RAIS KAGAME AWASAMEHE INGABIRE, KIZITO MIHIGO

0
489

KIGALI, RWANDARais Paul Kagame wa Rwanda, akitumia mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo, ametangaza kutoa msamaha na kuwaachilia huru zaidi ya wafungwa 2,000 waliokuwa wamefungwa kwa makosa mbalimbali.

Taarifa ya kuachiliwa wafungwa hao imetolewa na serikali kufuatia mkutano wa baraza la mawaziri, na kusema kuwa Rais aliwaonea huruma, hivyo kwa mamlaka yake aliamuru waachiliwe.

Miongoni mwa wafungwa hao waliofaidika na msamaha wa rais huyo ni mwanamuziki Kizito Mihigo, ambaye alikuwa akitumikia kifungo cha miaka 10 na mwanasiasa Victoire Ingabire, ambaye alikuwa kizuizini tangu 2010.

Victoire Ingabire alikuwa akitumikia kifungo cha miaka 15 kutokana na makosa ya kutishia usalama wa serikali na kudunisha mauaji ya halaiki ya mwaka 1994.

Amekuwa akiongoza ukosoaji wa Rais Paul Kagame, huku akiongezea kuwa hukumu yake ilishinikizwa kisiasa.

Rais Kagame amepongezwa kwa kurekebisha uchumi wa Rwanda, lakini pia ameshutumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu.

Mbali na Ingabire, ni mwanamuziki Kizito Mihigo ambaye mwaka 2015 alihukumiwa kifungo cha miaka 10, kwa kupanga njama za kumuua Rais Paul Kagame.

Akizungumza na shirika la habari la AFP mara baada ya kutolewa gerezani, Ingabire alimshukuru Rais Kagame, akisema huu ndio mwanzo wa kufunguka kwa sehemu ya kisiasa nchini Rwanda.

Kwa upande wake waziri wa haki, Johnston Businge, aliliambia Shirika la Habari la Reuters, kuwa hakuona jambo lolote la kisiasa katika suala la mfungwa Ingabire.

“Hakuna chochote cha kisiasa kuhusu kuachiliwa kwake, na hakuna chochote cha kisiasa kuhusu kufungwa kwake,” aliimbia Reuters.

Ingabire alirudi kutoka jela nchini Uholanzi 2010 ili kushiriki katika uchaguzi wa urais. Alikamatwa na kuzuiliwa kuwania urais na amekuwa akitumikia kifungo jela tangu wakati huo.

Ingabire, ambaye ni mwanachama wa kabila la Hutu, alikuwa akihoji ni kwa nini makumbusho ya mauaji ya halaiki nchini Rwanda ya 1994 hayakuhusisha watu wa kabila la Hutu.

Wengi wa watu 800,000 waliouawa walikuwa watu wa Kabila la Tutsi, lakini Wahutu wenye msimamo wa kati pia waliuawa na Wahutu wenye msimamo mkali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here