28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

RAHCO WAJIPANGA KUBORESHA USAFIRI WA TRENI DAR 

Na LEONARD MANG’OHA


KINACHOLIFANYA Jiji la Dar es Salaam kuwa kuu kiuchumi nchini ni kutokana na historia yake  iliyotukuka tangu wakati wa ukoloni, katika harakati za kutafuta ukombozi na kutegemewa zaidi katika upatikanaji wa huduma zote muhimu za kiserikali.

Pamoja na ukongwe wake, wananchi wengi wa mji huu kwa kipindi kisichopungua miaka 20, wamekuwa wakionja kile unachoweza kukiita ‘joto la jiwe’ kutokana na misongamano ya magari katika barabara zake zote kuu na na zile za michepuko.

Hali hii imechagizwa zaidi na ongezeko kubwa la watu na matumizi ya idadi ya vyombo vya moto visivyoendana na urahisi wa miundombinu ya barabara kutokana na maeneo mengi kujengwa bila kufuata utaratibu wa mipango miji kiasi cha kukosa barabara za mitaa ambazo zingesaidia kupunguza misongamano kwenye njia kuu.

Hali hii ilisababisha kupoteza muda mwingi barabarani ambao kwa kawaida ungetumika kufanya kazi za uzalishaji ili kuharakisha maendeleo kutokana na watu kutumia muda mwingi kwenda na kutoka kazini. Muda wa kazi ukashuka hadi kufikia saa sita badala ya saa nne kwa siku.

Japo kwa kuchelewa, Serikali ikaja na mpango wa usafiri wa treni maarufu treni ya Mwakyembe aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi wakati huo kutoka katikati ya jiji kwenda Pugu, walau ikasaidia kupunguza adha ya usafiri kwa wakazi wa Pugu na Gongo la Mboto, lakini haikufanikiwa kulimaliza maana jiji limeshehemi raia wengi.

Nasema haijafanikiwa kulimaliza kwa sababu kila treni hiyo inapotoka Pugu kuingia mjini inakuwa na shehena kubwa ya watu kiasi cha wengine kuning’inia sehemu za nje za treni tena bila kujali hatari ya kupoteza maisha, lakini watafanyaje na wanataka wawahi majukumu tena wakati huu wa Dk. Magufuli anaotaka watu wapige kazi.

Hivi karibuni gazeti moja lilichapisha picha kwenye ukurasa wake wa mbele ikionesha abiria wakiwa wamening’inia nje ya treni ikiwa kwenye mwendo. Hii ni hatari kweli watu hawana hofu kabisa.

Hii ni ishara tosha kuwa kuna uhitaji mkubwa  wa kuimarishwa kwa huduma ya usafirishaji ndani ya jiji kukabiliana na ongezeko kubwa la watu katika jiji hili muhimu kibiashara  na kiutawala, kimbilio la kila mtafuta maisha.

Je, Serikali kupitia Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco), Shirika la reli (TRL) hawajaliona hili na kujitanua zaidi kibiashara na kurahisisha huduma?

Masanja Kadogosa ni Kaimu Mkurugenzi wa Rahco, anasema wanajipanga kuhakikisha wanaimarisha usafiri wa treni ndani ya jiji kwa kujenga reli katika maeneo mengi hususani yenye idadi kubwa ya watu.

Anasema tayari wanafanya  upembuzi  yakinifu (feasibility study) za ujenzi wa reli  kwenye  ardhi na anadai kuwa zitajengwa  na kutoa huduma kutoka Bagamoyo Mkoa wa Pwani hadi katikati ya jiji kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA).

Reli nyingine itajengwa kutokea Mbagala hadi mjini na kisha kuelekea Ubungo. Anasema pia kutakuwa na reli itakayojengwa katika maeneo yote yatakayojengwa barabara za mabasi ya mwendo kasi.

Mtaalamu mmoja wa masuala ya usafirishaji ambaye hakutaka yeye mwenyewe wala taasisi yake kutajwa gazetini, anaeleza kuwa wafanyabiashara ya usafirishaji hususan wa mabasi yaendayo mikoani wanaweza kutumia fursa hii kuwekeza badala ya kutegemea usafirishaji wa mabasi pekee ambao hata hivyo umekuwa ukilegelega kwa siku za hivi karibuni.

Anasema ikiwa wafanyabiashara hao wanaweza kumiliki mabasi, wanaweza kubadilisha mtaji huo na kuuingiza katika usafirishaji wa treni.

“Hapa nadhani wanapaswa kubadilika kimtazamo tu wasifanye biashara moja wanaweza kuungana na kuagiza treni, lakini shida ninayoiona wengi wanapenda kufanyabiashara ya mtu mmoja mmoja kwa kutaka kuonekana na kuwa na sifa ya mtu binafsi,” anasema mtaalmu huyo.

Nchi nyingi barani Ulaya na mataifa mengine duniani ikiwamo India zimepiga hatua kubwa katika sekta ya usafirishaji kwa kutumia treni hususani katika miji mikuu na umesaidia kurahisisha huduma na kwa wananchi wake na kupunguza msongamano katika miji mikubwa kutokana na wananchi kuwa na uhakika wa kufika mahali pa kazi kwa wakati.

Unaweza kuona ni kwa namna gani miji imekuwa kama imekusanywa pamoja. Kwa mfano nchini Ujerumani si ajabu kumwona mtu akiishi Bonn na kufanya kazi Hamburg  umbali wa kilomita 373 kutokana na kuwa na uhakika wa usafiri kutokana na kuwapo kwa treni zinazofikia hadi mwendo wa kilomita 300 kwa saa na vilevile kwa Tokyo na Kobe umbali wa kilomita 426 au na Hiroshima umbali wa kilomita 600.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles