27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Bush wa Marekani afariki dunia

NEW YORK, MAREKANI


RAIS wa zamani wa Marekani, George Herbert Walker Bush, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 94, ambaye mwezi Aprili mwaka huu, alilazwa hospitalini akiwa na maambukizi kwenye damu lakini akatibiwa na kuruhusiwa kuondoka hospitalini.

Kwa mujibu wa gazeti la New York Times, limesema kuwa taarifa ya kuthibitisha kifo cha rais huyo wa zamani imetolewa na mtoto wake wa kiume, George W. Bush, ambaye naye aliwahi kuwa rais kati ya mwaka 2001 hadi 2009.

Mtoto huyo amethibitisha taarifa za kifo cha baba yake na kusema alikuwa mtu wa haiba ya hali ya juu katika kipindi cho utumishi wake ndani ya taifa hilo kubwa duniani.

Kifo cha Bush kinafuatia kifo cha mke wake Barbara, aliyefariki miezi saba tu iliyopita, yaani Aprili mwaka huu.

Viongozi wamekuwa wakituma salamu za rambirambi na kumkumbuka mwanasiasa huyo, wakiongozwa na Rais wa sasa wa Marekani Donald Trump, aliyemsifu kwa uhalisia wake, ucheshi na kujitolea kwake kudumisha imani, kwa familia na kwa taifa.

Aidha, taarifa zinasema bendera katika Ikulu ya White House zitapepea nusu mlingoti huku mipango ya mazishi ikiendelea.

Trump ambaye yupo kuhudhuria mkutano wa viongozi wa G20 nchini Argentina, katika salamu hizo za pole amesema Bush Senior kuwa mtu aliyejitoa kwa familia yake na nchi yao.

Salamu za pole pia zimetoka kwa Rais wa zamani, Barack Obama, aliyesema Marekani imepoteza kiongozi mzalendo.

George Herbert Walker Bush kutoka Republican, alikuwa rais wa 41 wa Marekani kati ya mwaka 1989-1993, wakati ambao aliiongoza nchi yake katikati mwa matukio muhimu ikiwemo kuanguka kwa ukuta wa Berlin na kuporomoka kwa Muungano wa kisovieti.

Je alikuwa mtu wa aina gani?

Kuapishwa kwa George H W Bush kuwa Rais wa Marekani mnamo Januari 1989 kilikuwa kilele cha ufanisi wake katika siasa. Alikuwa ameandaliwa kwa muda mrefu kupitia mafunzo ya kiwango cha juu, na kupandishwa madaraka mara kwa mara kabla ya kuishia Ikulu ya White House.

Rais huyu wa 41 wa Marekani alifanya kazi kama makamu wa Rais wa Ronald Reagan kwa miaka minane.

Alikuwa Makamu wa Rais wa kwanza aliyekuwa ofisini kufanikiwa kuchaguliwa kuwa Rais katika kipindi cha zaidi ya miaka 150.

Utawala wake unahusishwa sana na siasa za wakati ule ambapo Ukomunisti ulikuwa ukiporomoka Ulaya Mashariki na kusambaratika kwa Muungano wa Usovieti (USSR) ambapo Marekani iliachwa ikiwa taifa kubwa zaidi kiuchumi na kiviwanda duniani.

Uongozi wake ulisaidia kurejesha hadhi ya Marekani kwa dunia nzima na kurejesha heshima yake kufuatia uvamizi wa Marekani nchini Vietnam, ulioiletea Marekani aibu.

Hata hivyo alilaumiwa kwa kupuuza masuala ya ndani ya Marekani na kwa kupuuzilia mbali ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni ambapo aliahidi kuwa hataongeza kodi.

Kupuuzilia mbali kwa ahadi hiyo kulimfanya ashindwe katika uchaguzi uliofuata na Bill Clinton wa chama cha Democratic mwaka 1992.

George Herbert Walker Bush alizaliwa Julai 12, 1924 katika Milton, Massachusetts. Baba yake alikuwa mwekezaji katika benki na baadaye akawa Seneta wa Marekani.

Alijitolea kupigana katika jeshi la wanamaji Vita Vikuu vya Pili vya Dunia baada ya kushambuliwa kwa Pearl Harbor.

Alipata mafunzo ya kuendesha ndege za kivita kabla ya kupewa majukumu katika vita katika Bahari ya Pacific ambapo alishiriki katika vita dhidi ya Wajapani katika Vita Vikuu ya Pili ya Dunia.

Akiwa na umri wa miaka 18 pekee, ambapo inawezekana alikuwa miongoni mwa marubani wachanga sana Wamarekani, alipewa kazi ya urubani wa ndege za kijeshi za kuangusha mabomu zinazoruka angani kutoka kwa meli kubwa za kivita.

Ndege yake ilitunguliwa Septemba 1944 alipokuwa akielekea kuangusha mabomu. Ndege yake ilijaa moshi na ndimi za moto zilianza kuteketeza mbawa zote mbili.

Aliendelea kuendesha ndege hiyo na kuangushia mabomu kwa shabaha zake kadhaa. Aliwaamuru wanahewa wawili aliokuwa nao wajisalimishe kwa kuruka kwa miavuli kutoka kwenye ndege hiyo lakini wote wawili hawakunusurika.

Bush alisongwa na moshi lakini akavalia mwavuli pia na kuruka kama wenzake. Alianguka kwenye kisiwa kimoja baada ya kugongwa kichwa chake na sehemu ya nyuma ya ndege kwa sababu ya upepo akiruka.

Alifanikiwa kufikia boya na akaanza kulielekeza kama ngalawa akitumia mikono yake kama makasia kutoroka visiwa vilivyokuwa mikononi mwa Wajapani.

Alikuwa na bahati ajabu, kwani kabla hajakwenda mbali nyambizi iliibuka alikokuwa na kumwokoa. Nyambizi hiyo iliendesha shughuli zake kwa utaratibu sana hivi kwamba walirekodi kwa filamu.

Baada ya kuondoka kwenye kikosi cha wanamaji mwaka 1945 kwa heshima, Bush alimwoa msichana mwenye umri wa miaka 18, Barbara Pearce.

Ndoa yao ilidumu miaka 72 na wakafanikiwa kuwapata watoto sita. Mtoto wao wa kwanza, ambaye baadaye alikuwa Rais George Walker Bush, alizaliwa mwaka mmoja baadaye.

Awali Bush alikuwa amepewa nafasi kuendelea na elimu katika Chuo Kikuu cha Yale kabla ya kusajiliwa katika kikosi cha wanamaji. Mara tu alipotoka jeshini mwaka 1945 baada ya vita kumalizika, alirudi katika chuo kikuu na kukamilisha shahada yake katika sanaa.

Bush na familia yake kisha walihamia Texas ambako alitumia uhusiano mzuri wa kibiashara wa baba yake kupata kazi katika sekta ya mafuta.

Kabla ya kufikisha miaka 40, tayari alikuwa milionea. Bush na mkewe, Barbara walisononeka sana baada ya binti yao wa pekee kugunduliwa kuwa na maradhi ya kansa ya kukosekana kwa damu mwilini, kwa Kiingereza Leukemia. Robin alipelekwa hospitalini kutokana na uchovu mwilini, lakini Bush na mkewe walishtushwa na maelezo ya daktari.

Familia hiyo ilishtushwa na kifo cha Robin miezi michache baadaye. Pigo la tukio hilo lilijitokeza baada ya kifo cha Barbara Bush alipofariki miaka 65 baadaye, familia hiyo iliweka bango lenye maandishi yaliyosema “Tafadhali mama, mkumbatie Robin kwa niaba yetu.”

Uhafidhina

Mawazo ya kikazi ya George Bush yalibadilika na kuingilia siasa. Baada ya kutumikia kwa muda kama mwenyekiti wa tawi la chama cha Republican eneo la Texas, alifanya uamuzi mgumu. Alishindana kutaka kuteuliwa kama mgombea wa Useneta wa chama chake cha Republican katika jimbo la Texas.

Seneta wa eneo hilo wa chama cha Democratic aliwaambia watu kuwa Bush alikuwa mwanasiasa wa msimamo mkali wa mrengo wa kulia.

Mwanachama huyo wa Democratic alipata asilimia 56 ya kura zilizopigwa zikilinganisha na asilimia 43 za Bush. Bila kukata tamaa Bush aligombea kiti cha bunge la wawakilishi na akashinda kiti mwaka 1966. Alihudumu mihula mbili.

Rais Richard Nixon alimshawishi Bush kugombea Useneta tena mwaka 1970 lakini tena akashindwa na mgombea yule yule wa Democratic.

Rais Nixon alimteua Bush kuwa balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa 1971 na kisha akawa mwenyekiti wa chama cha Republican.

Wakati Nixon alipolazimishwa kujizulu 1974, Bush alifanya kila juhudi kuponya baadhi ya makovu yaliyosababishwa na kashfa ya Watergate, ambapo alitumia muda wake mwingi kuwatetea wagombezi wa Republican kwa kufanya ziara maeneo mbalimbali nchini humo.

Mwisho wa mwaka alienda Uchina kuwa balozi katika ubalozi mpya wa Marekani nchini humo.

Baada ya kuwa nchini Uchina kwa mwaka mmoja pekee, Rais Gerald Ford alimrejesha nyumbani Bush na kumteua kuwa mkurugenzi wa shirika la upelelezi la CIA, shirika ambalo lilikuwa limekabiliwa na msururu wa kashfa kuhusiana na operesheni za usiri mkubwa nje ya nchi pamoja na kuwapeleleza raia wa Marekani bila idhini.

Kutumwa kwake CIA kulitokea wakati ambapo mkewe Barbara alikuwa amezidiwa na ugonjwa wa kiakili.

Mke wake aliandika kwenye kitabu kuhusu maisha yake kwamba angelielekeza gari lake pembeni mwa barabara akiogopa kugonga mti au magari yaliyokuwa yakienda upande ule mwingine. Hisia hizo baadaye zilitokomea.

Bush aliondoka CIA baada ya Ford kuondoka madarakani na mwaka 1978 akaanza kufanya kampeni ya kutaka kuteuliwa kuwa mgombea wa urais wa chama chake katika uchaguzi wa mwaka 1980.

Alizuru kote nchini akieleza juu ya msimamo wake wa uhafidhina wa kadri. Kufikia 1980 ilionekana wazi kuwa ni yeye pekee aliyebakia ambaye angetoa ushindani mkali dhidi ya Ronald Reagan.

Mara tu alipojiingiza katika kinyang’anyiro cha kisiasa, Bush aligundua kuwa kulelewa kwake katika maisha ya hadhi awali kungekuwa kama gharama kwake kisiasa.

“Kuna kosa gani katika kufaulu maishani,” Bush aliuliza wakati ule. Aliongezea: “Kuna kosa gani kuwa na elimu nzuri? Kuna kosa gani ikiwa nilifaulu maishani na katika biashara zangu au kuwa balozi mzuri nchini China au katika Umoja wa Mataifa au kufanya kazi nzuri katika CIA. Haya yote nimefanya mimi. Najua wengine watasema ni kujigamba, lakini hiyo ndiyo rekodi yangu.”

Aliposhindwa na Reagan alikuwa na bahati nyingine ya kumliwaza. Aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Reagan ambapo alihudumu kama makamu wa Rais kwa miaka minane, ambapo ilikuwa ni kama kipindi cha mafunzo ya kujiandaa kuwa Rais.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles