24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

RANIERI: LEICESTER CITY WAMEUA NDOTO ZANGU

LONDON, ENGLAND

ALIYEKUWA kocha wa klabu ya Leicester City, Claudio Ranieri, ameweka wazi kuwa, klabu hiyo imeua ndoto zake, ikiwa ni miezi tisa tangu kocha huyo awape ubingwa wa Ligi Kuu nchini England.

Uongozi wa klabu hiyo ulimfungashia virago kocha huyo usiku wa kuamkia Ijumaa, huku klabu hiyo ikidai kuwa, umefanya maamuzi hayo kuhofia kushuka daraja katika Ligi Kuu kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo.

Kocha huyo ameacha ujumbe kwenye klabu hiyo baada ya kutimuliwa na kudai kuwa anajisikia vibaya sana kwa maamuzi ambayo yamefanywa na klabu, lakini bado moyo wake utaendelea kuwa ndani ya klabu hiyo kwa kuwa anaipenda.

“Leicester City wameziua ndoto zangu. Baada ya kuchukua ubingwa msimu uliopita niliweka wazi kuwa nitapambana na klabu hiyo hadi hatua za mwisho kwa ajili ya kuendelea kuipa mataji mengine, lakini tayari wameua ndoto zangu.

“Ni jambo la kusikitisha sana kwa upande wangu kwa kuwa sikutegemea kabisa, lakini napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru mke wangu Rosanna pamoja na familia kwa ujumla kwa kuonesha sapoti yao katika kipindi chote wakati naitumikia klabu hiyo. Namshukuru sana Paolo na Andrea kwa kushirikiana katika safari yote. Pia nawashukuru Steve Kutner na Franco Granello kwa kunipa nafasi hadi nimeweza kuwa bingwa msimu uliopita.

“Hata hivyo, ni vizuri nikaishukuru klabu ya Leicester City, nafasi ambayo walinipa ni kubwa sana, hivyo wataendelea kuwa moyoni mwangu daima. Pia napenda kuwashukuru waandishi wa habari pamoja na vyombo vya habari kwa kuwa pamoja na sisi na kuandika historia kubwa katika soka mara baada ya kutwaa ubingwa.

“Napenda kuwashukuru watu wote ndani ya klabu, wachezaji wote pamoja na wale wote ambao walikuwa pamoja na sisi hadi tunafanikiwa kutwaa ubingwa. Siwezi kuwasahau mashabiki wote kwa kuwa walinichukua nikawa kwenye mioyo yao kuanzia siku ya kwanza, walionesha upendo na mimi nawapenda zaidi. 

“Hakuna ambaye anaweza kupoteza historia ambayo tumeiweka, ninaamini kila mmoja analijua hilo na tunafurahia hilo, ulikuwa ni muda wa kushangaza watu duniani na nilikuwa na furaha ambayo siwezi kuisahau katika maisha yangu,” alisema Ranieri.

Kocha huyo msimu uliopita alitwaa tuzo ya kocha bora wa mwaka, baada ya kuipa ubingwa klabu hiyo na baadaye aliweza kusaini mkataba wa miaka minne tangu Agosti mwaka jana, lakini kutokana na klabu hiyo kushika nafasi ya 17 katika msimamo wa Ligi, huku wakiwa mabingwa watetezi, uongozi umeona bora kumfukuza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles