23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

RIPOTI MAALUMU: MRADI WA MTAMBO GESI LNG WADODA

Aina ya meli zinazobeba shehena ya gesi ya LNG.
Aina ya meli zinazobeba shehena ya gesi ya LNG.

Na Mwandishi Wetu,

MATUMAINI ya Watanzania kupata mapema faida za mradi wa gesi iliyogunduliwa Lindi miaka 15 iliyopita yamedoda kwani juhudi za Serikali kulazimisha mradi huo utekelezwe haraka zimegonga mwamba kwa wadau wa mradi huu kuonesha hawako tayari hadi miaka mitatu ya kujadiliana iishe na kuandika sheria mpya ya kuyapendelea makampuni matano ya mradi huo.

Kampuni hizo ni kampuni za kimataifa za gesi na mafuta za Statoil (Norway) BG Group na Ophir  Energy (Uingereza) Exxon Mobil (Marekani), wakishirikiana na Tanzania Petroleum Development Corporation (TPDC) kama  kampuni ya Taifa ya Mafuta Tanzania  (NOC) zijadiliane kwa awamu tano ni mijadala itakayochukua miaka mitano.

Hali hiyo tata imekatisha tamaa watu wengi na kuitaka Serikali itafute wawekezaji wengine ili mambo yaende shoti kuliko kutumia magwiji hawa ambao wana vitimbi na ajenda ya siri kwani kimsingi hawana shida yoyote ya kifedha.

Kwa maana hiyo ndiyo sababu BG Group bado ipo kwenye kundi ingawa  rasilimali yake alikwishamuuzia Royal Dutch Shell  kwa dola bilioni 55 na inadaiwa na TRA kodi ya ‘capital gains tax’.

Haitaki kulipa ikisubiri sheria zibadilishwe na zilengwe kuwanufaisha wao au Serikali iuze gesi hiyo bei ya jumla ya kutupa na waachane nayo.

Wanoko wa masuala ya uchumi  wanasema kuwa Nigeria ilipata na kuendelea kuteseka na kampuni hiyo eneo la Ogoni katika Delta ya Niger na  hivyo ikiingia hapa itafanya kasheshe mpaka nchi hii tukome kwanini tulikuwa na gesi.

Ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi ya LNG ni muhimu ili kuweza kuuza gesi yetu nje ya nchi ikiwa kama  kichuruzika (liquid) kwa kila hali ni mchakato mrefu na mgumu na sasa ndio kwanza umeanza kwenye hatua inayoitwa Host Government Agreement (HGA).

Yaani hayo ni mapatano kati ya Serikali na kampuni hizo za uchimbaji za nje na mahusiano yao.

“HGA ni makubaliano ya kisheria kati ya mwekezaji wa nje na Serikali ya nchi inahusu haki na wajibu  wa mwekezaji kuhusu uendelezaji, ujenzi na uendeshaji  wa mradi na mwekezaji wa nje. Huweka misingi ya utendaji kazi na mahusiano,” anasema  Prof. Ntalikwa.

Agosti mwaka jana, Rais Dk. John Magufuli, aliagiza Wizara ya Nishati na Madini  kuongeza juhudi kwenye mradi wa mtambo wa kuchakata gesi ya LNG ili mradi huo wa dola bilioni 30 au shilingi trilioni 65 haucheleweshwi na vikwazo vya urasimu na kutowajibika kwa upande wa Serikali.

Rais Magufuli alisisitiza  kutaka kuona mradi unakwenda mbele, hakujua kuwa suala hilo ni kizungumkuti na lina  masilahi ya wengi na hivyo litakwenda tu kwa makubaliano ya wengi (consensus) na huliwezi kulipangia ratiba mjarabu ila kwa maelewano.

Rais Magufuli alizungumzia hayo akiwa Ikulu baada ya kupata taarifa ya mradi  wa gesi kutoka kwa Meneja wa Statoil  nchini Tanzania, Oystein Michelsen,  ambaye alisema itachukua miaka mitano kufikia uamuzi wa kuwekeza (final  investment decision).

Wengi walishangaa na ucheleweshaji huo lakini mambo yanavyokwenda inaonekana itakuwa hivyo.

Tokea mwanzo ilionekana kutokubaliana na kiu na ari ya kuwekeza kwa pande hizo mbili ambapo wakati Magufuli anataka mradi uende haraka, Statoil kwa niaba ya wadau wawekezaji hawana haraka na kuonekana kusubiri hali fulani ya soko la mafuta au biashara ya gesi na hivyo ndivyo itakavyokuwa mpaka  gesi tuiuze kwa bei ya kutupa kutokana na njaa ya fedha.

Rais alifikiri kuwa ni maofisa wa Serikali ni kikwazo lakini sasa iko wazi kuwa kampuni za mafuta ndio tatizo.

Profesa Justin Ntalikwa  ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini  ambaye  amesema kwenye vyombo vya habari kuwa  timu ya wataalamu wa Serikali wako kwenye majadiliano na kampuni za mafuta hizo tano kujenga Mtambo huo wa LNG.

Katibu Mkuu huyo alisema chini ya HGA pande hizo mbili watatengeneza  miundo ya kifedha ambayo itaamua namna gani bei ya gesi itakavyopangwa, masuala ya ardhi na mengine yanayohusiana nayo.

Mambo yaliyopo mezani ni pamoja na kampuni hizo kutaka sheria mahususi itakayotumika katika mradi huu kabambe  na kudai HGA iwe sehemu ya hiyo sheria.

Prof. Ntalikwa anasema katika majadiliano hayo yataamua kutumia sheria zilizopo za gesi na mafuta au kutunga mpya na hasa ikizingatiwa  kuwa kutaka sheria mpya kunaweza kuhitaji mwaka mmoja zaidi ili kuipata.

Anasema majadiliano ya aina hii huchukua muda mrefu na inaweza kuchukua zaidi ya miaka mitatu kuanzia mwaka jana (2016).

Baada ya hapo kampuni hizo zitaunda timu ya usanifu wa mbele wa mradi yaani  Front End Engineering Design (FEED), ni usanifu wa msingi baada ya usanifu wa awali  (Conceptual design) au  Feasibility Study na FEED design inajizatiti juu ya usanifu wa kifundi (Technical Design) na kutolewa makisio  ya gharama ya mradi  kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho wa uwekezaji (Financial Investment Decision (FID).

Hayo ni majumuisho  na uamuzi wa mwisho kuhusu uwekezaji wa mtaji (Capital Investment Decision) CID ikiwa ni sehemu ya matumizi ya muda mrefu wa shirika katika  vianishi vya namna ya kutawala na kuendesha rasilimali za kampuni na muundo wa mtaji.

Prof. Ntalikwa anasema ana imani itakapofikia  mwaka 2020  mradi utafikia  michoro ya msanifu majengo na kila kitu kitakamilika ifikapo mwaka 2029.

Uko hapo? Anasema ni safari ndefu lakini hakuna jinsi ya kufanya.

Wananchi wanataka leo si kesho

Taarifa ya kuchelewa mradi imeleta sononeko kwa watu wengi kwa utafiti mdogo uliofanywa na Mtanzania, ambao walifikiri matatizo yao ya uchumi yamekwisha kwani Serikali ingepata uwezo mkubwa katika huduma za jamii ikiwa ni pamoja na elimu, afya, maendeleo ya miundombinu mbalimbali na ustawi wa maendeleo kwenye uchumi.

Kwa kifupi ni utajirisho ambao unaonekana sasa kucheleweshwa na kukubali kuzugwa na mahitaji ya wawekezaji na kutaka Serikali ifanye mazungumzo na wawekezaji wengine ili tupate maendeleo haraka kwani mwenye shibe hamjui mwenye njaa.

Wengi wanafikiri China inaweza ikaisaidia Tanzania vizuri zaidi kuliko hawa wengine kwani wana matatizo ya kisera na kimtazamo kwani wamezoea vya kunyonga na hivyo vya kuchinja hawaviwezi.

Ni kweli la kuvunda halina ubani, lakini kwa vigezo vya miradi kama hii sehemu nyingine ulimwenguni imechukua muda mfupi zaidi  na hivyo ni vizuri kwa uongozi Petroleum Upstream  Regulatory Authority (PURA) na Tanzania Petroleum Development Corporation (TPDC) pamoja na wizara wakachukua hatua nyingine za ziada kuharakisha  kwani suala hili linatawaliwa na siasa vile vile  na hivyo linaweza kuvurugika.

Kule Ghana na Nigeria muda uliotumika toka uvumbuzi hadi kuuza gesi na mafuta ni chini ya miaka sita na hivyo kuna nafasi ya kujadiliana badala hiyo ya kwetu ya miaka 20, kuna haja ya Serikali kuchunguza kwa  makini  na undani zaidi.

Hatari za kisiasa (political risks)  ni kubwa na zinaweza kuukwamisha mradi  na kufanya ndoto ya Watanzania ikaishia kuwa ndoto. Ni lawama tupu!

Mengineyo

Gesi ya Tanzania kiwango chake kimefikia ujazo wa futi mraba trilioni  57.27 na wawekezaji ni hao watano ambao wameainishwa hapo awali.

Timu hiyo ya majadiliano itajadili faida kwa Tanzania katika kile kinachoitwa maudhui ya nyumbani (local content) masoko ya gesi na maamuzi kwa kiasi gani kitauzwa nyumbani na kiasi kipi kitauzwa nje na nani ili kulipia madeni ya utafutaji na uendelezaji.

Wazo la jumla ni kujenga Mtambo wa LNG wa nchi kavu karibuni kilomita 120 kutoka baharini na makisio ya awali ni gharama ya dola bilioni 30 sawa na shilingi trilioni 65 katika ardhi ya hekta 20,000 ambapo 18,000 zitakuwa kwa viwanda na hekta 2,000 kwa Mtambo wa LNG pale Likong’o Lindi.

Mtaalamu alonga

 Neema Lugangira ni mtaalamu wa Kujitegemea wa Masuala ya Maudhui (Local Content) anayeishauri Serikali  katika Ofisi ya Waziri Mkuu nini cha kufanya kuhusu suala la gesi na ujenzi wa Mtambo wa LNG  na anasema kuna haja ya kuyaelewa baadhi ya mambo ambayo kwasasa ni nyeti lakini ni muhimu watu kuwa nayo kichwani ili yasije yakapotoshwa na wajanja na kuleta purukushani katika jamii. Ni rahisi kutoeleweka katika masuala hayo ambayo yana mahitaji tata na yanayokinzana toka sehemu nyingi za uchumi.

Anasema Serikali imechagua kuwa na mtambo nchi kavu wa LNG badala ya baharini ili kuhakikisha kuwa Tanzania inafaidika vilivyo kwa kuona inashiriki katika shughuli za mwenendo wa mtambo kwa urahisi zaidi. Nchi ya Msumbiji kwa kufananisha, imeamua kuwa na mitambo yote miwili ya kuelea (floating plant) na ule wa nchi kavu (onshore plant) kuvuna rasilimali yake inayokadiriwa kufikia futi za mraba trilioni 185 mara tatu ya hazina ya Tanzania.

Anasisitiza kuwa ni muhimu kwa Tanzania na wananchi wake kushiriki  kikamilifu na kuvuna faida ya shughuli hizo za  uchumi wa gesi na zinazoendana nazo.

Mtaalamu huyo ambaye ndio mwasisi wa kitengo cha maudhui ya nchi (local content) ofisi ya Waziri Mkuu anasema Mtambo wa Baharini hautoi fursa nzuri ya kushiriki kwa ukamilifu kwa kampuni  zetu za nyumbani.  

Kutokana na Msumbiji kuwa na mpango wa mtambo wa kiboya (floating plant), wao watatutangulia kuwa na LNG plant na hivyo watakamata mwanzo masoko.

Neema anaupongeza msimamo thabiti wa Tanzania lakini wawekezaji hawautaki kwani unapunguza kula yao na kuchelewesha kulipa deni la ujenzi wa mtambo na hivyo ni shubiri kwao.

“Tanzania inakusudia kulinda masilahi ya nchi na hivyo kusisitiza kuwa asilimia 10 ya gesi iwe ni kwa matumizi ya soko la nyumbani pekee bila kujali inatumika au hapana,” alidokeza Neema.

Anasema nchi lazima iweke kikomo cha chini cha kutumika na kubaki nyumbani vinginenvyo wawekezaji watapenda kuondoka na kila kitu  na kusafirisha nje na kuwaacha mtupu ndani ya nchi. Hata tukiagiza gesi nje tutahitaji LNG Plant kwani gesi ni chanzo rahisi cha kuzalisha  umeme kwa matumizi ya viwanda, uzalishaji viwandani na kwa usafiri wa magari. Ni mradi wa kudumu kwa miaka 40 ijayo.

Kuzingatia mambo yake yaende kama ilivyopangwa Tanzania ina Mpango Kabambe wa Matumizi ya Gesi yaani  National Gas Use Master Plan (NGUMP) ambao kazi zake ni pamoja na kutoa mwongozo na dira ya matumizi ya gesi asilia nchini.

Matokeo chanya ya shughuli ya gesi itawezekana kupatikana kwa mapana tu kama nchi itajizatiti kwenye maudhui ya nyumbani ambayo italeta uwezo wa kupata ziada ya kuwekeza na kushiriki kwenye shughuli za gesi na hivyo kuongeza uwezo wa uchumi kufanya mengine yanayostahili.

Suala la ajira lipo tu wakati wa ujenzi wa LNG plant, lakini ajira itanywea wakati  ujenzi ukikamilika na uendeshaji wa kiwanda  kuwa wa kitaalamu zaidi ambapo watu wachache wenye ujuzi stahiki nchini wataajiriwa  na wageni ndio watatawala kiajira kutokana na ujuzi wao maalumu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles