25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Marcon na ukweli wa ustaarabu wa Afrika

KATIKA  gazeti moja la kila wiki mwandishi Karen Attiah ameandika makala ndefu akimkosoa  Rais wa Ufaransa dhidi ya matamshi yake kuwa tatizo kubwa la Afrika ni kukosa ustaarabu ikiwa ni pamoja na wanawake kuzaa watoto wengi kuliko uwezo wao, wa jamii yao na taifa kuweza kuwatunza.

 

Attiah, Mwandishi na Mhariri wa Makala wa Washington Post anasema hilo lilikuwa kosa na dharau kwa Afrika. Mimi nataka kumuunga mkono Rais Marcon, ingawa najua ukweli kuwa ukoloni mkongwe na ukoloni mamboleo vimechangia kudunisha maendeleo yetu! Lakini tutaendelea kuwalaumu wakoloni hadi lini, mwaka huu ukiwa wa 60 au hata zaidi kwa mataifa mengine, kama Ghana, Siera Leone, Ethiopia , kupata uhuru.

 

Kumekuwa na tabia ya kutoa matamshi na maandiko endelevu yanayolenga kuitetea Afrika kuwa kutoendelea kwake kunatokana na kuendelea kuwa na uhusiano mbaya kati ya nchi za Marekani na Ulaya kwa upande mmoja na nchi za Afrika kwa upande mwingine. Ni Jambo la kweli, lakini Je, unapojua kuwa unalala kitanda kimoja na mwenza wa ndoa ambaye ni habithi na hasidi unaendelea kulalamika tu bila kufanya jambo ujiokoe?

 

Unabaki kulalamika tu? Afrika imeunda umoja wake mwaka 1963 huku viongozi wakiweka ahadi ya kuunda umajumui wa Afrika, pan-Africanism, wameishia wapi? Marehemu Ghadafi alikuwa akihimiza umuhimu wa kujenga  Taifa moja la Afrika, nani alimsikiliza miongoni mwa viongozi wa Waafrika. Unapokuwa na viongozi ambao hawataki kuachia madaraka iwe kwa kura au kwa vita, unataka kusema kuwa hilo ni kosa la Ufaransa na nchi zingine za Magharibi? Imefikia wakati, umekuwa mtindo kwa viongozi wa kizazi kipya Afrika kuamua kuivunja Katiba na kuamua kuondoa vigezo vya umri na ukomo wa madaraka na kusema kuwa hawataachia madaraka.

 

Na wengi wanasema; “Kwa sababu nilichukua madaraka kwa mtutu wa bunduki, sitoki, anayetaka madaraka naye aende msituni.” Kuna nchi ambako Rais anamweka kama Jaji Mkuu, mke wake. Kuna nchi ambako ukitangaza kugombea urais utafungwa; na katika Afrika wananchi kutoa maoni namna gani wanataka kusimamia maendeleo yao, wanakuwa wamefanya kosa. Naingalia nchi yangu Tanzania, kuzungumza siasa, kujadili matatizo ya kijamii, kuiambia Serikali kuwa kuna tatizo hapa au pale, kuchora picha ambayo inaakisi udhaifu katika Serikali au watendaji wake, ni kosa. Hakuna kukosoana. Sidhani kama Wazungu ndio walitufikisha hapa.

 

Attiah anaandika: “Rather than critizing Africans’ alleged failings, and sustaining a culture if colonial dependency, Marcon could help African nations build self sufficiency,”  Ni jambo la kuchekesha kusema hivyo. Angalia ni nani matajiri kuliko wote Afrika, ni familia za marais, wapambe wao na viongozi wanaowasaidia. Viongozi wanajitajirisha huku wakijua kuwa sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamaa haziko sawa na kuna wakati zinakosa Bajeti kabisa na hela zote zinaenda kwenye mifuko binafsi ya viongozi.

 

Donald Trump alisema kwa uzuri kabisa kuwa watu wanaiba fedha huko Afrika na wakati mwingine fedha za misaada na kwenda  kuzificha Marekani au Ulaya. Je, hawa watu hawajui kuwa nchi zao zinahitaji kujitegemea? Viongozi wanaamua kuanzisha miradi ambayo haina faida kabisa ya moja kwa moja kwa wananchi. Naingalia Tanzania yangu kuwa kwa mwaka mmoja uliopita na kama si miaka mingi sasa uwekezaji katika kilimo umepungua na huduma zinazohusiana na kilimo kama vile ugani, uhimizaji wa kuongeza thamani, masoko, nguvu kazi ya kilimo na mengi mengine hakuna kabisa kama si kupungua.

 

Serikali zetu Afrika zinaamua kujenga viwanja vya ndege, majengo ya kisasa kabisa ya ofisi, madaraja ya juu huku wakijua kabisa mikoa ya jirani na hapo makao makuu watu wake hawana uhakika wa dawa wala madaftari na madawati  na wafanyakazi kipato chao hakiwezi kuwafikisha mwisho wa mwezi, achilia ukweli kwamba uzalishaji kwa ujumla umepungua sana katika kila sekta. Lakini kwa viongozi wanapata mishahara yao na wafanyakazi wanapata, hao wengine watajijua. Afrika haihitaji msaada kutoka nje kujiendeleza kama Mwandishi wa Ivory Coast alivyotaka Marcon ajieleze, bali inahitaji viongozi wanaojitambua n kutambua kuwa wako pale juu kwa ajili ya wananchi na Taifa lao.

CONTACTS: 0766959349

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles