24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

RAIS MAGUFULI AMWAGA AJIRA

AJIRA: Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, akizungumza
kuhusu ajira mpya kwa madaktari 258 waliokuwa waende nchini Kenya, mjini Dodoma jana. Kulia ni
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Mpoki Ulisubisya.

 

 

Na ELIZABETH HOMBO-DODOMA

RAIS Dk. John Magufuli, ameagiza madaktari 258 ambao walikuwa tayari kwenda kufanya kazi nchini Kenya, waajiriwe mara moja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Agizo hilo linatokana na Mahakama ya Kenya kutoondoa pingamizi lililofunguliwa kuhusu ajira za madaktari wa Tanzania kwenda kufanya kazi nchini humo.

Mwezi uliopita, madaktari watano nchini Kenya waliwasilisha pingamizi mahakamani kuitaka Serikali ya nchi yao kusitisha kuajiri madaktari kutoka Tanzania.

Akizungumnza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema madaktari hao ndio waliokidhi vigezo vilivyotakiwa kwenda kufanya kazi nchini Kenya kati ya maombi 496 yaliyowasilishwa.

“Mheshimiwa Rais ameagiza jambo hili lifanyike, lakini sisi hatujui fedha hizo amepata wapi. Sisi tunamshukuru na kumpongeza tu,” alisema Ummy.

Alisema Machi 18, mwaka huu, ujumbe wa Serikali ya Kenya ukiongozwa na Waziri wa Afya, Dk. Cleopa Mailu, ulikutana na Rais Magufuli kwa madhumuni ya kuomba kuajiri kwa mkataba madaktari wa Tanzania 500 ili kupunguza uhaba wa madaktari nchini humo.

“Rais Magufuli alikubali ombi hilo na Machi 18, mwaka huu, wizara yetu ilitangaza nafasi hizo za ajira kwa madaktari wa Tanzania kwenda kufanya kazi nchini Kenya ambapo hadi Machi 21, mwaka huu, jumla ya maombi takribani 496 yaliwasilishwa,” alisema Ummy.

Alivitaja baadhi ya vigezo walivyokidhi madaktari 258 kuwa ni uhakiki wa vyeti vya taaluma na vyeti vya sekondari, chuo walichosoma na mwaka wa kuhitimu masomo, sehemu walikofanya mafunzo ya vitendo na mwaka wa kuhitimu mafunzo hayo.

Vigezo vingine,ni  uzoefu wa kazi, umri wa mwombaji usiozidi miaka 55, usajili wa mwombaji katika Baraza la Madaktari la Tanganyika na asiwe mtumishi wa umma, hospitali teule za halmashauri na hospitali za mashirika ya hiari wanaolipwa mishahara na Serikali.

Alisema ratiba ya utekelezaji wa ajira hizo za madaktari ilikubalika na pande zote mbili kuwa iwe imekamilika ifikapo Aprili 6, mwaka huu na kuwa madaktari hao wawe tayari kusafiri kwenda nchini Kenya kati ya Aprili 6 na 10, mwaka huu.

“Kwa kuwa hadi tarehe hii mahakama nchini Kenya haijaondoa pingamizi lililofunguliwa kuhusu ajira za madaktari wa Tanzania nchini Kenya, hivyo Rais ameamua waajiriwe na Serikali ya Tanzania mara moja,” alisema Ummy.

Alisema kutokana na uamuzi huo, majina ya madaktari husika na vituo watakavyopangiwa kazi yatatangazwa katika tovuti ya wizara pamoja na wataalamu wengine wa afya 11 waliopeleka maombi yao na kukidhi vigezo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles