30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

RAIS NICOLAS MADURO ANASABABISHA UCHURO VENEZUELA

NINGEKUWA na uwezo wa kubadilisha maisha ya viumbe kwa nafasi zao hapa duniani ningefanya hivyo kwa Rais wa Venezuela, Nicolas Moros Maduro, ningemgeuza paka ili abashiri uchuro wa mdororo wa Taifa hilo kwenye sekta nyingi zikiwamo hamkani za siasa zinazoporomosha uchumi.

 

Katika kubashiri uchuro huo angetoa sauti za mingurumo ya kihoro kama ambavyo paka hususani shume hufanya, wakitaka kutoa taarifa mbaya ikiwamo kufariki kwa mtu au ujio wa msiba kutokana na maumbile ya wanyama kuwa na uwezo wao kubaini mapema mambo ambayo binadamu hatuwezi. Lakini sina uwezo wa kufanya uhuisho wa uhai wa viumbe kama inavyoaminiwa katika imani nyingi kuhusiana na maisha baada ya kifo, ambapo baadhi huamini kuwa ukifa hurudi tena duniani katika umbile la mnyama mwenye nafasi husika kutokana na matendo yako ya awali hapa duniani, mathalan, kama ulikuwa mtenda mema unaweza kuzaliwa tena kama farasi ambaye ni mnyama mwenye thamani lakini kama ulikuwa mtenda mabaya unaweza kuzaliwa tena kama panya mnyama anaiyeshi kwa kuvia riziki.

 

Rais Maduro mwenye vibweka vinavyomtambulisha kwa kazi yake ya zamani ya udereva wa daladala kabla hajajitosa kwenye siasa, ameshindwa kuvaa viatu vya mtangulizi wake Hayati Hugo Chaves kutokana na staili yake ya kuongoza inayosababisha kuyumba kwa utangamano nchini humo, vurugu za mara kwa mara kutokana na mlipuko wa maandamano yanayompinga ambayo mara nyingi hukumbana na mapambano na polisi wa kuzuia ghasia lakini pia kukosekana kwa ithibati ya kiuchumi wa Taifa hilo licha ya mali ghafi muhimu ya mafuta inayomiliki. Kwa jinsi anavyoliongoza Taifa hilo unaweza kuhisi kwamba hana uzoefu wa uongozi lakini ukweli ni kwamba amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na kuwa Makamu wa Rais nyadhifa alizozishika pamoja kwa miaka saba.

 

Ni sahihi kabisa kutamka kwamba analisababishia uchuro wa anguko kubwa Taifa lake kutokana na kusababisha maisha ya wananchi wake kuwa magumu kwa mfumuko wa bei, ongezeko la uhalifu, ukosefu wa bidhaa muhimu kwa wananchi pamoja na umaskini na baa la njaa.

 

Venezuela imegubikwa migomo na maandamano yasiyokwisha yanayoibuka kila mara katika majaribio ya wapinzani kumng’oa madarakani Rais huyo king’ang’anizi anayetumia Mahakama Kuu, Tume ya Uchaguzi na taasisi nyingine za kiutawala kujikinga ili aendelee kubakia madarakani pengine si kwa  ustawi wa Taifa lake bali kwa manufaa yake binafsi kutokana na Taifa hilo kuyumba mno kuliko wakati wowote wa historia yake.

 

Katika mfululizo wa matendo yake yanayolichuria Taifa hilo hivi karibuni alianza mchakato wa kubadilisha Katiba ili asalie madarakani zaidi ya muda unaopaswa, hatua iliyosababisha wapinzani wake waitishe kura ya hiyari ya maoni kumpinga lakini pia wakaenda mbali zaidi kwa kuwaondoa majaji wote wa Mahakama Kuu kupitia Bunge wanalolidhibiti na kuwateua wengine kushika nafasi zao, lakini Serikali ya Maduro kwa kutumia mamlaka yake ya dola ikawatia nguvuni baadhi yao ili kuifanya mahakama hiyo isiweze kutekeleza kazi zake hivyo kufanikisha mkakati wa Maduro wa kubadili Katiba kwa kutumia mahakama hiyo.

 

Kabla hata ya mkakati wake huo haujafahamika wazi na kuongeza mafuta kwenye moto baada ya kubainika, wapinzani wamekuwa wakiandamana kupinga kila hatua ya Rais Maduro kujisimika zaidi madarakani kwa mfululizo wa maandamano yasiyoisha yenye ukubwa mbalimbali katika maeneo tofauti na kuudhofisha zaidi uchumi ambao tayari umeyumba, kwa kuwa kazi hazifanyiki kutokana na vurumai zisizoisha baina ya upinzani na Serikali na wananchi wanaotoshana nguvu kila mara na vyombo vya usalama. Bado hakuna kuaminiana katika Taifa hilo ambalo linajimithilisha na wachezaji wawili wa sataranji, kila mmoja akisogeza kete kukabili iliyosogezwa na mpinzani wake kutokana na kuzungukana wakati Rais Maduro amepania kuunda Bunge mahususi la Katiba ili libadilishe Katiba ya mwaka 1999.

 

Wapinzani waliamua kufanya Kura ya Maoni kupinga hatua hiyo inayoweza kutumiwa na Maduro na washirika wake kufuta uchaguzi na kusalia madarakani. Kama ni uhuisho wa maisha kama nilivyobainisha awali basi ni suala la muda tu kufahamu upande gani umehuishwa kuwa na thamani ipi kutokana na hila za kuzungukana zilizojaa uchuro, huku Taifa hilo likikabiliwa na kitisho cha vikwazo kutokana na Serikali isiyojiamini kutimiza hatua za kubinya demokrasia na kupigiwa kelele na mataifa jirani na jumuiya ya Kimataifa kurejea katika mstari wa utangamano, lakini sikio la kufa halisikii dawa kutokana na yanayoendelea nchini humo na kusababisha mkanganyiko ambao haufahamiki utaisha lini.

 

Utangamano umetoweka wakati Taifa hilo likigawanyika katika pande mbili zinazomuunga mkono na kumpinga Rais Maduro na hakuna uhakika wa usalama, kama ilivyotokea hivi karibuni  kutokana na kushambuliwa kwa ofisi za  Shirika la Utangazaji la Taifa na mapigano ya mara kwa mara ya pande mbili zinazopingana yakijumuisha polisi katikati yake, lakini pia mhimili unaoyumba  kutokana na Bunge kudhibitiwa na wapinzani lakini vyombo vya usalama vikidhibitiwa na Serikali inayodhamiria kujiongezea nguvu kwa kuishika Mahakama Kuu na kuunda Bunge la Katiba.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles