31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

RC awataka viongozi, watendaji wawajibike inavyopaswa

Na BENJAMIN MASESE

 MKUU wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, amewaonya    na kuwataka watumishi katika mkoa huo    kila mmoja abebe msalaba wake.

Amewasisitizia kufanya kazi, kuacha visingizio  na  kila mtu awajibike  kwa nafasi yake  kutekeleza mipango na maelekezo ya Serikali.

Mongella alikuwa akizungumzia hatua ya wananchi    kujitokeza na mabango wakati wa ziara za viongozi wa  taifa katika mkoa huo.

RC alisema hali hiyo haimpendezi na yeyote atakayezembea kuwahudumia wananchi kwa nafasi yake na malalamiko yakajitokeza kwa viongozi wa  taifa, atawajibishwa baadaye.

Alitoa angalizo hilo  huku kukiwa na taarifa  kuwa  Rais Dk. Magufuli anatarajiwa kuwasili mkoani Mwanza  Mei 11, mwaka huu   kutembelea shughuli mbalimbali za miradi ya maendeleo.

  Mongella alikuwa akizungumza katika kikao cha kupokea  taarifa ya utekelezaji wa  hatua ya  kuanzishwa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi  Tanzania (HPV) kwa wasichana wenye umri wa miaka 14  mkoani Mwanza.

Alisema imekuwapo tabia ya watumishi kupoteza muda kubishania jambo  fulani badala ya kutumia nguvu  kufanikisha mipango ya Serikali.

Mongella alisema wapo baadhi ya watumishi wanakwamisha mipango ya Serikali kutokana na tabia yao ya    visingizio vingi na kutaka wabembelezwe  kutimiza wajibu wao hata kupitisha barua wakati wameajiriwa kwa kazi hiyo.

Aliwataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi   kuwasilisha taarifa  kwake ya utekelezaji miradi  kila baada ya miezi mitatu.

“Hapa leo tunajadili suala la  chanjo ya saratani ya  mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 lakini tunashuhudia watumishi wanavyotafuta   visingizio kibao.

“Wanatumia muda mwingi kubishania jambo lisilo na maana badala ya kutumia nguvu kufanikisha kitu kilicho mbele yao.

“Tambueni hata vitabu vitakatifu vinasema kwamba mtu akibembelezwa kutimiza wajibu wake ni dhambi, sasa mimi sitaki kubeba dhambi ya mtu kisa hataki kutimiza wajibu wake kila mmoja abebe msalaba wake.

“Mnataka kiongozi aje hapa wa  taifa    wananchi wajitokeze  na mabango, sitakubali tutaajibishana.

“Twendeni vijijini tukawahudumie wananchi, mfano katika hili la saratani linakwamisha   maendeleo kwa sababu mama mmoja akiwa na saratani lazima familia itayumba hata kama wana uwezo wa fedha.

“Tambueni asilimia 80 ya shughuli za nyumbani zinafanywa na mama, bila kusimamia afya na uhai wa watu tutakuwa tunajidanganya kupata maendeleo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles