muuaji mkuu ukiyaongoza maradhi ya moyo, kiharusi, saratani ya mapafu na magonjwa mengine.

Uchafuzi wa hewa ya nje ukisababishwa zaidi na magari na viwanda husababisha vifo milioni 4.5 kila mwaka huku vifo kutokana na hewa ya majumbani kama vile kuni ikisababisha hupoteza watu milioni 2.9.

Muuaji mwingine mkubwa ni uchafuzi wa maji mara nyingi kutokana na taka akiua watu milioni 1.8 kwa mwaka.

 

Asilimia 92 ya vifo vinavyotokana na uchafuzi wa mazingira vilitokea katika nchi zinazoendelea zenye mapato ya chini au ya kati, huku India ikiongoza kwenye orodha kwa milioni 2.5, ikifuatiwa na China  vifo milioni 1.8.

India imeathirika kwa njia zote mbili za uchafuzi unaotokana na kienyeji na kisasa huku Urusi na Marekani pia zikiwa ndani ya vinara 10.

Linapokuja suala la vifo vinavyohusiana na uchafuzi wa mahali pa kazi Uingereza, Japan na Ujerumani zinaonekana kuongoza miongoni mwa vinara hao 10

Ripoti hiyo pia imeonyesha  gharama kubwa zinazotokana na vifo vinavyosababishwa na uchafuzi wa mazingira, magonjwa na ustawi.

Umekadiria gharama hizo kufikia dola bilioni 4.6 katika hasara za kila mwaka – au sawa na  asilimia 6.2 ya uchumi wa dunia.

“Kile ambacho watu hawafahamu ni kwamba uchafuzi wa mazingira unaathiri uchumi. Watu ambao ni wagonjwa au wafu hawawezi kuchangia katika uchumi, wanahitaji kutunzwa,” anasema mmoja wa waandishi wa utafiti huo, Richard Fuller.

Fuller ni mkuu wa shirika la kimataifa linalochunguza masuala ya uchafuzi wa mazingira la Pure Earth.

Kulingana na utafiti huo, mzigo wa kifedha pia unaathiri nchi maskini zaidi, na nchi za kipato cha chini zikitoa asilimia 8.3 ya Pato la Ndani (GDP)  ili kukabiliana na madhara yaliyosababishwa na uchafuzi wa mazingira, ikilinganishwa na asilimia 4.5 katika nchi tajiri.

Mataifa tajiri yana mengi ya kufanya kukabiliana na uchafuzi wa mazingira: Marekani na Japan wako juu ya vinara 10 wa vifo vinavyotokana na aina ya kisasa ya uchafuzi, kama vile hewa sumu inayotokana na mafuta na kemikali za viwandani.

Lakini wanasayansi wamesema mafanikio yanaonekana kwa upande wa mataifa yaliyoendelea katika miongo ya karibuni katika kukabiliana na uchafuzi na kwamba ushindi utapatikana kukiwepo utashi wa kisiasa.

“Uchafuzi ni moja ya changamoto kubwa kabisa katika kipindi hiki,” ilhitimisha ripoti hiyo iliyochapishwa katika jarida hilo Ijumaa iliyopita.

Profesa Philip Landrigan, wa Shule ya Tiba ya Icahn nchini Marekani ambaye ni mwenyekiti mwenza wa tume hiyo anasema:

“Vifo kutokana na uchafuzi wa hewa kusini mashariki mwa Asia vinazidi kuongezeka na vitapanda maradufu ifikapo mwaka 2050 iwapo hatua za makusudi hazitachukuliwa.

Landrigan anasema kiwango cha vifo kutokana na uchafuzi kimewashangaza wanasayansi na sababu kubwa ya tishio hilo kupuuzwa miaka mingi ni pamoja na:

Kwamba dunia haikuwa ikifahamu tishio la vifo vinavyotokana na uchafuzi wa ‘kisasa’ wakati vile vinavyotokana na njia za kienyeji kama vile maji na kuni vikipungua kutokana na hatua zilizochukuliwa.

Aidha, wanasayansi bado wanaendelea kugunduia uhusiano baina ya uchafuzi na maradhi kama vile uhusiano baina ya uchafuzi wa hewa na maradhi ya akili au kusahau, kisukari na figo.

Wahariri wa Lancet, Pamela Das na Richard Horton wanasema ripoti hii imekuja wakati wa hofu, kipindi ambacho Shirika la Ulinzi wa Mazingira la Serikali ya Marekani  (EPA) likiongozwa na Scott Pruitt likikandamiza kanuni imara za kulinda mazingira.

Pruitt alitangaza mwezi huu kuwa Marekani, ambaye ni msababishaji mkubwa wa uchafuzi wa hewa na gesi chafu kuwa itajitoa kutoka katika mpango wa kuzalisha hewa safi ulioundwa na aliyekuwa Rais Barack Obama.

Mpango huo, ambao ulilenga kupunguza utoaji wa hewa ya sumu ya carbon dioxide kutokana na uzalishaji wa umeme ulitarajiwa na EPA pia kupunguza ukungu na masizi kwa asilimia 25 na hivyo kuepuka maelfu ya vifo vya Marekani kupitia maradhi ya pumu na mapafu.

Das na Horton wanasema matokeo haya yanapaswa kuwa ‘wito wa kutaka hatua zaidi zichukuliwe.’

“Uchafuzi unaelekea kushinda vita, vizazi vya sasa na baadaye vinahitaji dunia iliyo huru na uchafuzi,” walisema.

Masuala yote muhimu yanatarajiwa kuwasilishwa wakati wa Mkutano wa mwaka huu wa Umoja wa Mataifa wa Mazingira utakaofanyika mjini Nairobi, Kenya Desemba 4-6.

Mawaziri wa mazingira kutoka mataifa wanachama pamoja na taasisi zisizo za kiserikali na sekta binafasi watahudhuria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles