33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

RAILA AFICHUA SABABU YA KUTOSWA KINA RUTO, KALONZO

NAIROBI, KENYA


KIONGOZI wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga juzi alifichua namna yeye na Rais Uhuru Kenyatta walivyowatosa watu wao wa karibu na kupuuza shinikizo la wafuasi wao ili kuiepusha nchi kuingia katika machafuko makubwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Odinga alisema hayo baada ya kuzindua Hoteli ya Kitui Villa, inayomilikiwa na mmoja wa washauri wake wakuu, mwanasheria aishiye Marekani, Profesa Makau Mutua.

Miongoni mwa watu mashuhuri waliohudhuria tukio hilo mbali ya Odinga na Profesa Mutua ni aliyekuwa mgombea mwenza wa urais wa Odinga, Kalonzo Musyoka, Gavana wa Kitui, Charity Ngilu na mke wa Odinga, Ida.

Odinga alisema wafuasi wake walidhamiria kususa kulipa kodi serikalini na kuondoa picha za Rais Kenyatta kutoka ofisini na maeneo ya biashara katika ngome zake kupinga uchaguzi mkuu uliochakachuliwa.

Kwa upande wake, Rais Kenyatta alikuwa katika shinikizo kubwa la wafuasi wa chama chake cha Jubilee amkamate na kumshitaki Odinga kwa uhaini kufuatia tukio la kujiapisha kuwa rais wa watu Januari 30 kwenye Bustani ya Uhuru.

Kwa mujibu wa Odinga, wasiwasi wa nchi kuingia katika machafuko ya kikabila yalisababisha yeye na Rais Kenyatta kufikia mwafaka wa kuyazuia, kwa gharama ya ghadhabu ya kambi zao.

Ni mwenendo huo ulioshuhudia mazungumzo na hatimaye kukutana kwa tukio maarufu la kushikana mikono lililoziacha kambi zao kinywa wazi.

“Baada ya kuapishwa kwangu, niligundua kuwa Uhuru alikuwa katika shinikizo kutoka kwa wafuasi wake wa Jubilee kunikamata na kuniburuza mahakamani kwa mashitaka ya uhaini lakini alipuuza kwa sababu alifahamu fika hilo lingeiingiza nchi katika maandamano na machafuko yasiyo na mwisho,” alisema Odinga katika hotuba iliyoeleza hatua kwa hatua kilichojiri nyuma ya pazia na kumlazimisha yeye na Kenyatta kujadiliana bila masharti yoyote makubwa lakini bila kuwashirikisha washirika wao.

Odinga alisema Rais Kenyatta awali alikubali kumkamata kabla ya kuachana na mpango huo baada ya kutafakari athari za kuchukua uamuzi kama huo.

“Wafuasi wangu walipanga kukusanya picha zote za rais na kuzichoma moto. Pia tulikuwa tayari kuanza kukusanya kodi katika ngome zetu. Nililitafakari hili na kubaini kuwa kwa urahisi kabisa lingeipeleka nchi ziliko Syria au Yemen,” alisema na kuongeza kwamba wafuasi wake wasiosikia kitu walitaka kuchoma moto picha za Kenyatta katika tukio la wazi kudharau mamlaka yake kama Rais kupinga uchaguzi uliojaa udanganyifu.

“Ningeruhusu maandamano ya kitaifa, serikali ya Jubilee ingeitikia kwa nguvu kubwa kupambana na wafuasi wa NASA na hilo lingeiweka nchi katika mwelekeo wa hatari” alisema.

Odinga alisema wakati Rais Kenyatta alipowasiliana naye kwa majadiliano, alitoa sharti la kutohusisha mwanasiasa yeyote kutoka chama cha Jubilee anayeelekeza macho yake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

“Tulikuwa na mazungumzo ya awali ya kujadili namna ya kuendesha yale ya mwisho. Nilitoa masharti yangu naye akakubali tukutane wawili tu. Naye pia alisisitiza kuwa vinara wenzangu wa Nasa pia wasihusishwe bali tuwaache gizani,” alisema Odinga, akiongeza kuwa ni sababu ya kutomjulisha kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka.

“Rais Kenyatta alinitaka nisimhusishe kaka yangu Musyoka katika mazungumzo nami nikamwambia naibu wake William Ruto asiwepo, kitu alichokubali. Nilisisitiza kwamba sihitaji watu ambao watatutaka tujadili 2022.

“ Yeye (Uhuru) alisema hatakuja na Ruto lakini pia alitaka nami nisije na Kalonzo,” alisema Odinga katika tukio hilo.

Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Odinga kujadili matukio yaliyopelekea tukio la kushikana mikono na Rais Kenyatta Machi 9 pamoja na sababu za kutohusisha vinara wenzake; Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula.

Kutohusishwa kwa vigogo hao watatu wa upinzani nusura kuusambaratishe muungano huo wa NASA na wakamtuhumu Odinga kwa usaliti.

Aidha tukio hilo pia limekitikisa Chama tawala cha Jubilee, ambapo kambi ya Ruto inatuhumu limelenga kukwamisha ndoto zake za kuwania urais 2022.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles