23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

RIPOTI MAALUM: MAJI YA ARDHINI HATARINI KUTOWEKA KATIKA KARNE HII

akivuna

VITABU vya dini vinasema maji ni neema iliyoshushwa kwa ajili ya binadamu, ulimwengu na viumbe vilivyomo kwa ujumla wake.

Na linapokuja suala la kisayansi, maji ni molekule yenye atomi mbili za haidrojeni na atomi moja ya oxygen. Kwa maneno mengine molekule hizo ndizo zinazounda kitu kiitwacho maji.

Maji hupatikana kutoka katika chemchem, mvua na vyanzo vingine vingi tu kama vile maji madini ya visima virefu na kadhalika.

Umuhimu wa maji kwa binadamu ni mkubwa kupita maelezo kiasi kwamba wataalamu wa afya wa aina zote duniani wamekiri kuwa maji ndio uhai.

Unaweza ukanywa, ukaoga, ukapikia, ukaoshea, ukanyweshea mifugo, mazao mashambani,  kujaza mabwawa kwa ajili ya nguvu ya umeme.

Kupoza mitambo ikiwamo magari bila kusahau shughuli za kiroho kama vile kubatiza, masuala ya kuapisha na mengineyo mengi.

Baada ya oksijeni, maji ndicho kitu muhimu kinachohitajika ili kiumbe hai aweze kuishi mbali pia ya chakula, ndiyo maana wanasema maji ni uhai.

Kama tulivyoona maji yanatokana na vyanzo mbalimbali yakiwamo yale yatokayo chini ya ardhi (groundwater), ambayo ndiyo makusudio ya makala haya.

Maji ya chini ya ardhi, ambayo huvunwa kwa njia mbalimbali ikiwamo visima ni chanzo muhimu kabisa cha maji safi.

Maji haya ya ardhini husaidia watu bilioni mbili kwa ajili ya kunywa na shughuli za umwangiliaji zinazochangia sehemu kubwa ya uzalishaji chakula duniani.

Kwa mfano nchini Marekani, maji ya ardhini yanachangia kutoa maji ya kunywa kwa asilimia 51 ya Wamarekani wote na asilimia 99 ya watu waishio vijijini.

Asilimia 64 ya maji ya ardhini hutumika kwa shughuli za umwagiliaji mazao na ni muhimu kwa sekta ya viwanda kwani ni chanzo cha nishati katika maziwa, mito na kadhalika.

Hata hivyo, katika maeneo mengi duniani, akiba ya maji ya ardhini imekuwa ikipungua siku hadi siku.

Akiba hii imekuwa ikivunwa kwa kasi kuliko kiwango kile cha uzalishaji wake, ambacho kinahusisha maji ya mvua yanayopenya hadi ardhini.

Licha ya changamoto hiyo inayoashiria mwelekeo mbaya wa huko mbele, mataifa hayaonekani kushtuka na hivyo hakuna juhudi zozote za kushughulikia wasiwasi huo.

Wakati mataifa mengine hasa ya Kiafrika hayana hili wala lile kuhusu hatari hii ya kutoweka kwa maji ya ardhini, kwa yale mataifa yanayofahamu uwapo wa hatari hii hayaonekani kulipa uzito suala hilo.

Naam, hayaonekani kuwa na utashi wa kutosha kuilinda au kutafuta njia mbadala ya kukabiliana na hatari hii dhidi ya kutoweka kitu ambacho kitakuja kuathiri mifumo ya kimazingira na kijamii na kiuchumi duniani.

Mbaya zaidi wakati kipindi cha miongo iliyopita, mahitaji ya maji ya adhini yamekuwa yakiongezeka maradufu na yataendelea bado kupaa kwa kadiri ya ukuaji wa idadi ya watu na mabadiliko ya tabia nchi.

Kwakweli athari hizi mbaya zimeanza kubainika baada ya Shirika la Jiofizikia la Marekani kutoa ripoti mpya likisema katika miongo kadhaa ijayo, matumizi ya maji ya binadamu huenda yakasababisha maji yaliyoko chini ya ardhi kutokomea huko India, Ulaya, Australia  na baadhi ya sehemu nchini Marekani.

Ardhi au mwamba majimaji (porous rocks) yenye kutoa maji ya ardhini katika Bonde la Mto Ganges nchini India, kusini mwa Hispania na Italia na maeneo ya Australia itatokomea kati ya mwaka 2040 na 2060.

Nchini Marekani maji ya ardhini katika Bonde la California Kati, Bonde la Tulare na kusini mwa Bonde San Joaquin, akiba hiyo inaweza kutokomea ndani ya miaka ya 2030.

Aidha, katika nyanda za juu kusini, ambazo zinasambaza maji ya ardhini katika sehemu za Texas, Oklahoma na New Mexico, akiba inaweza kufikia ukomo wake kati ya miaka ya 2050 na 2070 kwa mujibu wa utafiti huo mpya.

Mtalaamu wa maji wa Chuo cha Madini cha Colorado cha Marekani, Inge de Graaf alipotoa hotuba kwenye mkutano wa mwaka wa shirika hilo anasema ifikapo miaka ya 50 katika karne hii kutokana na matumizi ya kupita kiasi ya maji yaliyoko chini ya ardhi, watu bilioni 1.8 duniani wataishi katika maeneo yasiyo na maji ya chini ya ardhi.

Graaf anasema; India, Ulaya na baadhi ya sehemu nchini Marekani zitakabiliwa na hali mbaya zaidi huku China itakuwa nzuri kidogo, na sehemu ya kusini mwa China zitakuwa nzuri zaidi kuliko kaskazini mwa nchi.

Kabla ya hapo, Shirika la Anga ya Juu la Marekani NASA na idara nyingine zimetafiti maji yaliyoko chini ya ardhi duniani kupitia takwimu zilizokusanywa na satelaiti.

Katika tafiti hizo, shirika na idara hizo ziligundua kuwa kiasi cha maji kinapungua kwa kasi ya kushangaza katika matabaka kadhaa makubwa yenye udongo na mawe yenye mashimo mengi ambayo yanafaa kuhifadhi maji duniani.

Graaf na watafiti wengine walikadiria muda wa kuendelea kuwapo wa maji ya chini ya ardhi kwa kutumia takwimu hizo, ambazo zimehitimisha ni katikati ya karne hii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles