33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Karume amfuata shemeji yake mahabusu

Na Is-haka Omar, Zanzibar

RAIS mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, jana alifika katika Kituo Kikuu cha Polisi Mwembe Madema mjini Zanzibar, kumtembelea shemeji yake, Mansour Yussuf Himid aliyekamatwa juzi kwa tuhuma za kukutwa na silaha za moto kinyume cha sheria.

Baada ya Karume kufika kituoni hapo akiwa na msafara wake, aliruhusiwa kuonana na shemeji yake huyo baada ya kutolewa mahabusu alikokuwa akishikiliwa.

Karume na Himid, waliteta kwa dakika zisizozidi kumi kisha rais huyo mstaafu akaondoka.

Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Sulum Msangi, alithibitisha Rais Karume kumtembelea shemeji yake ambaye anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi Zanzibar.

“Ni kweli Rais Karume akiwa na mkewe Shadia, walifika kituoni Mwembe Madema leo saa mbili asubuhi kumuona mtuhumiwa.

“Kilichowapeleka pale ilikuwa ni kumsalimia tu na hawakuwa na nia ya kumwekea dhamana au shida nyingine,” alisema Msangi.

Mbali na Dk. Karume, viongozi wengine wa kisiasa akiwemo Naibu Waziri wa Maji, Makazi, Ardhi na Ujenzi, Haji Mwadini Makame pamoja na Wawakilishi wenzake kutoka Chama cha Wananchi (CUF) ambao ni Hija Hassan Hija (Kiwani), Saleh Nassor Juma (Wawi) na Hassan Omar Hamad (Kojani) walifika kituoni hapo kumjulia hali Himid.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Zanzibar, linatarajia kumpandisha kizimbani Himid kwa tuhuma za kumiliki silaha hizo.

Taarifa hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Msangi mwenyewe alipokuwa akizungumza na MTANZANIA Jumatatu kwa simu.

“Huyo mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika kwa sababu hadi sasa tunaendelea na upelelezi pamoja na kupitia sheria mbalimbali za masuala ya umiliki wa silaha.

“Pindi upelelezi utakapokamilika, mtuhumiwa huyo atapelekwa mahakamani.

“Kuhusu suala la kupewa dhamana, itategemea na vielelezo vitakavyopatikana baada ya kuhojiwa kwa kuangalia zaidi mazingira ya ushahidi. Kama mazingira yataruhusu, anaweza kupewa dhamana huku kesi yake ikiendelea kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Katika sakata hili, Mansour alikamatwa nyumbani kwake huko Chukwani na kufanyiwa upekuzi mkali na askari wa kikosi cha upelelezi wakiongozwa na Msangi.

Akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya Jeshi hilo juzi, Msangi alisema Jeshi la Polisi lilipata taarifa za kiintelijensia kuwa Himid anamiliki silaha kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa Msangi, baada ya kupokea taarifa hiyo, jeshi hilo lilianza kuifanyia kazi na juzi ilikuwa siku rasmi ya kwenda kufanya upekuzi ndani ya nyumba yake na kufanikiwa kupata bunduki aina ya shotgun yenye namba za usajili 1904136413 aina ya Bore Browning pamoja na risasi 112.

Alisema kwamba, ni kosa kisheria mtu kumiliki zaidi ya risasi 55 kwa silaha aina ya shotgun na ni sababu hiyo ndiyo iliyolielekeza jeshi hilo kuendelea kumhoji.

Msangi aliitaja silaha nyingine aliyokamatwa nayo kuwa ni bastola yenye namba F76172W pamoja na risasi 295, jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya umiliki wa silaha za moto, ambapo mmiliki anatakiwa kuwa na risasi zisizozidi 25.

“Mbali na silaha hizo, vitu vingine vilivyokamatwa na jeshi hilo ni kompyuta mpakato (laptop) pamoja na vifaa vinavyodaiwa kuwa ni vya mawasiliano ambavyo vinaendelea kufanyiwa uchunguzi.

Pamoja na hayo alisema Himid amekamatwa wakati huu ambao jeshi hilo liko kwenye operesheni ya kawaida tangu kuanzishwa kwa Jeshi la Polisi nchini.

Upekuzi huo ulioanza saa saba mchana unadaiwa kufanyika chini ya ulinzi mkali wa polisi wapatao 30 na kisha Himid akafikishwa Makao Makuu ya Polisi kabla ya kuhamishiwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Madema kwa ajili ya kufanyiwa mahojiano.

Mansour ni mtoto wa Mwanamapinduzi Brigedia Yusuph Himid, ambaye alikuwa ni muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Aliingia kwenye siasa wakati Rais Amani Abeid Karume akiwa Rais wa Zanzibar na alifukuzwa CCM baada ya kile ambacho wengi wanahisi kuwa ni msimamo wake wa kuunga mkono muundo wa Serikali ya mkataba unaoungwa mkono na Chama cha Wananchi (CUF).

Mansour amewahi kuwa waziri katika wizara mbalimbali kuanzia mwaka 2000 alipoteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi na mwaka 2005 alikuwa waziri kamili.

Baada ya Rais Karume kuondoka madarakani mwaka 2010, aliteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo chini ya Serikali ya Dk. Ali Mohamed Shein na baadaye kuwa Waziri asiyekuwa na Wizara maalumu, baada ya afya yake kuzorota na kubadilishiwa nafasi.

Shemeji yake ambaye ni Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, alifanya naye kazi kwa karibu na kumpa wizara nyeti ya Ardhi na Nishati katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wake kabla ya kustaafu.

Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Karume
Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Karume
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles