RAIS MAGUFULI TILIA MKAZO UCHANGIAJI DAMU 

0
2

  

Na CLARA MATIMO -MWANZA

TATIZO la uhaba wa damu katika hospitali mbalimbali hapa nchini limekuwa likiripotiwa kila mara na madaktari pamoja na maofisa uhamasishaji damu salama wa kanda.

Hii yote ni kutokana na kuwepo kwa baadhi ya vifo vitokanavyo na wagonjwa kukosa damu salama ambayo ingewasaidia kuokoa maisha yao.

Kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama  nchini, bado kuna upungufu mkubwa wa damu kutokana na uchangiaji mdogo kutoka kwa wananchi ambao huchangia chupa 150,000 pekee kwa mwaka, huku mahitaji yakiwa ni chupa 450,000.

Wakati kukiwa na upungufu wa chupa 300,000 za damu nchini, mkoani Mwanza Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk. Leonard Subi, anasema mahitaji ni chupa 30,000 kwa mwaka wakati kwa siku zinahitajika chupa 80, lakini mkoa umekuwa ukikusanya chupa 45 kwa siku, hivyo kuwa katika uhitaji au uhaba wa chupa 35 kila siku.

Kama tujuavyo duniani kote hakuna kiwanda chochote ambacho kinatengeneza damu bali inatoka kwa binadamu, hivyo wenye wajibu wa kuhakikisha inapatikana na tunakuwa na akiba ya kutosha ni sisi wenyewe.

Nakuomba Rais wangu Dk. John  Magufuli uliye kipenzi cha Watanzania, mchapakazi na ambaye hupendi kuona wananchi wako wakipata shida ambazo una uwezo wa kuzitatua, ulivalie njuga suala la upatikanaji wa damu.

Namaanisha rais na Serikali yake anayoiongoza wakiwemo mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya wote kwa nafasi zao kila wanapoongea na wananchi wawahamasishe kujitolea kuchangia damu kwa hiari.

Suala la kuchangia damu kwa hiari liende sawa na upigaji vita dawa za kulevya, mauaji ya Kibiti, mimba kwa wanafunzi na mengineyo ambayo yanapewa kipaumbele na Serikali.

Wananchi wanamuunga mkono Rais Magufuli, naamini itakuwa  vyema akiwahamasisha ili wajenge utaratibu wa kuchangia damu kwa hiari mara kwa mara.

Hata aliposema ukinunua kitu chochote dai risiti  na ukiuza toa  risiti, mtoto wangu mwenye umri wa miaka mitano akienda dukani kununua ‘chipsy  snack’ anadai risiti anamwambia muuzaji Rais Magufuli amesema nidai risiti.

Hii inaonyesha kauli ya rais  kuhusu jambo fulani inaporejewa kila mara kupitia vyombo vya  habari, inaingia na kuishi masikioni mwa watu wanaoisikiliza bila kujali umri walionao.

Nasema hivyo kwa sababu kuna mambo au jambo ambalo likisemwa na kiongozi au mtu maarufu duniani ama nchini,  jamii hulipa uzito wa hali ya juu lakini jambo hilo hilo na pengine zuri zaidi likisemwa na mwananchi wa kawaida halipewi uzito wowote.

Hapo ndipo unapotimia usemi usemao haijalishi wewe umesema nini bali nani kasema nini, hivyo naamini endapo Rais Magufuli akitoa kauli ya kuwahamasisha wananchi kuchangia damu kwa hiari hakika wengi watajitokeza na hatutakuwa na uhaba wa damu salama katika hospitali zetu.

Hata watoto wakiwa wakubwa watakuwa na moyo wa kuchangia damu sababu walishawekewa msingi mzuri tangu wakiwa wadogo, wakitambua kwamba kuchangia damu ni njia mojawapo ya kutoa sadaka maana wanaokoa maisha ya watu wengine.

Hata Mratibu wa Huduma za Maabara Mkoa wa Mwanza, Juma Shigella, alikwishasema kati ya asilimia 100 ya damu ambayo huchangwa na wachangia damu kwa hiari katika Mkoa huo, wanafunzi wa sekondari na vyuo wamekuwa mstari wa mbele ambapo huchangia asilimia 85 na mafanikio hayo yamepatikana kutokana na kuelewa umuhimu wa kuchangia damu na kisha kuhamasishana wao kwa wao.

Hii inadhihirisha kwamba kabla hawajafikisha umri wa miaka 18, walikuwa wakisikia sauti za viongozi mbalimbali ama watoa huduma za afya wakiihamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari.

Pia tukiwa na damu ya kutosha tutafanikiwa kuokoa maisha ya watu ambao wangeweza kupoteza maisha  kutokana na kukosa  damu  tutafikia adhima ya kuwa na uchumi wa kati unaohamasisha viwanda maana nguvu kazi inayopotea itaendelea kufanya kazi na kuinua uchumi wa Taifa.

Nakuomba Rais wangu Magufuli kila mara unapomaliza kuongea na wananchi, wanasiasa, wafanyabiashara, wanafunzi wa kada mbalimbali, watumishi wa umma na binafsi wasisitize bila kuchoka wajitolee kuchangia damu kwa hiari ili tumalize tatizo la uhaba wa damu nchini kwetu.

Hakika kupitia wewe hakuna kinachoshindikana katika nchi yetu hasa ninapoiona dhamira yako ya dhati uliyonayo ya kuboresha sekta ya afya, ukiwa na lengo la kuhakikisha wananchi wanapata matibabu bora ili kuepuka vifo vinavyoweza kuzuilika badala ya kusubiri siku ya maadhimishio ya wachangia damu kwa hiari duniani ndipo tuhamasishe wananchi kuchangia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here