RC SHIGELA AMWONYA MKURUGENZI LUSHOTO

0
3

NA OSCAR ASSENGA-TANGA



MKUU wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella amemwonya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto mkoani humo, Kazimbaya Makwega kuacha kutaka ukubwa na kupandikiza migogoro.
Alimtaka badala yake atumie nafasi aliyonayo kuwaunganisha watumishi.

Onyo hilo alilitoa jana kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC).
Alisema hakuna haja ya kuendelea na migogoro ndani ya halmashauri hiyo kwa kuwa haina tija kwa wananchi.

RC alisema jukumu la mkurugenzi ni kuwaunganisha watendaji wake na kupinga migawanyiko inayojitokeza ambayo inaweza kajenga chuki baina ya watumishi na viongozi wa siasa.

“Labda niseme kitu, Mkurugenzi wa Lushoto upo hapa… ndugu yangu ukipenda ukubwa utapata shida, jaribu kuishi na kufanyakazi na jamii zote bila ya kubagua.
“Lazima uwaunganishe watumishi badala ya kuwaacha wakijigawa, tutakuwa tunashindwa kupata maendeleo,” alisema Shigella.

Alisema azma ya Serikali ni kuwatumikia wananchi waweze kuondokana na kero walizonazo badala ya kuendelea kulumbana na kukuza migogoro isiyokuwa na tija kwa maendeleo ya wananchi.

Pia aliutaka uongozi mzima wa halmashauri hiyo kupunguza misuguano isiyokuwa na tija badala yake waone namna bora ya kuwaunganisha wananchi kuchangia juhudi kubwa za maendeleo.

Alisema ni jambo la ajabu kwa uongozi wa halmashauri kuacha kutekeleza majukumu yao.
Ni vema waepushe misuguano ambayo madhara yake ni makubwa kwa ukuaji wa maendeleo ya wananchi wanaowaongoza, alisema.

Pia alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, January Lugangika kusimamia vema changamoto zinazochangia kuibuka migogoro ya mara kwa mara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here